Sie sind auf Seite 1von 13

Hotuba ya kufunga mwaka ya Mhe: Zitto Kabwe (Mb), wakati

wa mkutano wa pamoja wa hadhara na Mwenyekiti wa CUF,


Profesa Ibrahim Lipumba, mjini Mtwara (31/12/2014).

Ndugu Profesa Ibrahimu Lipumba


Mwenyekiti wa Taifa wa CUF,
Ndugu Viongozi mbalimbali mliopo hapa leo,
Ndugu Wananchi

Mtwara Hakiii

Mtwara kuchele? Mtwara kumekucha?

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,


nashukuru sana kwa mwaliko wako kuja kuzungumza na watu wa
Mtwara na kujumuika nao katika kufurahia mafanikio makubwa
waliyoyapata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Nakushukuru kwa kipekee kwa upendo wako kwangu. Umekuwa mlezi


wangu kisiasa na kimaisha. Hata pale nilipopitia mikiki mikiki na
mihemko ya kisiasa, kamwe hukunikatia hukumu, bali uliona namna bora
zaidi ya kunijenga kiuongozi. Wakati baadhi ya watu wakiandikia tanzia
yangu ya kisiasa, uliniita na kufuturu nawe nyumbani kwako ukiwa katika
moja ya sunna zako unazofunga kila wiki. Nakushukuru sana sana, na
ninaomba uendelee kunilea katika maisha yangu ya kisiasa, kifamilia,
kijamii na hata kitaaluma. Ukiwa mbobezi wa kimataifa katika taaluma ya
uchumi nami nafuata nyayo zako, nataka nipite humohumo ulimopita na
inshallah na hata zaidi.

Ndugu wananchi,
Ni kwa sababu ya upendo wa Profesa Lipumba kwangu nilishindwa
kukataa kukubali mwaliko wake kuja hapa kujumuika nanyi katika siku
hii muhimu sana. Hakuna namna bora zaidi ya kushukuru zaidi ya
kuendelea kufanya kazi pamoja katika kuwatetea Watanzania na Tanzania
yetu. Umoja wa upinzani ndio silaha dhidi ya mabwenyenye wa kiuchumi
na kisiasa hapa nchini. Najua huko waliko inawauma sana wanapoona
wapinzani wanaungana bila kujali tofauti ndogondogo zinazojitokeza
miongoni mwao. Tutaendelea kushirikiana kwa maslahi mapana ya nchi
yetu na katika kuhakikisha kwamba utawala wa Chama cha Mapinduzi
ambacho sasa ni chama cha mabwenyenye unakoma katika nchi yetu
mapema iwezekanavyo.

Nimekuja pia Mtwara kwa sababu huu ni Mkoa wa kipekee katika historia
ya nchi yetu. Mtwara ni Mkoa ambao kwa miaka zaidi ya miaka 25 baada
ya nchi yetu kupata uhuru ulibaki kuwa ngome imara dhidi ya mabeberu
wa Kireno na waasi wa nchi jirani ya Msumbiji. Wakati mikoa mingine
ikisonga mbele katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Mikoa ya
Mtwara na Lindi ilibaki nyuma kwa sababu ya kulinda heshima ya mipaka
ya nchi yetu. Hii ni historia muhimu sana ambayo vijana wetu inabidi
waijue na waithamini.
Katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mtwara umechukua sura mpya
kabisa kitaifa kufuatia kugunduliwa kwa gesi. Na katika hili wananchi wa
Mtwara mmeonyesha kwamba watanzania wanaweza kupigania maslahi
ya Taifa wakiamua. Mmesimama kidete kuhakikisha kwamba utajiri huu
hauporwi na kwamba haturudii makosa yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pale
tuliporuhusu madini kuporwa na mabeberu wa kimagharibi kwa msaada
wa mabwenyenye uchwara nchini mwetu. Nyie wananchi wa Mtwara
mmesimama kidete katika kulinda maliasiali hii iliyogunduliwa kwa niaba
ya wananchi wenzenu nchi nzima ya Tanzania.
Najua bado mnalia kuhusu Bomba la kupeleka Gesi Asili Dar es Salaam.
Machozi yenu yatafutika tu kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika
ujenzi wa Bomba hili zimeanza kuchomoza. Kiongozi wa Upinzani
Bungeni ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika
ujenzi wa Bomba la Gesi. Sisi wengine, pale atakapohitaji msaada wetu,
tutamsaidia kwani tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara
mbili na inawezakana kabisa kuwa zaidi ya dola za Marekani 600 milioni
3

zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia Uchina mpaka hapa


Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa tu, kwa uwezo wa mola.
Kwa hiyo kwangu mimi Mtwara ni alama ya harakati za kupigania haki za
wananchi kumiliki, kuendesha na kufaidika na mali asili za Taifa.
Tutaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba utajiri unaoendelea
kugunduliwa hapa Mtwara na Tanzania kwa ujumla unasaidia wananchi
katika kuboresha maisha yao, elimu zao na kumaliza umaskini.
Mimi kama mwana michezo na ambaye napigania maendeleo na
mafanikio ya timu za hapa nyumbani Tanzania, niwapongeze pia wana
Mtwara kwa sababu ya timu yenu ya mpira ya Ndanda FC ambayo imeleta
changamoto sana kwenye maendeleo ya soka nchini kwetu. Napenda
kuitakia kheri timu yenu ya Ndanda FC katika mashindano ya Ligi Kuu ya
Tanzania yanaendelea hivi sasa.

Ndugu Wananchi,
Imekuwa baraka na neema sana kufunga mwaka huu hapa Mtwara, ikiwa
ni alama ya harakati za mapambano dhidi ya mabeberu na vibaraka wao
popote walipo. Mtwara ni uwanja wa mapambano ya uwajibikaji na
demokrasia. Ndio maana nasema imekuwa neema na baraka kufungia
mwaka huu hapa. Kama Mwalimu Nyerere alivyotanagza Azimio la
Arusha mwaka 1967 katika kujenga Nchi ya kijamaa, wana mabadiliko
wote nchini wanapaswa kutangaza Azimio la Mtwara la Uwajibikaji
katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi yetu.
4

Mwaka huu tunaouaga leo ulianza kwa matumaini makubwa sana kwa
Taifa letu katika kupata Katiba Mpya ilitayozamiwa kuweka misingi imara
zaidi ya Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi. Bahati mbaya mwaka
umemalizika kwa kubwaga chini mioyo ya Watanzania wengi sana baada
ya

kupata

Katiba

Inayopendekezwa

yenye

mambo

yale

yale

yaliyotufikisha hapa tulipo zaidi ya nusu karne tangia tupate Uhuru.


Hatutakubali nchi yetu irudi nyuma katika maendeleo ya demokrasia na
kuruhusu watu wachache wapore uhuru wa wananchi kwa maslahi yao na
vyama vyao vilivyogeuka mapango ya uporaji wa mali asili zetu kupitia
mabeberu wa kimagharibi na vibaraka wao. Hatutakubali katiba mpya
kwa jina. Hatutakubali mvinyo huohuo katika chupa mpya na muda
ukifika tutawaambia namna ya kuikataa katiba hii inayopendekezwa.
Busara inataka kura ya maoni ifanyike baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini
wakiileta tukusanye nguvu zetu zote kuikataa Katiba Inayopendekezwa.

Ndugu Wananchi,
Mwaka 2014 unaisha kwa hasira. Tumeshuhudia Bunge letu likijadili moja
ya kashfa kubwa kabisa kupata kutokea katika nchi yetu. Zaidi ya shilingi
Bilioni mia tatu zimechotwa na kugawaiwa kama njugu tena na watu
wenye mamlaka na waliopewa heshima kubwa na umma. Hakuna kashfa
kubwa kama wizi uliofanyika kupitia Akaunti ya Tegeta Esrow. Ni wizi
mkubwa na tumewakamata wezi mchana kweupe kabisa. Nawakikishieni
kwamba juhudi zinazoendelea kufanywa na baadhi ya wezi wa fedha hizi
na vibaraka wao zitashindwa vibaya kwa sababu ukweli haujawahi
5

kushindwa. Watashindwa kwa aibu. Na mimi nawashauri wanyamaze na


wakubali yaishe kwa sababu wataumbuka zaidi wakiendelea na
ujasiriamali wao wa kupika uwongo barabarani.
Kilichofanyika bungeni katika Mkutano wa 16 na 17 uliomalizika mwezi
Novemba mwaka 2014 kimeonyesha namna ambavyo umoja ni nguvu.
Wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao walisimama kidete katika
kuhakikisha kwamba maazimio yaliyopendekezwa na Kamati ya PAC
yanatekelezwa kikamilifu.

Somo moja tunalojifunza ni kwamba tukishirikiana hakuna linaloweza


kushindikana katika kupigania maslahi ya taifa letu pendwa la Tanzania.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni ushahidi tosha wa faida za kushirikiana.
Wananchi pia wameonyesha hasira zao dhidi ya Wizi wa fedha za Umma
kupitia uchaguzi huu.
Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na zilizopaswa kuwa katika akaunti
ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali inasema hazikuwa 306
bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi ni kwamba
hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za
umma na ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha
tozo ya uwekezaji kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma.
Tapeli Harbinder Singh Seth alilipwa hizo zilizokuwemo katika
akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na TANESCO kiasi kwamba shirika
hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu shilingi milioni 400.
6

Kila siku inayokwenda kwa mungu tunamlipa mtu ambaye hajawekeza


hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma kuna
neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni
umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali.
Watu watatu tu ambao ni raia wa kigeni walichora wizi huu kwa miaka
mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin kutoka Malaysia, Bwana
Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na anaishi
Afrika Kusini.
Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana Baharuddin
akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa
kampuni ya PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa
zimezuiwa na Mahakama kwa Bwana Seth wa kampuni PAP.
Mabwana

hawa

wanajua

Watanzania ni mazwazwa

na

hawafanyi

uchunguzi wa kina, yaani due diligence kwani hata kwenye EPA fedha
ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu kinaitwa deed
of assignment.
Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi za umma wana
njaa na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo
ilivyofanyika.
Kama viongozi wetu wangefanya due diligence kwenye manunuzi ya
makampuni haya kama Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka,
tusingekuwa na skandali ya Tegeta Escrow.

Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya malipo kutoka


akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha
zimekwenda benki za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo
zilikwenda kuwalipa mabwana Baharuddin na Issa.
Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha fedha zilizokuwamo
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi wa mahakama ya
kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na zile
za binafsi zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya
kubariki utapeli wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii
ya kimataifa.
Baraza la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari
wameamua na kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo
kutekelezwa na Serikali. Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge,
maana katika maazimio hayo Serikali nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika
kuyandaa na hatimaye kupitishwa na Bunge. Hakuna namna ya kukwepa
kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake; nasema hakuna, ni
utekelezaji tu.

Ndugu Wananchi,
Nataka niwambie watanzania kupitia mkutano huu muhimu wa Mtwara
kwamba yaliyotokea Bungeni ni mwanzo na si mwisho. Ni mwanzo wa
safari ndefu wa kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika nchi yetu.

Dhana ya Uwajibikaji ni dhana inayotaka kila kiongozi kuwajibika kwa


matendo yake katika utekelezaji wa shughuli za umma. Ni dhana ambayo
ni lazima kuienzi kama tunataka nchi yetu ibakie salama na yenye utulivu
kwani kukosekana kwa uwajibikaji kunaleta rushwa na ufisadi. Tusikubali
watu wachache kwa maslahi yao binafsi waendelea kuharibu heshima ya
nchi yetu. Tusikubali kamwe.
Ufisadi unarudisha nyuma maendeleo, unaleta umasikini, unaleta
vita na umwagaji damu. Ndio maana ni lazima kuimarisha taasisi za
uwajibikaji katika nchi yetu. Kufukuza mawaziri wanaposhindwa
kutekeleza wajibu, japo haitoshi, sio udhaifu bali ni mchakato wa
kuimarisha taasisi za Uwajibikaji na kukuza demokrasia kwa ujumla.
Mwalimu Nyerere alituasa kwamba cheo ni dhamana. Ukipewa heshima
ya kuongoza lazima ujiheshimu, ukishindwa kujiheshimu lazima uondoke,
kwa hiari au kwa kulazimishwa.
Waziri Mkuu mstaafu, Mzee wangu, Jaji Joseph Warioba, alipata
kunihadithia alivyojiuzulu wadhifa wake huo mwezi Machi mwaka
1990. Rais Mwinyi alihutubia Taifa kuingia mwaka mpya wa 1990 kwamba
rushwa imeshamiri mpaka muuza njugu anaombwa rushwa. Wizara
takribani nane zikahusishwa na rushwa ikiwamo Wizara ya Sheria
(mahakama), Wizara ya Mambo ya Ndani (uhamiaji na polisi) na Wizara
ya Ardhi.

Mawaziri hawa nane walipaswa kuwajibika kwa kujiuzulu, lakini Mzee


Warioba aliona hiyo ni takribani nusu ya Serikali akamwomba Rais
ajiuzulu yeye ili Serikali mpya iundwe. Baada ya majadiliano marefu Mzee
Mwinyi akakubali na akalitaka Baraza zima la Mawaziri kujiuzulu. Lote
kabisa.
Akaunda upya Serikali, akamrejesha Warioba kama Waziri Mkuu lakini
akaondoa baadhi ya mawaziri. Mwaka 1990 ulikuwa mwaka wa Uchaguzi,
lakini Mzee Mwinyi hakusita kuunda upya Serikali. Maamuzi hayo ndio
yaliyomwingiza kwenye Baraza la Mawaziri ( kama Waziri Kamili) Meja
(wakati huo) Jakaya Mrisho Kikwete ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri yetu.
Hivyo Rais akifanya leo sio jambo jipya. Uwaziri sio usultani, ni dhamana
tu ya kuongoza sehemu ya idara za Serikali.

Ndugu Wananchi,
Ni katika nchi ya Tanzania pekee ambapo waziri anaweza kutukana
wananchi waziwazi mchana kweupe na kuwaambia kwamba ni wajinga
na wapumbavu na akabaki katika ofisi ya Umma. Ni Tanzania tu ndipo
Katibu Mkuu wa Wizara anaweza kutukana wabunge kuwa ni washenzi
akaachwa bila kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Huwezi kuwa na Taifa
lisiloheshimu wananchi na wawakilishi wao. Uwajibikaji ni suluhisho.
Uwajibikaji unaweka nidhamu. Uwajibikaji unatoa matumaini kwa watu
kuwa viongozi wao wanawajali.

10

Mwenyezi Mungu ameweka utajiri wa nchi yetu wa mafuta na gesi asilia


kwenye mikoa ya Pwani na Kusini. Mikoa mingine pia mungu amejaalia
utajiri. Kanda ya Ziwa kuna dhahabu na almasi, nyanda za juu makaa ya
mawe, Kaskazini Mlima Kilimanjaro na Tanzanite na kadhalika. Hata
hivyo katika dhahabu yote iliyochimbwa na kuuzwa nje ya thamani ya
dola za kimarekani bilioni 13 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2013, yaani
miaka 15, nchi yetu ilipata mapato ya dola za Kimarekani 650 milioni tu,
sawa na asilimia tano.
Naomba kurudia. Kwa miaka 15 ambayo dhahabu yetu ilichimbwa na
kuuzwa, Watanzania tumepata shilingi tano tu katika kila shilingi 100 !
Shilingi 95 zote zimekwenda kwa wageni. Kama sio umazwazwa ni nini?

Yote ni kwa sababu ya mikataba ya siri yenye makosa makubwa na yenye


kupendelea wawekezaji. Tunataka mikataba ya gesi iwe wazi kabla ya
uvunaji mkubwa kuanza ili kama kuna makosa turekebishe. Ndiyo maana
Kamati yenu ya PAC iliamuru viongozi wa TPDC waswekwe ndani kwa
kukataa kuweka mikataba hii wazi kwa wajumbe wa Kamati ili
waitathimini kwa niaba ya wananchi.
Hatutaki viongozi ambao kazi yao ni kuombaomba kwa wawekezaji ili
kuwasaidia katika miradi yao ya kisiasa. Tunataka, kwa mfano, mtu kama
DANGOTE anapowekeza hapa Mtwara, watu wa Mtwara na Watanzania
wafaidike na sio wanasiasa. Kuomba omba rushwa kunatia doa heshima
yetu mbele ya mataifa ya ulimwengu.
11

Ndugu Wananchi,
Tunaingia mwaka 2015 kifua mbele katika vita dhidi ya ufisadi na katika
kusimika

uwajibikaji

nchini.

Tunataka

Watanzania

wote

wenye

uzalendo kwa nchi yao kuungana na vyama vya upinzani katika


kuhakikisha uwazi na uwajibikaji nchini kwetu. Kwa upande wa Kamati
ya PAC tunawahakikishia utendaji uliotukuka zaidi. Katika Bunge la
mwezi Januari, mkutano wa 18 moja ya jambo tutakalolitolea taarifa ni
ukwepaji mkubwa wa kodi katika mauzo ya Korosho nje ya nchi, uagizaji
holela wa Sukari na nguo. Fuatilie Bunge hili kwa makini.
Tunautangaza

Mwaka

2015

kuwa

ni mwaka

wa

kuwajibishana.

Uwajibikaji unahitajika zaidi mwaka 2015 kuliko wakati mwingine wowote


katika

miaka

mitano

iliyopita.

Tuungane

kuhakikisha

Serikali

inawajibika kwa wananchi badala ya kuweka mipango ya kuchakachua


uchaguzi.
Lakini nimalizie kwa kusema wazi wazi kwamba kujaribu kuiajibisha
serikali ya CCM kupitia Bunge ni kazi kubwa na ngumu mno. Hawa watu
ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Hawasikii. Hawaoni. Hawaambiliki.
Wameshazibwa mifumo ya fahamu. Hiyo ndiyo hatatari ya rushwa na
ufisadi. Yote tunayoyafanya bungeni na nje ya Bunge kama wapinzani ni
mambo ya muda mfupi. Suluhu ya kudumu ya uwajibikaji kwa serikali ya
CCM mnayo ninyi wananchi. Nami nawaomba mtusaidie muda ukifika
mwakani mchukue HATUA kupitia kura zetu.
12

Hakuna tena muda wa kuwachekea hawa CCM. Tuwaweke pembeni na


hili linawezekana kwa sababu tayari mmeshaonyesha kwamba mnaweza
kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa.
Tunapouanza mwaka mpya, kila mwenye mapenzi ya kweli ya nchi hii
aungane na kufanya kazi pamoja na kwa bidii katika kuijenga Tanzania
bora kwa kila Mtanzania. Tanzania imara, yenye kujali haki na utu wa raia
wake na yenye demokrasia na uwajibikaji inawezekana. Tuchukue hatua
sasa!
Namshukuru tena ndugu yangu, mjomba wangu Profesa Ibrahimu
Lipumba, msomi mwana mapinduzi, kwa fursa hii adimu.

Asanteni sana kwa kunisikiliza

Hakiiii..

13

Das könnte Ihnen auch gefallen