Sie sind auf Seite 1von 5

Mambo ya kuzingatiwa na Kamati za Bunge katika kusimamia fedha na Rasilimali za Umma Zitto Kabwe Utangulizi Katika madaraka yote

ambayo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kwa Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63, wajibu wa kuisimamia Serikali ndio wajibu unaoelezea hasa kazi za Kamati za Bunge. Ni kupitia Kamati za Bunge, za kisekta au za mahesabu, Serikali huwajibika kujieleza kinaga ubaga kuhusu mipango yake,kuomba fedha na kuelezea matumizi ya Fedha hizo. Mfumo wa utendaji kazi wa Kamati za Bunge ni mfumo ambao unaweza kuimarisha uwajibikaji nchini na hivyo rasilimali za nchi kutumika vema na kuendeleza wananchi. Mfumo dhaifu wa Kamati za Bunge huipa fursa Serikali kufanya itakavyo na kuimarisha ufisadi kama vile matumizi matumizi mabaya ya madaraka, wizi, udanganyifu,hongo,uzembe uvivu. Mada hii itajikita katika maeneo ya kuzingatia ili kuwezesha Kamati za Bunge kusimamia misingi ya Uwajibikaji na hivyo kuzuia ufisadi na kuelekeza rasilimali za nchi kwenye maeneo ya Maendeleo ya wananchi badala ya anasa na kutajirisha kundi dogo la viongozi.Tutaona majukumu ya Kamati katika kusimamia Fedha za Umma na maeneo muhimu sana ya kuweka kipaumbele katika usimamizi huo. Tutaona changamoto za Kamati na namna ya kuzitatua ili kuwezesha Bunge kutekeleza wajibu wake inavyopasa. UWAJIBIKAJI Demokrasia ya kibunge ni moja ya mfumo wa kutazamana kati ya Tawi la Utendaji (tunaita Serikali), Tawi la Uwakilishi (Bunge) na Tawi la utekelezaji wa Sheria (mahakama). Demokrasia inajumuisha uwajibikaji katika matumizi ya madaraka (McGee, D 2002). Uwajibikaji ni pamoja na kuweka mifumo ya kuwezesha maamuzi kufanyika kwa namna ambayo uadilifu unazingatiwa na kwa ufanisi. Uwajibikaji unapaswa kuhusisha matawi yote ya Serikali na jamii kwa kupitia asasi za kiraia na vyombo vya habari. Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imegawa madaraka kwa Mhimili wa Bunge ambapo majukumu matatu makuu yameainishwa, nayo ni Uwakilishi, Kuisimamia Serikali na Kutunga sheria. Kwa kupitia mambo kama kuuliza maswali kwa mawaziri na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja binafsi,kuwasilisha miswada binafsi na kujadili miswada ya Serikali, hoja ya kuahirisha Bunge nk, Bunge huweza kuifanya Serikali kuwajibika kwayo. Kamati za Bunge mahesabu Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaana Kamati ya Bajeti, ni muundombinu muhimu sana katika kuhakikisha kuwa Serikali inajieleza na kujibu

hoja kuhusu sera zake na namna inavyotekeleza sera hizo, maombi ya fedha na matumizi ya fedha hizo ili kufanikisha sera za Serikali. Uwajibikaji hauna lengo tu la kukamata watu wanaovunja sheria bali unalengo la kuweka mfumo ambapo kila mtu mwenye mamlaka anajibu kwa matendo yake na hata pale asipotenda ikiwa alitakiwa kutenda ( answerable to actions and inactions). Uwajibikaji unajenga tabia ya watu, na hasa watu wenye mamlaka, kuzingatia Katiba, Sheria, kanuni na taratibu katika kufikia maamuzi yao. Iwapo mtu mwenye mamlaka akifanya jambo ambalo hawezi kulitetea mbele ya umma, au analionea aibu kulielezea, ni dalili kubwa kwamba jambo hilo au uamuzi huo unatokana na rushwa. Uwajibikaji unaweza mfumo ambao kila mtu mwenye mamlaka atapaswa kujielezea na kutetea uamuzi wake hadharani. Kwa mfano, Waziri anapochukua uamuzi fulani wa kisera akijua kuwa ni lazima uamuzi ule aujibie maswali ndani ya Bunge, itamfanya Waziri huyo afanye uamuzi mzuri na wenye maslahi kwa Taifa. Lakini kama Waziri huyo anaweza kuwaona wabunge fulani na kuwataka wamlinde kwa uamuzi huo ni dhahiri uamuzi huo ni wa kutilia mashaka maana jambo jema halihitaji kulindwa. Hivyo wakati mwingine uwajibikaji huonekana kufanyika ilhali ufanisi haupo kwani sehemu fulani ya Wabunge inakuwa imeamua kutetea jambo lolote linaloletwa na Waziri aliyezungumza kabla na wabunge. Hii ndio hatari kubwa sana inayokabili mabunge mengi duniani. Wakati kila mwaka Kamati ya Bajeti inapaswa kusimamia uwajibikaji katika mapato ya Serikali (finance bill) na mgawanyo wake (appropriation bill), Kamati za Mahesabu zina wajibu wa kutumia sheria hizo kuhakikisha (i) makusanyo ya fedha hizo yamekusanywa kama ilivyoombwa na kuidhinishwa na Bunge na (ii) Matumizi ya Fedha hizo yamefanyika kama ilivyoidhinishwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for money). KAMATI ZA BUNGE ZA MAHESABU Kamati za Bunge za Mahesabu ni asasi muhimu za Bunge katika kuhakikisha Serikali inawajibika kwa wawakilishi wa wananchi. Majukumu ya kamati hizi yameainishwa na Kanuni za Bunge, nyongeza ya nane. Kama tutakavyoona katika kiambatanisho cha mada hii, majukumu yote yanahusisha kazi iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Nyaraka muhimu na ya kwanza katika kazi za Kamati za kusimamia mahesabu ni Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hivyo Kamati za Bunge za mahesabu na CAG wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mkubwa sana. Ndio maana Bajeti ya CAG inapitishwa na Kamati ya PAC na ikishapitishwa hakuna mamlaka ya kuhoji tena. Vile vile PAC ndio Kamati yenye mamlaka ya kuteua Mkaguzi wa kukagua mahesabu ya Ofisi ya CAG.

Ni wajibu wa Kamati za Bunge za mahesabu kulisaidia Bunge katika kuiwajibisha Serikali. Mara kadhaa kumekuwa na maelezo kwamba kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, hapana. Katika kuisimamia Serikali ndani yake kuna kuna ushauri hivyo ushauri haupaswi kuwekewa mkazo zaidi ya usimamizi. Warasimu wa Serikali wanapenda neno ushauri na kuchukia neno usimamizi. Wabunge hawapaswi kuingia katika mtego wa kazi yao ni kushauri kwani huo ni mtego uliotegwa na warasimu ili kupunguza nguvu ya Bunge. Kazi ya Bunge ni kusimamia Serikali. Kamati za Bunge za mahesabu ndio zenye kubeba mzigo huo mkubwa sana kwa niaba ya Bunge.Hivyo tutaona ni namna gani uadilifu ni jambo la msingi sana katika wajibu huu. Vilevile ndio maana ni rahisi sana kuona Kamati za Mahesabu zikipewa kila aina ya shutuma kutoka kwa wasimamiwa na wakati mwingine kwa kuwatumia baadhi ya Wabunge kwa kujua au kutokujua. Wakati mwingine Kamati za Bunge huambiwa kuangalia mahesabu tu basi. Ni wajibu wa Kamati za Bunge kuangalia mahesabu ya Umma na kuona kama matumizi ya Fedha za Umma yanafanikisha malengo yaliyotarajiwa (performance audit). Itakuwa ni uwendawazimu kwa Kamati kuridhika kwa kuangalia tu mizania ya Serikali au Mashirika ya Umma au Serikali za Mitaa. Kwa mfano ni wajibu wa Kamati kuangalia kama Fedha zilizotolewa kwa ujenzi wa Barabara zimetumika kwa kazi hiyo. Ni wajibu zaidi wa kamati kuangalia kama gharama hiyo iliyotumika kujenga barabara husika ndio gharama halisi na sio kwamba imezidishwa ili kunufaisha watu wachache. Ni wajibu mkubwa zaidi wa kamati kaungalia kama barabara hiyo imejengwa kwa kiwango kinachotakiwa. Hii inaitwa value for money. Katika utendaji wa Kazi hizi ni muhimu na lazima, Kamati za Bunge kutumia kwanza Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hata hivyo Kamati pia zaweza kutumia taarifa kutoka vyanzo vingine mbalimbali kama wananchi na vyombo vya habari katika kufikia malengo ya kuchunguza. Kwa mfano, hivi karibuni moja ya Magazeti hapa nchini (Gazeti la Jamhuri) liliandika kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika Mkutano wa Smart Partnership. Kwamba takribani shilingi bilioni nane zimefanyiwa ufisadi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amenukuliwa akisema kwamba hajapat barua yeyote inayomwomba (CAG haagizwi, anaombwa) kufanya ukaguzi maalumu wa mkutano ule. Kamati ya Bunge ya PAC inaweza kutumia mamlaka yake kumwomba CAG kufanya ukaguzi maalumu na kuwasilisha matokeo yake kwenye Kamati na hatimaye Bungeni. Iliyokuwa Kamati ya POAC ilifanya wajibu huu vizuri sana kwenye suala la nyumba ya Gavana wa Benki Kuu na kutokana na ukaguzi huo hoja ile ilifungwa. Ili kutekeleza wajibu huu muhimu wa uwajibikaji, Kamati za Bunge za mahesabu ni lazima ziwezeshwe vya kutosha kwa mafunzo ya ujuzi (skills) na maarifa

(knowledge). Bila ya kuwa na uelewa mpana wa mambo Kamati hujikuta zikifanya maamuzi ambayo yanakuwa na madhara makubwa kwa Taifa. Katika kutekeleza wajibu, ni muhimu na lazima wajumbe wa Kamati kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani vitendo hivyo huzuia usimamizi na hatimaye kuendeleza rushwa kwa wanaosimamiwa. Uwajibikaji ni silaha dhidi ya rushwa na hivyo wanaosimaima uwajibikaji ni lazima wawe wasafi wao binafsi kwanza kabla ya kusafisha walio wachafu. Uadilifu ni msingi muhimu sana katika kujenga uwajibikaji. Bila ya uadilifu hakuna uwajibikaji na vile vile kukosekana kwa uwajibikaji humomonyoa utamaduni wa uadilifu katika jamii. Mambo gani ya kuzingatia? Tumeona Wajibu wa Kamati katika kusimamia uwajibikaji wa Serikali. Kiambatanisho kimeweka kinabaga ubaga majukumu na wajibu huo. Masuala machache yafuatayo ni ya kuzingatia sana katika utekelezaji wa wajibu huu. Moja, Pamoja na Matumizi yote ya Serikali ambayo Kamati husimamia,kuna matumizi ambayo inabidi kuweka msisitizo maalumu. Moja ya matumizi hayo ni ya Deni la Taifa. Katika Ripoti ya CAG ya mwaka 2012, hoja za kuhusu Deni la Taifa zimeendelea kutokana na kasi ya ongezeko la Deni. Kamati inapaswa kufahamu kwamba Mzigo mkubwa wa Deni la Taifa ni katika kulipa ambapo Fedha nyingi za umma hutumika. Kila mwaka Bajeti ya kuhudumia Deni la Taifa huwa ni moja ya Bajeti kubwa zaidi ya Bajeti nyingine zote. Kwa mfano mwaka 2012/13, Serikali ilitenga takribani shilingi trilioni mbili kuhudumia Deni laTaifa peke yake ilhali robo tu ya fedha hizo ilitengwa kwa ajili ya Wizara ya Afya. Kamati zinapaswa kukagua kwa kina na kila wakati matumizi ya mikopo ili kuhakikisha kwamba mikopo mingi inatumika kujenga uwezo wa nchi kuzalisha rasilimali za kuhudumia mikopo hiyo kwa kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza kodi. Pili, Makusanyo ya Kodi ya Serikali. Bunge hupitisha fedha kuwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi. Hivi sasa ni takribani Watanzania milioni moja tu ndio wanalipa kodi (kwa maana ya watu binafsi walio kwenye mfumo rasmi). Hivyo tuna wigo mdogo sana wa kodi wakati tunatumia fedha nyingi sana kukusanya kodi hiyo kidogo. Ni Wajibu wa Kamati kuona kwamba ufanisi katika kukusanya kodi unafikiwa ikiwemo kwa kiasi kikubwa sana kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, asilimia 15 ya makusanyo tarajiwa huwa hayakusanywi kwenye idara ya Mapato peke yake kutokana na ukwepaji wa Kodi. Hii ni sawa na takribani shilingi 490 bilioni kwa kutumia makadirio ya mwaka wa fedha 2012/13. Wakati Bandari ya Dar es Salaam inapakua makontena 600 kwa siku, kuna wakala wa upakuaji (clearingand forwarding agents) wa idadi hiyo hiyo katika Bandari hiyo. Haiwezekani kuwe na wastani wa kontena moja kwa kila wakala. Eneo hili linahitaji jicho pevu kutoka

kwenye Kamati za Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Ukwepaji kodi wa makampuni ya kimataifa pia ni ajenda kubwa ambayo kila mara kamati inapaswa kuizingatia ili kuzuia. Kamati ya PAC tayari imepitisha pendekezo la ukaguzi wa misamaha ya kodi na kuiweka wazi (audit of tax exemptions and transparency). Ni matarajio kwamba kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni 2013 Watanzania wataona taarfa ya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Tatu, ukaguzi wa mikataba na taratibu za Manunuzi. Hili ni eneo ambalo limekuwa chanzo kikubwa cha ubadhirifu katika nchi yetu. Ni muhimu kila mara kamati kuzinagtia eneo hili katika kazi zake. Eneo hili linaathiri zaidi Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo udokozi imekuwa kama utamaduni na hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ni muhimu Kamati kuhitaji mara kwa mara ukaguzi maalumu kwenye manunuzi ili kujenga uwajibikaji katika eneo hilo na kuepusha hasara kubwa kwa nchi. Nne, hivi sasa nchi yetu imekuwa kitovu cha biashara ya dawa za kulevya. Vijana wa kitanzania wamekuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali duniani wakihusishwa na biashara ya madawa ya kulevya. Moja ya njia ya kupambana na uharamia huu ni uwajibikaji wa mamlaka zenye wajibu wa kupambana na madawa ya kulevya. Hivyo, Kamati za Bunge zihoji katika mahesabu ya mamlaka hizo matumizi ya fedha za umma kupambana na biashara ya madawa ya kulevya ilhali biashara hiyo inazidi kushamiri. Iwapo tutawajibisha Wizara ya mambo ya ndani kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya tutakuwa tumechangia katika vita hii. Hatuwezi kuwa tunatenga fedha kila mwaka dhidi ya biashara hii haramu lakini bado inazidi kushamiri. Kila mwenye wajibu awajibishwe. Mwisho, Ukaguzi wa zoezi la ubinafsishaji. Bado sera ya ubinafshishaji inatekelezwa na Serikali. Ni wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukagua zoezi la ubinafsishaji na Kamati za Bunge kusimamia uwajibikaji katika zoezi hili. Ubinafsishaji ni uuzaji wa mali ya Umma, hivyo ni lazima upate usimamizi kamilifu. Hitimisho Kamati za Bunge za Mahesabu ni asasi muhimu za demokrasia kwani husimamia uwajibikaji. Ni vema kamati hizi kupewa uzito stahili kwa kuwa na rasilimali za kutosha katika kufanya kazi zake na kuhakikisha taarifa zake zinapata uzito katika utekelezaji. Kimsingi Kamati zote za Bunge ni sawa kihadhi lakini Kamati za mahesabu ndio Bunge kiuhalisia.

Das könnte Ihnen auch gefallen