Sie sind auf Seite 1von 5

KAMATI YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) NA JAMII1

Zitto Kabwe, Mb
Mwenyekiti wa PAC, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Utangulizi
Baraza la Wawakilishi kama chombo cha kikatiba cha Kuisimamia na Kuishauri
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limepewa haki na Katiba ya Zanzibar ya
Mwaka 1984 ya kujiunda katika Kamati mbalimbali (Ibara ya 85 ya Katiba ya
Zanzibar). Kamati ya PAC ndio haswa Kamati ya Usimamizi (oversight) wa
Serikali na hivyo kuifanya kuwa Kamati muhimu kuliko Kamati nyingine zote za
Baraza. Wakati Kamati nyingine za Baraza na Baraza kwa ujumla wake hutimiza
wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 88 ya Katiba ya Zanzibar, Kamati ya
Hesabu za Serikali husimamia matumizi yote ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar yaliyoidhinishwa na Baraza na kutoa Taarifa yake kwa Umma. Kwa hiyo
Kamati hii inapaswa kuwezeshwa na kujipambanua vilivyo katika kutekeleza
majukumu yake. Ni muhimu kusisitiza kuwa Kamati nyingine za Baraza ni
muhimu pia katika kusimamia utekelezaji wa Sheria zilizotungwa na Baraza la
Wawakilishi (oversight over execution of laws by ministries and agencies).

Ukaguzi na Kamati

Baraza la Wawakilishi katika mkutano wake wa kila mwaka wa Bajeti hupitisha


mpango wa mapato na matumizi ya Serikali ya Zanzibar. Baada ya makusanyo ya
Mapato hayo na kugawanywa kwa kila Wizara hutumiwa kwa malipo ya

Mjadala katika Semina ya Kamati ya PAC Zanzibar iliyofanyika katika Hotel ya


SeaCliff tarehe 6 Disemba 2014.

huduma, mishahara na miradi ya maendeleo. Mara baada ya kufungwa kwa


mahesabu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hukagua na
kuwasilisha Taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi. Kamati ya PAC sasa
huchukua Taarifa hiyo na kuwahoji kila Katibu Mkuu wa Wizara kuhusu hoja za
ukaguzi. Baada ya kukamilisha Taarifa yake PAC huwasilisha Taarifa hiyo
kwenye Baraza kwa mjadala na kupitisha Maazimio.

Hivyo Ripoti ya CAG ndio nyenzo kuu ya Baraza katika kusimamia fedha za
Umma. Hata hivyo pale ambapo PAC huona inafaa, huweza kuagiza ukaguzi
maalumu kwenye maeneo mahususi. Siku zilizopita nyenzo hii ya ukaguzi
maalumu ilikuwa haitumiki sana. Kutumika kwake hivi sasa ni moja ya
maendeleo ya kiusimamizi katika PAC. Huko Tanzania bara njia hii imekuwa
ikitumika sana hivi sasa na kupitia njia hiyo mambo mengi yameibuliwa kuhusu
matumizi ya fedha za umma.

CAG anatazama mambo mengi kwa wakati mmoja na ndani ya mwaka mmoja.
Hivyo kuna nyakati mkaguzi anakuwa haoni masuala Fulani Fulani mpaka
anapoombwa na vyombo vingine na hata wananchi. Ni vema Kamati ya PAC
Zanzibar kutumia pia njia hii ili kuimarisha usimamizi bora wa fedha za Umma
katika Nchi ya Zanzibar kama ilivyo sasa katika Jamhuri ya Muungano.

Ni muhimu sana kuzingatia kwamba Wawakilishi ndio chombo za mwisho cha


maamuzi kuhusu masuala ya wananchi wa Zanzibar ikiwemo matumizi ya fedha
za umma. Kwa hiyo ni wajibu wa PAC kuhakikisha kuwa Taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inafikishwa Barazani, inajadiliwa na

kuamuliwa.

Muhimu zaidi kuhakikisha kuwa Wizara ya Fedha ya Zanzibar

inajibu hoja za PAC ( treasury notes) na hapo ndipo mzunguko wa uwajibikaji


unakuwa umekamilika (accountability loop). Hata katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wakati mwingine treasury notes hazipewi msukumo wa kutosha na
Wabunge na hivyo kujikuta masuala mengi yanabaki yanaelea bila kumalizwa na
kufanya mfumo wa Uwajibikaji kuwa dhaifu.

Mageuzi muhimu kufanyika

Wakaguzi wa Mahesabu wana chombo chao cha Kimataifa ambacho kinatoa


miongozo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya ukaguzi ( International
Accounting Standards). Hii huwafanya kuleta mabadiliko ya mara kwa mara
katika taaluma yao na kuboresha utendaji wa kazi zao. Siku hizi ukaguzi wa
thamani ya fedha (value for money) hufanywa ili kugundua kama kweli fedha
iliyotumika inaendana na huduma iliyotolewa. Kwa mfano, kama barabara
imejengwa kwa tshs 50 bilioni, wakaguzi sasa wanaweza kuona kama kweli
barabara hiyo ina thamani tajwa.
Kamati ya PAC pia huweza kutembelea miradi kujiridhisha kama taarifa ya
mkaguzi inakubaliana na mradi uliopo. Hata hivyo, Wawakilishi kama ilivyo
Wabunge wanaweza wasiwe na taaluma husika katika jambo linalofanyiwa
ufuatiliaji wa thamani ya fedha. Ni muhimu basi kuwa na mahusiano ya karibu
kati ya CAG na PAC ili lugha ya kikaguzi kuwa ni lugha inayoeleweka kwa
Wawakilishi.
Wawakilishi wanapaswa kuendana na mageuzi ya mara kwa mara katika
ukaguzi na usimamizi wa fedha. Kwa mfano, badala ya kusubiri Taarifa ya

mwaka ya CAG ndio wafanye kazi, PAC yaweza kuona ni jambo gani katika jamii
ambalo linalalamikiwa na wananchi kwamba kuna matumizi mabaya na kuagiza
ukaguzi maalumu katika eneo hilo. Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
mijadala mingi Bungeni yenye hoja kali kali zenye kuleta mabadiliko makubwa
imetokana na ukaguzi maalumu. Hii hoja iliyomalizika katika Mkutano wa Bunge
wa 16 na 17 ( Tegeta Escrow ) ilitokana na habari ya Gazeti la kila siku la The
Citizen. Kutokana na uzito wa hoja hiyo PAC iliagiza ukaguzi maalumu na
hatimaye kuwasilishwa Bungeni.
Mwezi Februari katika Taarifa ya mwaka ya PAC moja ya taarifa
itakayowasilishwa inahusu ukaguzi maalumu kuhusu mchakato wa ubinafsishaji
wa Benki ya Taifa ya Biashara mwaka 2000 na mapitio ya mkataba wa
uendeshaji wa Benki hiyo kati ya mwekazaji kama mwanahisa mmoja na Serikali
kama mwanahisa mwingine.
Mageuzi muhimu sana kufanyika ni hayo, PAC Zanzibar itoke katika kutegemea
tu Taarifa ya mwaka ya CAG na ijielekeze pia katika masuala yanayozungumzwa
na Jamii kuhusu matumizi ya Fedha za Umma.
Eneo lingine la kusisitiza katika mageuzi ni eneo la itikadi za vyama. Iwapo PAC
ikifanya kazi kwa kuegemea itikadi za vyama za wajumbe, kazi ya usimamizi wa
Serikali haitafanyika. Ni vigumu kwa wajumbe kusahau vyama vilivyowaingiza
barazani, lakini ni muhimu wajumbe kufahamu kuwa utendaji mbovu wa Serikali
unaathiri wananchi wote bila kujali itikadi. Kazi za PAC zinakuwa na ufanisi
mkubwa pale ambapo wajumbe wake wanaweka mbele maslahi ya Taifa.
Kwenye Nchi za Jumuiya ya Madola PAC hufanya postmorterm. Kwamba jambo
limekwisha fanywa ndio ukaguzi unafanyika na mjadala kufuata. Kuna haja ya
kutazama upya mfumo huu kwani mara nyingi hausaidii. Ni wakati wa kufikiria

namna ambavyo CAG na PAC wanaweza kutimiza wajibu katika kuzuia matumizi
yanayoelekea kutokuwa na ufanisi. Nchini Ujerumani PAC ni sehemu ya Kamati
ya Bunge ya Bajeti, hivyo inashiriki katika kupitisha Bajeti na kusimamia
utekelezaji wa Bajeti. Pale ambapo PAC inaona kuwa Wizara Fulani katika
mwaka uliotangulia imepata hoja ya ukaguzi katika eneo Fulani, inaweza kuzuia
Bajeti ya item hiyo mpaka CAG aridhie majibu ya hoja ya ukaguzi. Iwapo
Zanzibar itaridhia mfumo kama huu fedha nyingi za Umma zaweza kuokolewa na
Jamhuri ya Muungano yaweza kujifunza baada ya kuona matunda yake Zanzibar.
Hitimisho
Usimamizi ya Fedha za Umma ni jukumu endelevu. Kamati ya PAC inapaswa
kukua kwa kujifunza ukuaji wa sekta ya ukaguzi na vile vile kuangalia
malalamiko ya wananchi. Mageuzi yaliyoainishwa hapo juu ni sehemu tu ya
maeneo ambayo PAC inaweza kutafakari na kufanyia kazi ili kuboresha wajibu
wake.

Das könnte Ihnen auch gefallen