Sie sind auf Seite 1von 102

2

UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:

MAGUFULI VS LOWASSA
3

Kwa Marehemu Mzee Philemon Chahali na marehemu Adelina, wazazi wangu mliotangulia

mbele ya haki wakati ninawahitaji sana. Asanteni kwa kunizaa, kunilea, na kunipa imani ya

kuwa mtu ninayetaka kuwa.


4

FARAHASA

Kuhusu Mwandishi

Shukrani

Utangulizi

SURA YA KWANZA: Historia ya uchaguzi mkuu Tanzania hadi mwaka 200520

SURA YA PILI: Chaguzi za mwaka 2005 na 2010 na msingi wa changamoto zilizopo


katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.29

SURA YA TATU: Mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais...40

SURA YA NNE: Mchakato wa UKAWA kupata mgombea wake wa kiti cha urais...56

SURA YA TANO: Nafasi na vikwazo kwa kila upande.67

SURA YA SITA: Hitimisho...94


5

Kuhusu mwandishi

Mwandishi wa kitabu hiki, Evarist Chahali, ni Mtanzania mwenye makazi yake jijini Glasgow,
Uskochi, na anajitambulisha kama mwanaharakati wa mtandaoni (e-activitist) katika masuala ya
haki za kijamii. Ni mhitimu wa Shahada ya kwanza katika Sosholojia (BA in Sociology) aliyoipata
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, Shahada ya Uzamili katika Stadi za Vita (Master
of Letters in War Studies) na Shahada ya Uzamili katika Utafiti wa Siasa (Master of Research in
Political Research) alizopata katika Chuo Kikuu cha Aberdeen, Uskochi, ambapo bado anaendelea
na Shahada ya Uzamifu katika Stadi za Siasa (PhD in Political Studies Part-Time).

Kwa zaidi ya miaka 10, amekuwa akiandika makala katika magazeti mbalimbali nchini Tanzania,
ambapo huko nyuma aliandikia magazeti ya Kulikoni na Mtanzania, na kwa sasa ni mwandishi
wa makala katika gazeti la kila wiki linaloongoza nchini Tanzania, la Raia Mwema. Kadhalika,
mwandishi anamiliki blogu ya Kulikoni Ughaibuni iliyoanzishwa mwaka 2006.

Awali, mwandishi alikuwa Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Ecknforde, Tanga, Tanzania
kabla ya kujiunga na utumishi serikalini katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri wa Munngano wa
Tanzania. Hivi sasa, licha ya kuendelea na masomo yake ya Shahada ya Uzamifu (part-time)
anajihusisha ushauri wa masuala ya intelijensia (intelligence consultancy).
6

Shukrani

Kitabu hiki kinajadili kwa kina kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini
Tanzania, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Kilichonisukuma kuandikia kitabu
hiki ni pamoja na ukweli kwamba nimekuwa mfuatiliaji wa karibu wa siasa za Tanzania. Licha ya
uandishi wa makala za uchambuzi katika gazeti la kila wiki la Raia Mwema, vilevile nimekuwa
nikiandika masuala mengi kuhusu nchi yetu katika blogu yangu ya Kulikoni Ughaibuni.

Vilevile mimi ni mwanafunzi wa stadi za siasa, na mara zote nimekuwa nikiamini kwamba njia
mwafaka zaidi ya kuitumia elimu yangu ipasavyo ni kuitumikia nchi yangu kwa njia ya maongezi,
aidha kupitia maandishi ya kwenye makala gazetini au bloguni au kwa makala za sauti ninzozitoa
mara kwa mara. Ninasema meongezi kwa vile mimi si mwandishi kitaaluma, na ninajitambulisha
kama mfanya-maongezi (conversationalist) kuliko mwandishi. Kwahiyo, kitabu hiki ni sehemu na
mwendelezo wa maongezi hayo.

Lengo la kitabu hiki si kumshawishi msomaji abadili itikadi yake au mtizamo wake kisiasa bali
kufanya maongezi kuhusu uchaguzi huo muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu. Iwapo maongezi
hayo yatapelekea msomaji kubadili mtizamo wake, itakuwa ni jambo zuri japo si lengo langu.

Kadhalika, kwa muda mrefu nimekuwa nikihubiri umuhimu wa wananchi kutambua fursa yao
katika uongozi wa taifa. Kwa bahati nzuri, kila miaka mitano wananchi wanapata fursa ya
kushirikia katika uongozi huo kwa njia ya kura kwa Rais, wabunge na madiwani, sambamba na
chaguzi za serikali za mitaa zinazojiri katikati ya kipindi hicho.

Licha ya kuwa mwanafunzi wa stadi za siasa, kitabu hiki, kama zilizvyo makala zangu gazetini na
bloguni, sio cha kitaaluma. Ni maongezi kati yangu na Mtanzania wa kawaida, awe mwenye
shahada ya uzamifu kutoka chuo kikuu au mhitimu wa elimu ya msingi. Hii isitafsiriwe kama
kukosa imani katika kujadili masuala mbalimbali kitaaluma bali nimeonelea kuwa ndio njia
mwafaka ya kuongea na watu wengi pasi kuwepo kwa vikwazo vinavyoweza kuwanyima fursa
wenzetu ambao hawakubahatika kielimu. Kitabu hili ni kwa ajili ya kila Mtanzania wa rika lolote,
7

jinsia yoyote na wa kada yoyote mwanasiasa au raia anayeichukia siasa, mama ntilie au
mwanasheria, mwanafunzi au Mwalimu, nk.

Awali, Siku ya Mwaka Mpya, Januari Mosi 2015 niliweka nadhiri ya kuandika vitabu viwili ndani
ya mwaka huu. Hiki cha uchaguzi mkuu na kingine kuhusu fani ya Uafisa Usalama wa Taifa
(ushushushu). Kuhapishwa kwa kitabu hiki ni utekelezaji wa dhamira hiyo, huku kitabu kingine
kikiwa mbioni kuchapishwa hivi karibuni.

Nilianza uandishi wa kitabu hiki mwezi Mei mwaka huu lakini ilinilazimu kusitisha shughuli hiyo
mwezi Julai kufuatia kifo cha baba yangu mpendwa, marehemu Mzee Philemon Chahali, ambaye
pamoja na mkewe, mama yangu mpendwa, marehemu Adelina Mapango, ninawatunuku (dedicate)
kitabu hiki kwao. Japo hampo nasi kimwili, ninaamini kiroho mnafurahishwa na kazi hii yangu
mtoto wenu.

Ninamshukuru dada yangu Mary, na wadogo zangu, Sr Maria-Solana na mapacha Peter na Paul
(Kulwa na Doto) kwa upendo wao ulionisaidia mno kuandika kitabu hiki. Pamoja nao ni binamu
zangu Gordian Mapango, George Mapango na Dignatus Mapango.

Kadhalika, ninatoa shukrani zangu za dhati Christher Mghamba kwa kila aina ya sapoti
aliyonipatia katika uandishi wa kitabu hiki. Kila asubuhi alinikumbusha kutozembea kukamilisha
jukumu hilo, na kila usiku alinibana kujua nimepiga hatua gani. Sambamba nae ni rafiki yangu
wa muda mrefu, Iman Saidi Zangira wa Perth, hapa Uskochi, kwa kila aina ya msaada na msukumo
alionipatia.

Shukrani za kipekee kwa Dokta Joachim Mwami wa Chuo Kikuu cha Umaru Musa Yar Ardua,
Nigeria, ambaye tangu mwanzo aliniunga mkono kuhusu wazo la kuandika kitabu hiki.

Vilevile, ninatoa shukrani nyingi kwa mwanaharakati maarufu nchini Tanzania, Maria Sarungi, na
Mkurugenzi wa Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu, Dkt Mwele Malecela, na Naibu wa
Mwasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, kwa
kunihamasisha kuandika kitabu hiki. Kadhalika, ninawashukuru watu mbalimbali kwenye
mitandao ya kijamii, hususan Twitter na Facebook, kwa kulipokea vema wazo langu la kuandika
8

kitabu hiki na kuonyesha kukisubiri kwa hamu. Hilo lilisaidia kunisukuma kuandika kwa kasi ili
kitabu hiki kichapishwe kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu.

Mapungufu yoyote yaliyomo katika kitabu hiki ni yangu mwenyewe na ninabeba lawama zote.
Kama nilivyotanabaisha hapo juu, mimi si mwandishi kitaaluma. Na pia ninakichukulia kitabu
hiki kama maongezi (conversation) niliyoamua kuyaweka katika maandishi.

Ni matumaini yangu makubwa kuwa licha ya faida tarajiwa kuhusiana na uchaguzi mkuu, kitabu
hiki kitawahamasisha Watanzania wenzangu kuhusu haja ya kuweka fikra au mitizamo yetu katika
maandishi, sambamba na kuendeleza filosofia isiyo rasmi ya sharing is caring.

Ninawatakia usomaji mwema

Evarist Chahali, Glasgow, Uskochi

Oktoba 2015
9

Kwa Marehemu Mzee Philemon Chahali na marehemu Adelina, wazazi wangu mliotangulia
mbele ya haki wakati ninawahitaji sana. Asanteni kwa kunizaa, kunilea, na kunipa imani ya
kuwa mtu ninayetaka kuwa.
10

Utangulizi:

Tarehe 25 Oktoba huu 2015, Watanzania watapiga kura ya kumchagua Rais mpya, atakayemrithi
Rais wa sasa, Jakaya Kikwete. Japo huu si uchaguzi mkuu wa kwanza katika historia ya nchi yetu,
mazingira ya uchaguzi huo na hali halisi ya Tanzania yetu kwa sasa, yanaufanya uwe na umuhimu
wa kipekee.

Kisiasa, angalau kwa chama tawala, CCM, yayumkinika kuhitimisha kuwa uchaguzi mkuu huu ni
wa kwanza kufanyika ambapo nguvu za Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere,
hazipo moja kwa moja (directly). Mara baada ya kungatua, Nyerere alimteua Ali Hassan
Mwinyi kuwa Rais, akitumia nafasi yake kama mwanasiasa mwenye nguvu zaidi nchini Tanzania.
Baada ya Rais Mwinyi kumaliza mihula yake mawili mwaka 1995, Nyerere alitumia tena nguvu
zake kisiasa na kuwezesha msaidizi wake wa zamani, Benjamin Mkapa kupitishwa na CCM, na
hatimaye kushinda urais, madaraka aliyoshikilia kwa mihula mawili, kama mtangulizi wake, yaani
Rais Mwinyi.

Hata hivyo, duru za kisiasa zinaelezwa kuwa nguvu ya kisiasa aliyotumia Nyerere kumpitisha
Mkapa iliwaathiri wanasiasa wawili vijana, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, ambao miaka 10
baadaye, walifanikiwa kmwingiza mmoja wao Ikulu.

Kwahiyo japo Nyerere hakuwa hai wakati Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, safari yake
ya kuingiza Ikulu ilicheleweshwa kwa miaka 10 na nguvu za kisiasa za Nyerere. Kadhalika,
kushinda urais kwa Kikwete akisaidiwa na rafiki yake Lowassa mwaka huo kulitazamwa kama
manufaa ya kutokuwepo Nyerere.

Mwaka 2010, Kikwete alishinda tena urais, kama ilivyo kanuni isiyo rasmi ndani ya chama tawala
CCM kwa rais aliye madarakani kuruhusiwa kumaliza mihula miwili. Kwahiyo, hata kama
nguvu za Nyerere zilikuwepo wakati huo bado zisingemzuwia Kikwete kushinda tena.

Katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya urais mwaka huu hali ni tofauti kabisa. Nguvu za
Nyerere zinaonekana kuondoka kabisa. Hata wanasiasa waliokuwa waamini wa itikadi zake, kwa
11

mfano mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, wamekuwa na mtizamo tofauti. Jina la Nyerere
limebaki kama heshima tu lakini lisilo na uwezo wa kubadili chochote ndani ya CCM.

Lakini, tukiacha kumhusisha Nyerere, mwaka huu kinyanganyiro cha kumpata mgombea wa
CCM katika nafasi ya urais kimeweka historia mpya, ambapo makada zaidi ya 40 walijitokeza
kuwania kuteuliwa. Kuna waliotafsiri iwngi huo ya idadi ya watangaza nia kama kukua kwa
demokrasia ndani ya chama hicho, huku wengine wakieleza kuwa wingi huo ni ishara ya uchu wa
madaraka, na wengine wakienda mbali zaidi na kudai kuwa rais Kikwete ameishusha hadhi ya
urais kiasi kwamba kila Dick, Tom na Harry alidhani anaweza kuwa Rais.

Kwa mara ya kwanza, CCM na Watanzania walishuhudia kampeni zisizo rasmi za makada
waliotangaza nia za kuomba kupitishwa na CCM kugombea urais. Kampeni hizo zilikuwa kali,
kana kwamba ni kampeni rasmi za kuwania urais. Iwapo ukali wa mchuano huo ulipelekea chama
hicho kupata mgombea bora au la, ni suala la muda.

Jingine kisiasa, ni athari za mchakato wa CCM kupata mgombea wake, ambapo jina la Waziri
Mkuu Mstaafu Lowassa halikupitishwa, na hatimaye akaamua kuhama chama hicho na kujiunga
na chama cha upinzani, Chadema. Kuhama kwa Lowassa kutabaki kuwa moja ya kumbukumbu
muhimu za uchaguzi huu. Japo kinyume na ilivyotarajiwa kuwa kuhama kwake kungeambatana
na kuhama kwa wanasiasa wengi wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono, ukweli tu kuwa
mwanasiasa huyo ambaye kura mbalimbali za maoni zilimwonyesha akiongoza kwenye
uwezekano wa kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho, kuamua kujiondoa katika chama
tawala si jambo dogo hata chembe.

Na baadaye, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye naye alitangaza kujiunga na Upinzani, na
kuweka historia mpya ya mawaziri wakuu wa zamani kuhama CCM na kujiunga na Upinzani.

Uamuzi wa Lowassa kuhamia Chadema, ambayo awali ilifikia maafikiano ya kusimamisha


mgombea mmoja wa urais na vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na NLD ambavyo kwa pamoja
vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), na kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa
tiketi ya UKAWA kumebadili kabisa mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Yayumkinika
kuhitimisha kuwa kwa mara ya kwanza kabisa, vyama vya upinzani, hususan vinavyounda
12

UKAWA, na wanachama wake, wanaonekana kuwa na matumaini makubwa ya kuingoa CCM


madarakani. Kwamba matumaini hayo yana uzito au la, itajadiliwa katika sura inayojadili nafasi
ya Lowassa katika uchaguzi huo.

Lakini eneo jingine linachoufanya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa tofauti na chaguzi
zilizotangulia ni matumizi ya teknolojia ya kisasa, hususan mitandao ya kijamii. Kama ilivyokuwa
wakati CCM inafanya mchakato wa kupata mgombea wake wa tiketi ya urais, ambapo watangaza
nia mbalimbali walijiunga na mitandao ya kijamii na baadhi yao kufanya kampeni za waziwazi,
kampeni zinazoendelea kati ya CCM na UKAWA zimetawala mno katika mitandao mbalimbali
ya kijamii, hususan Twitter, Facebook, Instagram na kwenye blogu. Kadhalika, teknolojia ya
mawasiliano ya kutumiana ujumbe, hususan Whatsapp, imekuwa nyenzo kubwa ya ushirikishwaji
wa umma katika siasa zinazohusiana na uchaguzi huo. Yayumkinika kuhitimisha kuwa huu
utakuwa uchaguzi mkuu wa kwanza ambapo teknolojia ya kisasa imekuwa na nafasi kubwa,
kulinganisha na chaguzi zilizotangulia.

Matumizi ya teknolojia hayajaishia kwenye kampeni tu bali pia hata shughuli nyingine
zinazohusiana na uchaguzi huo na siasa za Tanzania kwa ujumla. Kwa mfano, wakati ninaandika
paragrafu hii, kuna majadala kuhusu hatma ya nchi unaoendelea jijini Dar es Salaam, nami
niliyepo Glasgow, hapa Uingereza ninaufatilia live. Japo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania,
raia wa nchi hiyo walio nje hawaruhusiwi kupira kura, ukweli kwamba baadhi yao ni washiriki
muhimu katika mijadala mbalimbali ya mustakabali wa taifa unaweza kuwa na nafasi katika
ushawishi wa kisiasa.

Lakini tukiweka kando mazingira hayo ya kisiasa na kiteknolojia, uchaguzi mkuu wa mwaka huu
una umuhimu mkubwa kwa kila Mtanzania, hasa kwa kuzingatia hali halisi iliyopo nchini. Pamoja
na taarifa mbalimbali zinazoashiria kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi, mamilioni
ya Watanzania bado ni masikini mno. Na kana kwamba hiyo haitoshi, pengo kati ya wenye nacho
na wasio nacho linazidi kuongezeka.

Kibaya zaidi, kadri pengo hilo linavyozidi kukua ndivyo hisia miongoni mwa wasio nacho kuwa
wengi wa wenye nacho ni mafisadi. Kwa lugha nyingine, kwa kiasi kikubwa, utajiri nchini
13

Tanzania umekuwa ukiangaliwa kwa jicho la mashaka. Hisia hizi zinaathiri umuhimu wa watu
kujituma na pengine kuweza kuingiza kwenye kundi la wenye nacho.

Wakati hakujawahi kutolewa maelezo ya kueleweka kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri
mkubwa wa raslimali ilionao, yayumkinika kuhitimisha kuwa ufisadi ni moja ya sababu ambazo
sio tu zinachangia umasikini wa nchi wa nchi yetu bali pia unazidisha hali hiyo. Kwahiyo moja ya
changamoto kwa serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana kwa dhati na ufisadi. Suala hilo
litajadiliwa kwa undani katika sura zinazojadili changamoto zinazoikabili CCM na UKAWA.

Suala la kukosekana maelezo kuhusu umasikini unaoikabili nchi yetu lipo pia katika hisia kuhusu
mafanikio ya watu binafsi. Kama kuna wahanga wakubwa wa hisia hizo basi ni wasanii, ambapo
msanii akifanikiwa katika kazi zake, zinasikika tetesi kuwa ni muumini wa kundi la Freemason.
Kama ilivyo kwa wengi wa wanasiasa wetu kutanabaisha bayana kwanini nchi yetu ni masikini
ndivyo ambavyo baadhi ya wananchi wanashindwa kuelewa kwamba inawezekana kwa mtu kuwa
na mafanikio pasipo kujihusisha na ufisadi au kuwa Freemason.

Lakini licha ya umasikini mkubwa unaowakabili Watanzania wengi, ambao kwa mtizamo wangu
ninaamini unachangiwa zaidi na ufisadi, nchi yetu pia inakabiliwa na matatizo mengine lukuki,
ikiwa ni pamoja na tatizo sugu la nishati isiyo na uhakika kutokana na mgao wa kudumu wa
umeme. Matatizo mengine ni pamoja na ukosefu wa ajira, ambapo idadi kubwa ya wahitihimu
hukumbana na soko la ajira lisilowahitaji, matatizo kwenye sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na
miundombinu duni ya elimu na walimu kucheleweshewa mishahara yao. Kadhalika, meoneo
mengi ya Tanzania bado yanakabiliwa na tatizo la huduma ya uhakika ya maji, huku sekta ya afya
nayo ikiwa na matatizo mengi.

Uhalifu pia umezidi kuwa tatizo kwa Tanzania yetu huku biashara ya madawa ya kulevya
ikishamiri mno kiasi cha kudhani mihadarati ni miongoni mwa exports muhimu kwa nchi yetu.
Vita dhidi ya madawa ya kulevya inakwazwa sio tu na viongozi wa serikali na wanasiasa kwa
kutochukua hatua dhidi ya wahusika bali pia mtizamo wa jamii kwa wahusika ni wa kuwatukuza
zaidi (kwa mfano kuwapamba kwa jina la wazungu wa unga badala ya wahalifu).
14

Sambamba na tatizo la madawa ya kulevya ni ujangili ambao umechangia sana kuchafua taswira
ya nchi yetu kimataifa. Mabadiliko ya mara kwa mara ya mawaziri wanaoongoza Wizara na idara
zenye dhamana ya maliasili yameshindwa kabisa japo kupunguza tatizo hilo.

Tatizo jingine linalohusiana na uhalifu ni biashara ya kuchukiza inayohusisha viungo vya watu
wenye ulemavu wa ualbino. Kama kuna kitu ambacho kinaichafua mno Tanzania kwa sasa ni
kuhusu biashara hiyo ambapo vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vimemfanya vipindi
maalumu kuelezea kuhusu tatizo hilo. Tatizo hilo linachangiwa zaidi na ukweli kuwa imani za
ushirikina zimeota mizizi mno katika nchi yetu, na hakuna jitihada za dhati kukabiliana nalo.

Kuna baadhi ya wananchi wanaongea kwa mzaha kuwa shughuli pekee inayolipa, yaani yenye
faida, katika nchi yetu ni uhalifu. Licha ya biashara ya madawa ya kulevya na ujangili, nchi yetu
pia inakabiliwa na matatizo ya utakasishaji fedha sambamba na biashara ya kusafirisha binadamu
isivyo halali (human trafficking).

Kwa upande wa umoja wa kitaifa, kusuasua katika kuyashughulikia matatizo yanayoikabili


muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kumeendelea kuweka muungano huo katika hali ya
hatihati. Na katika suala hili la muungano, uchaguzi huu unaweza kuwa kama referendum kwani
wakati CCM ikibainisha katika ilani yake ya uchaguzi kuwa itaendelea kudumisha muundo uliopo
wa serikali mbili, UKAWA wameweka wazi kwamba miongoni mwa vipaumbele vyao ni muundo
wa serikali tatu kama ulivyopendekezwa na Tume ya kupokea maoni kuhusu Katiba Mpya,
maarufu kama Tume ya Warioba. Kwahiyo hatma ya muundo wa muungano uliopo itategemea
chama gani kitakachoshinda kati ya CCM na UKAWA.

Lakini moja ya vichocheo vya kuporomoka kwa umoja wa kitaifa ni kupunguza kwa kasi kwa
uzalendo. Ni wazi kwamba ni vigumu kwa uzalendo kushamiri kwenye jamii yenye pengo
linalozidi kukua kati ya wenye nacho na wasio nacho. Kwa bahati mbaya au makusudi,
programu za miaka ya nyuma zilizochangia kukuza uzalendo kama vile wahitimu kujiunga na
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria zimekuwa za kusuasua.

Umoja wetu kitaifa unahatarishwa pia na tatizo linalozidi kukua pasipo kushughulikiwa ipasavyo
la migogoro ya kidini. Kubwa zaidi katika tatizo hili ni malalamiko ya muda mrefu ya Waislam
15

kuwa wenzao Wakristo wanapendelewa na serikali. Japo katika siku za hivi karibuni tatizo hili
limekuwa kimya, ukweli mchungu ni kwamba bado lipo na kuna uwezekano wa kuibuka tena huko
mbeleni. Wakati Awamu zilizotangulia ziliamua kulikwepa tatizo hilo kwa kutolizungumzia
waziwazi, ilani ya uchaguzi ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ilibainisha wazi
dhamira yake ya kushughulikia kero za Waislamu, na kuahidi kuwa ingewapatia Mahakama za
Kadhi. Hata hivyo, ahadi hiyo imeendelea kuwa ahadi tu na haijatekelezwa hadi muda huu. Ni
wazi kwamba suala hili litajitokeza tena huko mbeleni.

Kushamiri kwa udini pia kumechangia kuathiri umoja wa kitaifa. Udini hujitokeza katika sura
tofauti, na mfano mmojawapo ni hiyo ahadi ya CCM mwaka 2005 kuwa ingewapatia Waislamu
mahakama za kadhi, lengo likiwa ni kuvuta kura za waamini wa dini hiyo. Uchaguzi Mkuu
uliopita, mwaka 2010, ulishuhudia udini ukitumika tena kama turufu ya kisiasa, ambapo wanasiasa
mbalimbali wa CCM waliojaribu kujenga picha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,
Dokta Willbrod Slaa ni padri anayewakilisha Kanisa, na hafai kuwa rais. Mbinu chafu kama hiyo
iliwahi kutumika kwenye chaguzi za nyuma dhidi ya chama cha CUF ambapo zilifanyika jitihada
za kujenga picha kuwa chama hicho ni cha kidini, cha Kiislamu.

Tofauti za kiitikadi zimeendelea kuchangia mpasuko katika nchi yetu ambapo baadhi ya viongozi
wa ngazi za juu wa chama tawala wamekuwa weakifanya jitihada za waziwazi kujenga taswira
potofu kuwa vyama vya upinzani ni kama taasisi za kihaini. Tumeshuhudia huko nyumba jinsi
baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema walivyonyanyaswa na vyombo vya dola kwa
tuhuma za ugaidi. Kumekuwa na jitihada kubwa za kuwaaminisha Watanzania kuwa Wapinzani
si Watanzania kamili na hawaitakii mema nchi yetu.

Kingine kinachoweza kuingizwa katika kipengele hiki cha mmomonyoko wa umoja wetu wa
kitaifa ni mtizamo fyongo miongoni mwa wanasiasa na wananchi wa kawaida dhidi ya Watanzania
wenzao walio nje ya nchi kwa sababu moja au nyingine. Kama kuna kipindi hali hii ilijiweka
bayana zaidi basi ni wakati wa mjadala kwenye Bunge Maalum la Katiba ambapo suala la uraia
pacha liliigawa jamii, huku wengi wakiwaangalia Watanzania waliopo nje kama wenye
mapungufu katika sifa za utaifa, au kwa lugha nyepesi Watanzania nusu, kwa maana kuwa sio
kamili. Mchango wa Watanzania walio nje, au Diaspora kama inavyohamika, umekuwa
16

ukipuuzwa kwa hoja mbalimbali, kubwa ikiwa ni tishio kwa usalama wa taifa letu, kana kwamba
matishio yaliyopo yamechangiwa na watu wa Diaspora.

Rekodi ya Tanzania katika kuheshimu haki za binadamu sio ya kupendeza hata kidogo. Vyombo
vya dola, hususan Jeshi letu la Polisi, vimekuwa mstari wa mbele katika kutoheshimu haki za
binadamu. Licha ya suala hili kuchangia katika kumomonyoa umoja wetu kitaifa ambapo mara
nyingi wahanga wakubwa wamekuwa viongozi na wachama wa vyama vya upinzani, pia linaathiri
sana imani ya Watanzania wengi kwa vyombo vyao vya dola. Yayumkinika kuamini kuwa laiti
nguvu inayotumiwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti maandamano halali ya vyama vya upinzani,
kwa mfano, ingeelekezwa katika kukabili uhalifu, basi tatizo hilo lingepungua kwa kiasi kikubwa.

Kimataifa, Tanzania ya zama za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na hii ya leo ni vitu viwili
tofauti. Wakati nchi yetu sio tu ilikuwa miongoni mwa wapiganiaji wa umoja na ushirikiano katika
Bara la Afrika lakini pia ilishiriki katika mapambano ya ukombozi kusini mwa bara hilo, kwa sasa
ni vigumu kuielewa seraya nje ya Tanzania, kama ipo. Japo bado tumeendelea kuwa na mchango
katika utatuzi wa migogoro kwa nchi jirani, kwa mfano huko Burundi, sambamba na kuchangia
harakati za kimataifa katika utatuzi wa migogoro, kwa mfano uwepo wa majeshi yetu nchini
D.R.C, hatujaweza kurudi kwenye ramani ya kimataifa kama ilivyokuwa zama za Nyerere, na
tatizo kubwa limekuwa kutokuwa na msimamo imara.

Uwepo wetu katika eneo la Maziwa Makuu na hali ya mashaka inayotawala katika eneo hilo
inatupasa kutukumbusha umuhimu wa kujiimarisha kiulinzi na kiusalama, sambamba na
kudumisha amani yetu kwa kuzingatia kuwa hatuna pa kukimbilia. Kumekuwa na shutuma
nyingi dhidi ya taasisi muhimu kwa usalama wa taifa letu, yaani Idara ya Usalama wa Taifa.
Kisiasa, taasisi hiyo imekuwa ikituhumiwa kutekeleza majukumu yake kana kwamba ni kitengo
cha usalama cha chama tawala. Lakini shutuma kubwa kwa Idara hiyo ni jinsi inavyoonekana
kushindwa kukabiliana na matishio kadhaa ya usalama kama vile ufisadi. Uimara wa taasisi hiyo
ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu kwa sababu uimara wa ndani ndio unaowezesha
kukabiliana vizuri na matishio kutoka nje ya nchi.
17

Moja ya changamoto zitakazomkabili rais ajaye ni kuyumba kwa thamani ya sarafu yetu. Kwa
kuzingatia kuwa uchumi wetu unategemea sana misaada ya nchi kama China, ambayo wakati
ninaandika kitabu hiki ipo kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi baada ya soko lake la hisa
kuyumba, itamlazimu rais ajaye kuwa na mikakati imara ya kuinusuru sarafu yetu. Kwa bahati
mbaya au makusudi, hadi wakati huu kampeni za vyma vikuu, yaani CCM na UKAWA, zimelipa
kisogo suala hilo muhimu.

Ni vigumu kuorodhesha matatizo yote tuliyonayo (yanahitaji kitabu kizima) lakini kilicho wazi ni
kwamba uchaguzi huu ni fursa muhimu kwa Watanzania kuboresha mazingira ya safari ya
kuifikisha nchi yetu mahala inapostahili kuwa. Hatuwezi kuendelea kuwa masikini wa kutupa licha
ya utajiri lukuki tulionao.

Japo kitabu hiki kinazungumzia vyama vikuu viwili, yaani CCM na UKAWA, malengo na
matumaini yangu ni kwamba sio tu kuwa kitawanufaisha wasomaji kufanya maamuzi sahihi bila
kujali mtizamo yao kiitikadi bali pia ninatarajia kitawasaidia wapigakura kuwapima wagombea
katika nafasi za ubunge na udiwani kwa kuzingatia changamoto zinazolikabili taifa letu.

Kitabu hiki kina sura sita. Sura ya kwanza inazungumzia historia ya uchaguzi mkuu nchini
Tanzania hadi mwaka 2005, mkazo ukiwa katika zama za mfumo wa chama kimoja hadi kuingia
kwa siasa za vyama vingi. Kadhalika, sura hii inaangalia masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika
Awamu tatu za Urais zilizotangulia, ya Kwanza (ya Nyerere), ya Pili (ya Mwinyi), na ya Tatu (ya
Mkapa). Licha ya kupata picha ya chaguzi kuu zilizopita, mjadala kuhusu Awamu ya kwanza hadi
ya Nne unalenga kutoa mwangaza wa changamoto zilizoikabili Awamu ya Nne ya Rais Kikwete
na zinazoikabili serikali ya Awamu ya Tano itakayopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
huu. Kadhalika, mazingira ya baadhi za chaguzi zilizopita yanajadiliwa ili kutoa fursa ya kuangalia
chama gani kinaweza kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Sura ya pili inajalidili mazingira ya utawala wa Rais Kikwete ulivyongia madarakani, na kupigia
mstari ushindani uliogubika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais kwa
ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Imelazimu kuijadili Awamu hii peke yake, yani bila
kuichanganya na Awamu tatu zilizoitangulia, kwa sababu mbalimbali. Moja ya sababu hizo ni
18

ukweli kwamba uchaguzi wa mwaka huu utafanyika wakati Awamu ya Nne ikiwa madarakani.
Wakati kampeni za CCM zinatarajiwa kutumia rekodi ya utendaji wa Awamu ya Nne ambayo
mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Magufuli, alikuwa waziri, UKAWA pia
wanatarajiwa kutumia mapungufu yaliyojitokeza katika utendaji wa Awamu ya Nne (na zilizopita)
ili kuwashawishi wapigakura wasiirejeshe CCM madarakani na badala yake kuwapa fursa wao
(UKAWA).

Kadhalika, mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa, alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza
katika Awamu ya Nne, na hatimaye kulazimika kujiuzulu baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge
kumhusisha na ufisadi wa mradi wa umeme, skandali iliyofahamika kama ya Richmond. Tangu
Lowassa ajiunge na Chadema, na hatimaye kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, skandali
ya Richmond imekuwa hoja muhimu kwa CCM na hata wananchi wasiofungamana na chama
chochote, ikitumika kama kigezo kuwa "Lowassa hafai kuchaguliwa kuwa rais wa Awamu ya
Tano."

Kadhalika, Lowassa alikuwa mmoja wa waliotajwa katika orodha ya watuhumiwa wa ufisadi,


iliyojulikana kama List of Shame. Chadema ndio waliotangaza orodha hiyo, na tangu wakati huo
Lowassa alikuwa mlengwa mkubwa wa shutuma dhidi ya ufisadi kutoka kwa chama hicho.
Kuingia kwake katika chama hicho, na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya
UKAWA, kumechanganya mno mambo, hasa kwa vile licha ya chama hicho kunadi sera zake,
kimejikuta kinalazimika pia kufanya jitihada za kumsafisha Lowassa ambaye alichafuliwa kwa
muda mrefu na chama hichohicho. Kadhalika, ujio wa Lowassa umepelekea sintofahamu ndani
ya UKAWA ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alijiuzulu, na
Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Slaa kuamua kujitenga na shughuli za chama hicho.

Sura ya tatu inajadili mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, huku ikirejea matukio muhimu
yaliyojitokeza katika mchuano huo ulioshuhudia makada zaidi ya 40 wakitangaza nia ya kuwania
kumrithi Rais Kikwete. Kadhalika, sura hii inagusia pia tukio la jina la Lowassa kutopitishwa na
uamuzi wake wa kuhama chama hicho tawala na hatimaye kujiunga na Chadema, kabla ya
kutangazwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA.
19

Sura ya nne inajadili mchakato wa UKAWA kumpata mgombea wake, kubwa zaidi likiwa tukio
la Lowassa kujiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA,
sambamba na kujiuzulu kwa Prof Lipumba na Dkt Slaa kujitenga na shughuli za siasa. Kadhalika,
sura hii inaangalia shutuma nzito alizotoa Dkt Slaa dhidi ya Lowassa, wiki moja baada ya
muungano huo wa vyama kuzindua rasmi kampeni zake jijini Dar es Salaam.

Sura ya tano inajikita katika uchambuzi wa nafasi na vikwazo kwa Mgufuli na CCM, kwa upande
mmoja, na Lowassa na UKAWA, kwa upande mwingine.

Sura ya sita na ya mwisho ni hitimisho, ambapo kwa kuzingatia yaliyojadiliwa kwenye sura tano
zilizotangulia, kunafanyika tathmini ya jumla kwa wagombea hali wawili na vyama vyao,
kuangalia yupi kati yao ana nafasi bora zaidi ya ushindi. Kadhalika, sura hiyo inachambua
changamoto mbalimbali zinazokikabili kila chama na Tanzania yetu kwa ujumla.
20

SURA YA KWANZA: Historia ya uchaguzi mkuu Tanzania hadi mwaka 2005

Tanzania ina historia ndefu ya uchaguzi mkuu, kabla na baada ya uhuru. Historia hiyo yaweza
kugawanywa katika makundi makuu mwili : kabla uhuru (zama za Tangayika wakati nchi yetu
ikiwa chini ya utawala wa mkoloni) na baada ya uhuru ambapo baadaye mwaka 1964 Tanganyika
iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyonayo sasa.

Kadhalika, baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, historia ya uchaguzi mkuu yaweza kugawanywa
katika makundi mengine mawili, yaani chaguzi zilizofanyika katika mfumo wa chama kimoja,
kuanzia zama za TANU na ASP kabla ya vyama hivyo kuungana mwaka 1977 na kuunda CCM,
na chaguzi zilizofanyika baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa wa 14 katika historia ya taifa letu. Uchaguzi mkuu wa
kwanza ulifanyika mwaka 1958, wakati Tanganyika ikiwa koloni la Uingereza. Katika uchaguzi
huo, licha ya masharti yaliyowekwa na serikali ya mkoloni, ikiwa ni pamoja na wapigakura
kutakiwa kuwapigia kura wagombea kutoka kundi la Waafrika, Wahindi na Wazungu, chama cha
TANU kiliibuka na ushindi mkubwa na kuzoa viti 28 kati ya 30 vilivyokuwa vikishindaniwa.
Miaka miwili baadaye, kulifanyika uchaguzi wa wabunge, na TANU ikazoa viti 70 kati ya 71
vilivyokuwa vikishindaniwa.

Baada ya uhuru mwaka 1961, Tanganyika ilifanya uchaguzi mwingine mwaka 1962 baada ya
kuwa jamhuri, ambapo TANU ilishinda tena na Nyerere kuchaguliwa rasmi kuwa rais. Chaguzi
nyingine zilizofanyika mwaka 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na 1990 ziliendelea kuwa ndani ya
mfumo wa chama kimoja.

Hadi anastaafu mwaka 1985, Nyerere alisimama kama mgombea pekee katika chaguzi hizo na
kupita bila kupingwa, hali iliyoendelea katika utawala wa mtangulizi wake, Rais Mwinyi katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo 1985 na mwaka 1990. Mabadiliko ya sheria mwaka 1992
yaliyoruhusu siasa za mfumo wa vyama vingi sio tu yalimaanisha CCM kupambana na wagombea
wa vyama vingine vya siasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, bali pia yalishuhudia chama
21

hicho tawala kikiruhusu makada wake mbalimbali kuwania kuteuliwa kugombea nafasi ya urais
kwa tiketi ya chama hicho.

Licha ya Nyerere kustaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi, mwanasiasa huyo aliendelea
kuwa na nguvu kubwa ndani ya CCM, ingawaje taratibu nguvu hiyo ilianza kumomonyoka, na
hadi alipofariki mwaka 1999, CCM aliyoshiriki kuiasisi ilifanya mabadiliko kadhaa huku Nyerere
akiyashuhudia na kushindwa kuyazuwia. Kubwa katika hayo ni kile kinachofahamika kama
Azimio la Zanzibar,ambalo wachambuzi wa siasa wanalitafisiri kama ndio lililoua rasmi itikadi ya
Ujamaa.

Nguvu za kisiasa za Nyerere ndani ya CCM zilikuwa na mchango mkubwa sana katika chama
hicho kumpata mgombea wake wa kwanza wa kiti cha urais ndani ya mfumo wa vyama vingi,
mwaka 1995, ambapo kwa upande mmoja, Nyerere aliwezesha kada chaguo lake, Mkapa,
kushinda katika mchujo kwenye vikao vya chama hicho, na kwa upande mwingine,
kuwakwamisha makada wawili, Kikwete na Lowassa, waliokuwa wakijulikana kama 'Boyz II
Men.'

Lakini pengine kwa kutambua kuwa nguvu za Nyerere zisingedumu milele, na hasa ikizingatiwa
kuwa hata wakati huo wa mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, tayari zilishaanza
kuonyesha dalili za kupungua (kwa kuzingatia mafanikio ya Azimio la Zanzibar kuua Azimio
la Arusha na itikadi ya Ujamaa kwa ujumla), inaelezwa kuwa Kikwete na Lowassa (na baadaye
kwa kushirikiana na kada mwingine wa chama hicho, Rostam Aziz) waliunda mkakati wa muda
mrefu ambao hatimaye ulifanikisha mmoja wao (Kikwete) kuingiza madarakani.

Pamoja na mazuri mengi aliyefanya Nyerere kwa taifa na chama chake, moja ya mapungufu
makubwa wakati wa utawala wake ni kutoandaa wanasiasa wa kumrithi. Wakati kwa upande
mmoja hali hiyo ilichangia nguvu zake kupungua mara baada ya kustaafu mwaka 1985 kwa vile
kwa kiasi kikubwa hakukuwa na mwanasiasa wa kusimamia misingi aliyoijenga, kifo chake
mwaka 1999 sio tu kiliachia taifa ombwe la uongozi bali pia kiliiathiri CCM kwa tatizo hilohilo.

Mtangulizi wake, Mwinyi, alikumbana na mtihani wa kwanza kwa kuruhusu mageuzi ya kiuchumi
kutoka wa uchumi wa kijamaa ulioelemea katika umma kumiliki njia kuu za uchumi kwenda
22

mfumo wa soko huria ulioruhusu umiliki binafsi wa mali. Japo kwa mara ya kwanza Watanzania
waliweza kumiliki mali mbalimbali ikiwa pamoja na kufungua milango ya Tanzania kwa uchumi
wa kimataifa, maandalizi hafifu ya kuupokea mfumo mpya wa kiuchumi yalitoa mwanya kwa
waliokuwa katika fursa za uongozi kujineemesha zaidi huku wananchi wa kawaida wakizidi kuwa
masikini. Japo biadhaa zilizokuwa adimu wakati wa mfumo wa uchumi wa kijamaa zilianza
kupatikana katika maduka ya umma na ya binafsi, wananchi wengi wa kawaida hawakuwa na
uwezo wa kuzinunua.

Lakini kingine kilichojitokeza wakati huo ni ukweli kwamba licha ya Tanzania kuwa katika
mfumo wa kijamaa kabla ya mageuzi ya kiuchumi, kuibuka ghafla kwa matajiri waliotumia
nyadhifa zao mara baada ya mageuzi hayo kuliashiria kuwa baadhi ya wasaidizi wa Nyerere
walikuwa waumini wa siri wa mfumo wa ubepari. Katika mazingira ya kawaida, fursa za mfumo
mpya wa uchumi zilitarajiwa kuwanufaisha Watanzania wengi lakini hali ilikuwa tofauti.

Sambamba na mageuzi hayo, Tanzania ililazimika kufuata masharti magumu yaliyowekwa na


mashirika ya fedha ya kimataifa, kubwa zaidi likiwa mipango ya kubadilisha uchumi (Structural
Adjustment Programmes). Miongoni mwa masharti hayo ni wananchi kutakiwa kuchangia
gharama za huduma mbalimbali za jamii kama vile elimu na afya. Kwa vile Mageuzi hayo
yalilenga pia kupunguza matumizi ya serikali, baadhi ya watumishi wa umma walipoteza ajira zao,
na hilo lilipelekea ugumu kumudu mfumo mpya wa uchumi ambapo wananchi walitakiwa
kuchangia gharama za hudama mbalimbali za jamii. Lakini hali ilikuwa ngumu zaidi kwa wasio
na ajira ambapo iliwawia kumudu kuchangia gharama za huduma za jamii. Hii kwa kiasi kikubwa
ilitoa mwanya wa wananchi kutafuta vyanzo vingine vya mapato, halali na visivyo halali, na
rushwa ilianza kushamiri.

Kadhalika, miongoni mwa masharti yaliyoambatana na mageuzi ya kiuchumi ni pamoja na


ubinafsishaji wa mashirika na makampuni ya umma. Kwa kiasi kikubwa zoezi hili liliwanufaisha
wanasiasa na viongozi wengine serikalini huku wananchi wengi wakiachwa watazamaji wasio
na pa kukimbilia. Baadhi ya taasisi hizo, kwa mfano Shirika la Biashara la Mikoa (RTCs), zilikuwa
muhimu kwa mahitaji ya kila siku ya wananchi wengi na kubinafsihwa au kuuzwa kwake
kuliwaathiri wengi.
23

Kwahiyo, kwa ujumla utawala wa Rais Mwinyi ulikabiliwa na matatizo iliyoyarithi kutoka mfumo
wa uchumi wa kijamii na yaliyojitokeza katika mfumo mpya wa soko huria. Hata hivyo,
wachambuzi wa siasa za Tanzania wanauona utawala huo kama uliojenga misingi ya nchi kukosa
mwelekeo, hasa kutokana na Mwinyi kuendeshesha nchi kwa mtindo wa ruksa (laissez affaire).
Wenye uwezo wa kuchuma walichuma, hususan wanasiasa na washirika wao wa kibiashara, lakini
kwa walalahoi hali ya maisha ilizidi kuwa ngumu

Utawala wa Rais Mkapa

Akiwa chaguo la Nyerere, Mkapa aliingia madarakani akikabiliwa na changamoto mbalimbali


alizorithi kutoka kwa mtangulizi wake, Rais Mwinyi. Kingine cha muhimu ni ukweli kwamba
utawala wa Rais Mkapa ulikuwa wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi baada ya sheria
kuuhalalisha mwaka 1992.

Wakati awamu ya kwanza ya Mkapa ilionyesha dalili za matumaini hasa kwa vile ilitilia mkazo
utawala bora, ikiwa ni pamoja na kuunda Tume maarufu ya kuchunguza hali ya rushwa nchini
Tanzania (Tume ya Warioba), na nchi kuendeshwa kwa misingi ya uwazi na ukweli (japo kwa
kiasi kikubwa ni kinadharia), awamu ya pili ya utawala wake ilishuhudia kasi aliyoanza nayo
ikipungua kwa kiasi kikubwa.

Mkapa alipata sifa nyingi kutoka kwa nchi na mashirika wahisani kutokana na sera zake za
kuboresha uchumi wa nchi. Hata hivyo, sifa hizo hazikuweza kutafsirika vema kwa hali ya maisha
ya Watanzania wa kawaida, ambapo kama ilivyokuwa katika utawala wa Rais Mwinyi, bidhaa
mbalimbali za kigeni zilisheheni madukani lakini wananchi wengi hawakuweza kuzimudu
kutokana na kile kilichoitwa ukapa, yaani ukosefu wa fedha.

Mkapa atakumbukwa pia kwa kutilia mkazo sera ya ubinafsishaji. Wakati sera hiyo ilionekana
kuwapendeza wahisani wa kimataifa, ndani ya Tanzania zoezi hilo liligubikwa na ufisadi ambapo
baadhi ya wanasiasa na viongozi wa serikali walitumia fursa hiyo kununua taasisi za umma kwa
bei ya chini. Vilevile, licha ya kauli-mbiu yake ya uwazi na ukweli, kwa kiasi kikubwa zoezi la
ubinafsishaji liligubikwa na usiri mkubwa huku wananchi wa kawaida wakikosa fursa ya kumiliki
raslimali zao ilhali wageni wakimiminika kuzinunua kwa bei nafuu.
24

Wachambuzi wanabainisha kuwa miongoni mwa changamoto zilizoikabili awamu ya pili ya


utawala wa Rais Mkapa ilikuwa shinikizo la kisiasa kutoka kwa mwanasiasa ambaye baadaye
alikuja kuwa mrithi wake, yaani Jakaya Kikwete, anayemaliza muhula wake wa pili mwaka huu.
Inaelezwa kuwa shinikizo hilo lilikuwa sehemu ya harakati za timu ya kumwezesha Kikwete apate
urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, iliyofahamika kama Mtandao wa Kikwete, ambapo
pamoja na Kikwete mwenyewe, iliongozwa na Lowassa na Rostam.

Hata hivyo, mengi ya yaliyojiri katika utawala wa Mkapa hayakufahmika hadi alipotoka
madarakani. Kubwa zaidi lilikuwa kashfa ya kihistoria ya EPA ambapo mabilioni ya shilingi
yaliibiwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Wadadisi wa mambo wanadai kuwa Mkapa
alishinikizwa kufanikisha suala hilo kwa shinikizo la Mtandao wa Kikwete, na inadaiwa
zilisaidia kwa kiasi kikubwa kampeni ya mwanasiasa huyo (Kikwete) kuingia madarakani mwaka
2005.

Doa kubwa katika utawala wa Mkapa ni vurugu zilizotokea huko Zanzibar kufuatia matokeo ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2000. Tarehe 27 Januari 2001, wafuasi wa CUF walifanya
maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo, na vurugu zilizofuatia kati ya polisi na
waandamanaji wa CUF zilipelekea vifo vya watu 37 (kwa mujibu wa takwimu za vyombo vya
kimataifa). Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilizalisha wakimbizi baada ya baadhi ya wafuasi wa
CUF kusaka hifadhi ya ukimbizi katika nchi mbalimbali duniani.

Baada ya Mkapa kustaafu, zilijitokeza tuhuma kwamba wakati utawala wake ukihubiri dhana ya
uwazi na ukweli, aliitumia Ikulu kama sehemu ya kufanya biashara zake ambapo alihusishwa na
uanzishwaji wa benki moja ya biashara, sambamba na tuhuma za kujiuzia mgodi wa makaa ya
mawe wa Kiwira. Kimsingi, skandali ya EPA na tuhuma hizo nyingine ziliathiri legacy ya
Mkapa kwa kiasi kikubwa.

Licha ya sifa kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusu kuboresha uchumi wa Tanzania, hususan
kusimamia mapato kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), utawala wa Mkapa utakumbukwa pia kwa
mahusiano mabaya kati ya chama tawala CCM na vyama vya upinzani, hususan huko Visiwani
ambapo mahusiano kati ya CCM na CUF yalikuwa si ya kuridhisha.
25

Pengine matatizo yaliyoukabili utawala wa Mkapa, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake,
Mwinyi, yalichangiwa na kile kinachoonekana kama mapungufu ya Nyerere kuandaa mrithi wake.
Japo Nyerere alimchagua Mwinyi kumrithi, na baadaye kumpigia debe Mkapa, viongozi wote
hao wawili walikuwa na mapungufu makubwa ukilinganisha na uhodari wa Nyerere. Lakini
pengine mapungufu yao yalichangiwa na ukweli kwamba Tanzania ilikuwa ikipitia kipindi kigumu
cha mabadiliko pasipo maandalizi ya kutosha.

Kwa upande wa uchaguzi mkuu uliohitimisha utawala wa Mkapa na kumwingiza madarakani


Kikwete mwaka 2005, wachambuzi wa kisiasa wanaona kuwa nafasi ya Mkapa ilikuwa finyu hasa
kutokana na kinachoelezwa kuwa kuzidiwa na nguvu ya Mtandao wa Kikwete. Ushiriki wake
katika kampeni hizo ulikuwa ni kama kutimiza wajibu tu kwani nguvu ya Mtandao huo
(unaoelezwa kuwa uliundwa mara baada ya Mkapa kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya
CCM mwaka 1995) ilikuwa kubwa na ilisambaa katika takriban kila sekta ya maisha ya
Watanzania.

Na kana kwamba vurugu za uchaguzi huko Zanzibar mwaka 2000-2001 hazikutosha kutia doa
rekodi ya Mkapa, uchaguzi wa mwaka 2005 uliofanyika chini ya urais wake ulishuhudia tena
Zanzibar ikilipuka kwa vurugu, kufuatia madai kama yale ya mwaka 2000 kuwa CCM iliiba
kura huko Zanzibar.

Pia ni wakati wa utawala wa Mkapa ambapo jina la Tanzania liliingia kwenye anga za ufisadi wa
kimataifa kufuatia kashfa ya rada iliyoihusisha pia nchi ya Uingereza, jambo linaloweza sio tu
kuonyesha unafiki wa nchi wahisani linapokuja suala la utawala bora lakini pia laweza kueleza
kwanini Mkapa alikuwa kipenzi cha nchi na taasisi wahisani.

Licha ya utawala wake kuonekana kama uliofungua milango ya ufisadi nchini Tanzania, Mwinyi
ameendelea kuenziwa vema na Watanzania wengi, kinyume na mtangulizi wake, Mkapa. Sera
isiyo rasmi ya ruksa, licha ya kutoa urahisi kwa wahujumu wa uchumi na mafisadi, iliwapatia
wananchi fursa ya kwanza ya kuiona Tanzania zaidi ya mipaka yake, kufuatia kulegezwa
masharti ya umiliki wa vyombo vya habari, na Watanzania kupata fursa ya kuona kinachojiri nje
26

ya mipaka ya nchi yao kupitia televisheni na redio, sambamba na uingizwaji wa bidhaa mbalimbali
kutoka nje ya nchi.

Pengine legacy kubwa ya Mwinyi ilikuwa katika ustahimilivu wake. Nyingi ya hotuba zake
zilisheheni busara, na yayumkinika kuhitimisha kuwa alisimamia vema zoezi la kuitoa Tanzania
kutoka kwa mfumo wa chama kimoja kuelekea kwenye vyama vingi. Ni wakati wa utawala wake
ambapo Tanzania ilikumba na vuguvugu la kwanza la migogoro ya kidini kati ya Waislamu na
wasio Waislamu. Japo baadhi ya wachambuzi wanaulaumu utawala wa Mwinyi kwa ruksa yake
kwa mihadhara ya kidini ambayo hatimaye ilipelekea kikundi cha Waislam kuchukua sheria
mkononi na kuvunja mabucha kadhaa ya nguruwe jijini Dar es Salaam, akiwa kama Rais Muislam,
Mwinyi alifanikiwa kwa kiasi fulani kuwashawishi Waislamu wenzie juu ya umuhimu wa
kuwavumilia wenzao wasio Waislamu, kwa mfano, kusisitiza kwamba japo ni haramu kwa
Waislamu kula nyama ya nguruwe, imani za baadhi ya wasio Waislamu zinawaruhusu kufanya
hivyo, na ni muhimu kwa Waislamu kuheshimu hilo.

Kwa upande mwingine, utawala wa Mkapa licha ya kukumbukwa kwa tuhuma za ufisadi kama
wa EPA na mauzo fyongo ya mgodi wa Kiwira, ulionekana kama wa kibabe, ambapo sio tu
haukuwekeza katika kujenga mahusiano bora kati ya CCM na Wapinzani lakini pia nyingi ya
hotuba za Rais huyo zilitawaliwa zaidi na ukali kuliko lugha ya upole iliyozoeleka katika utawala
wa rais Mwinyi. Mkapa anakumbukwa kwa kebehi zake kwa vyombo vya habari vya ndani huku
akionekana kuvienzi vyombo vya habari vya kimataifa, licha ya ukweli kuwa mwanasiasa huyo
alikuwa na taaluma ya uanahabari. Kibaya zaidi, ni kwamba baada ya kustaafu kwake, baadhi ya
wachambuzi walitafisiri ukali huo kama kichekesho baada ya kubainika kuwa utawala wa Rais
huyo ulikuwa na maovu yaliyofanyika wakati akihubiri uwazi na ukweli kwa ukali.

Kimsingi, tawala za Mwinyi na Mkapa zilirithi matatizo kutoka katika mfumo wa Ujamaa
uliokuwa ukiingia katika mfumo wa soko huria pasipo maandalizi sahihi. Ni rahisi kwa viongozi
hao kujitetea kuwa walirithi serikali katika awamu zao wakati zikikabiliwa na matatizo chungu
nzima. Na pengine, katika kuwatendea haki, walijitahidi kujaribu kurekebisha mambo pasi
uhakika kuwa wakifanyacho ni sahihi au la. Ni muhimu kutambua kuwa Tanzania ilikuwa ikiingia
kwenye zama mpya pasipo kujifunza uzoefu kutoka nchi nyingine yoyote ile. Na hata kama
27

kungekuwa na nchi ya kujifunza, bado isingekuwa Tanzania, na hivyo kufanya zoezi hilo kubaki
la majaribio tu kama ilivyokuwa kwa Ujamaa. Wakati Mwinyi alifanikiwa kadri ya uwezo wake
kuingiza Tanzania katika mfumo mpya wa kiuchumi- kutoka uchumi wa kijamaa hadi uchumi wa
soko huria,- sambamba na kusimamia mageuzi ya mfumo wa kisiasa- kutoka siasa za chama
kimoja kwenda siasa za vyama vingi,- Mkapa alijitahidi kadri ya uwezo wake kuendeleza mageuzi
ya kiuchumi hasa katika nyanja ya uwekezaji na kubana matumizi, japo hakuwa na mafanikio
makubwa katika kudumisha mageuzi ya kisiasa.

Katika kuhitimisha, sura hii imejaribu kujenga taswira ya mazingira ambayo utawala uliopo
madarakani wa Rais Kikwete uliyakuta, matarajio yakiwa kwamba msingi huo utawezesha kueleza
vema changamoto zilizozikabili awamu mbili za Kikwete hadi muda huu ambapo Tanzania
inaingia kwenye mchakato mwingine wa kumpata rais wa awamu ya tano.

Kadhalika, sura hii imgusia kidogo kuhusu chaguzi zilizotangulia, kwa minajili ya kupata taswira
tarajiwa ya uchaguzi wa mwaka huu. Tukiweka kando matatizo yaliyojitokeza huko Zanzibar
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, na kidogo mwaka 2005, kwa kiasi kikubwa Tanzania
imeendelea kuwa nchi ya amani, hasa kwa kulinganisha na hali ilivyokuwa kwa nchi jirani zake.

Vurugu zilizotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 na kudumu hadi mwaka
uliofuatia, sambamba na vurugu zilizojitokeza nchini Burundi mwaka huu wakati nchi hiyo
ikijiandaa na uchaguzi wake mkuu, na ambazo hadi wakati ninaandika kitabu hiki bado
zinaendelea, na kwa kuzingatia chaguzi nyingine katika nchi mbalimbali zinazoendelea, zinaweza
kupelekea hitimisho kuwa chaguzi 13 zilizotangulia nchini mwetu zimekuwa za amani kwa
ujumla.

Vilevile, kwa kulinganisha na hali ya usalama kwa wengi wa majirani zetu, hususan Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Kenya (inayoendelea kupambana na tishio la ugaidi
kutoka kundi la Al-Shabaab la Somalia), Uganda (ambayo licha ya kupambana na vikundi vya
waasi imekuwa na hali tete ya kisiasa kutokana na Rais Yoweri Museveni kuwa madarakani kwa
muda mrefu), na Rwanda (ambayo licha ya kufanya vizuri kiuchumi imekuwa ikiandamwa na
28

tuhuma za unyanyasaji wa wapinzani wa serikali), Watanzania wana jukumu la kuhakikisha


uchaguzi huu unaendelea kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani.
29

SURA YA PILI: Chaguzi za mwaka 2005 na 2010 na msingi wa changamoto zilizopo


katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu

Yayumkinika kuhitimisha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani Rais
Kikwete uliacha historia ya aina yake, sio tu kwa jinsi chama tawala CCM kilivyopata mgombea
wake bali pia uchaguzi huo ulivyobeba matumaini makubwa kwa wapiga kura na Watanzania kwa
ujumla. Licha ya kushirikisha vyama mbalimbali vya siasa, mchakato wa CCM kumpata mgombea
wake kabla ya uchaguzi huo ulikuwa mithili ya uchaguzi ndani ya uchaguzi. Kimsingi hali hiyo
imekuwa hivyo tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, sio tu kwa sababu katika chaguzi
zote hizo CCM ilishiriki kama chama tawala, lakini mchakato wa chama hicho kumpata mgombea
wake hugusa hisia za Watanzania wengi hususan kutokana na majina 'makubwa' ya makada '
wanaojitokeza kuwania urais.

Kama ilivyoelezwa katika sura iliyopita, kwa kutumia nguvu zake za kisiasa, Nyerere
alimwezesha Mkapa kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka
1995, na hatimaye kushinda katika uchaguzi huo na kuwa Rais wa tatu wa Tanzania. Lakini
mafanikio ya Mkapa yalimaanisha kukwama kwa makada wawili marafiki, Kikwete na Lowassa,
kupata nafasi hiyo ya urais.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa makada hao waliwekeza vya kutosha katika mkakati wao wa
kumwingiza mmoja wao Ikulu, na walifanikiwa kufanya hivyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2005, ambapo Mkapa alikuwa anamaliza mihula yake mawili.

Awali, CCM ilikuwa na utaratibu usio rasmi wa kubadilishana marais, kwa maana kwamba
baada ya Nyerere, mwanasiasa wa CCM kutoka Bara, alifuatia Mwinyi, mwanasiasasa wa CCM
kutoka Zanzibar. Kisha akafuatia Mkapa, mwana-CCM kutoka Bara, na matarajio yalikuwa
kwamba mrithi wa Mkapa angekuwa mwana-CCM kutoka Zanzibar.

Lakini, katika kile kinachoelezwa na wachambuzi wa siasa za Tanzania kama ufanisi mkubwa wa
Mtandao wa Kikwete, utaratibu huo usio rasmi uliwekwa kando, na CCM ikampitisha Kikwete,
mwana-CCM mwingine kutoka Bara kama alivyokuwa mtangulizi wake, Mkapa.
30

Hakuna rekodi angalau ya kimaandishi kuhusu jinsi Mtandao wa Kikwete ulivyofanya kazi.
Mengi ya yanayozungumziwa kuhusu ufanisi wa Mtandao huo yamekuwa ni ya kufikirika zaidi
kwa maana ya kutegemea tetesi kuliko ushahidi halisi. Hata hivyo, moja ya mambo
yaliyoonekana bayana katika harakati za Kikwete na washirika wake kuingiza Ikulu mwaka huo
ni pamoja na kile kinachoweza kuelezwa kama kushika hatamu za ushindani wa kisiasa, kwa
maana ya kuonekana kukubalika na watu wa kada mbalimbali.

Kadri uchaguzi huo ulivyojongea ndivyo kila aina ya dalili ilivyoonekana kuwa sio tu Kikwete
angepitishwa na CCM kuwa mgombea wake bali pia angeshinda urais. Huku akilindwa na haiba
yake iliyofanywa wengi kumuita handsome boy yaani kijana mwenye sura nzuri, sambamba na
kile kilichoonekana kama rekodi isiyo na madoa, angalau kwa maana ya kutohusishwa na kashfa
yoyote kubwa, Kikwete alikuwa mgombea perfect (mwafaka).

Lakini taarifa zinaelezwa kuwa mafanikio ya Kikwete na Mtandao wake hayakutokana tu na sifa
zake binafsi bali pia mchezo mchafu unaodaiwa kufanyika dhidi ya makada wengine wa CCM
waliokuwa wanaowania kumrithi Rais Mkapa. Inaelezwa kuwa mmoja wa wahanga wa mchezo
huo mchafu alikuwa Dokta Salim Ahmed Salim, mwanasiasa na mwanadiplomasia mwenye sifa
kubwa, ndani na nje ya Tanzania, ambaye pia alitajwa kuwa chaguo la Nyerere wakati wa uhai
wake. Salim aliundiwa zengwe (kashfa) kadhaa, kuanzia asili yake (akidai kuwa Mwarabu) na
tuhuma za kuwa mpinzani wa Mapinduzi wa Zanzibar ya mwaka 1963 yaliyomwondoa Sultani na
hatimaye mauaji ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume.

Ushahidi kuwa Salim alihujumiwa waweza kuthibitishwa na habari iliyowekwa katika gazeti moja
wakati wa mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa urais, ambapo habari hiyo ilikuwa na
picha iliyotengenezwa ikimwonyesha Salim kama mwanachama wa kikundi haramu cha Hizbu
ambacho kilikuwa kwa ajili ya maslahi ya Waarabu. Licha ya waandishi wawili wa habari
waliotengeneza picha hiyo kuchukuliwa hatua, lakini madhara yalikuwa yameshafanyika, na
kwa vile Salim alikuwa akionekana kama kikwazo pekee cha kumzuwia Kikwete kuingiza Ikulu,
kuchafuka kwake kulimaanisha kuwa njia ilikuwa nyeupe kwa Kikwete kuwa mrithi wa Mkapa
(ambaye taarifa zilieleza kuwa chaguo lake lilikuwa Salim.
31

Baada ya Kikwete kupitishwa na CCM, Tanzania ilishuhudia kampeni za aina yake za kumnadi
mwanasiasa huyo. Yayumkinika kuhitimisha kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya
uchaguzi, Tanzania ilishuhudia mgombea urais akitangazwa na baadhi ya viongozi wa dini kuwa
ni chaguo la Mungu.

Kama nilivyobainisha awali, hakuna taarifa rasmi kuhusu jinsi Mtandao wa Kikwete ulivyofanya
kazi na kufanikiwa kumwingiza Ikulu mgombea wao. Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa mtandao
huo ulijumuisha watu kutoka kada mbalimbali, kuanzia wanasiasa, viongozi watendaji serikalini,
vyombo vya dola, viongozi wa kidini, wafanyabiashara wakubwa, na wananchi wengineo. Wakati
uratibu wa kampeni kichama uliongozwa na mwanasiasa na mwanamikakati maarufu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, Lowassa na Rostam walionekana kama viongozi wa mtandao, japo
haifahamiki vizuri ni jinsi gani CCM na Mtandao huo walivyoshirikiana, kwa maana ya mipaka
ya majukumu yao. Hata hivyo, kwa vile lengo la wote CCM na Mtandao lilikuwa
kumwezesha Kikwete ashinde uchaguzi huo, si vigumu kuhisi kuwa ushirikiano wao ulikuwa na
ufanisi.

Historia nyingine kuhusu uchaguzi huo, kwa upande wa CCM, ni mlolongo wa ahadi zilizotolewa
na mgombea wa chama hicho, yaani Kikwete. Ni vigumu kuziorodesha zote, lakini kauli mbiu ya
Maisha Baora kwa Kila Mtanzania yanawezekana, inajumuisha dhamira iliyoongoza kampeni
hizo. Licha ya ahadi za kisiasa, CCM na Kikwete walikwenda mbali zaidi na kugusa eneo hatari
la dini. Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ilionyesha kusikiliza kilio cha muda mrefu cha Waislamu
wengi nchini cha kudai kurejeshwa kwa mahakama za kadhi. Kwa kuingiza ahadi hiyo kwenye
ilani yake ya uchaguzi, chama hicho kiliashiria kuwa kimedhamiria kupambana na tatizo la
migogoro ya kidini, ambayo pamoja na mambo mengine ilihusisha suala hilo la mahakama ya
kadhi.

Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Tanzania walionyesha wasiwasi wao kuhusu ahadi hizo lukuki
za Kikwete na CCM, huku wengine wakidhani ingekuwa vigumu kuzitimiza zote katika utawala
wake wa miaka 10 (kwa matarajio kuwa angeshinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka 2010). Hata
hivyo, wananchi wengi walionekana kuwa na imani na Kikwete, na kuamini ahadi zake na za
32

chama chake, hasa ikizingatiwa kuwa katika mikutano yake ya kampeni alionekana sio tu kama
mtu aliyekuwa akiguswa na matatizo mengi ya Watanzania bali pia alionyesha kuyaelewa.

Kwa waliokuwa wanamfahamu katika maisha yake binafsi, walimwona Kikwete kama mtu wa
watu, asiye na makuu, na mwenye rekodi ya kuwasaidia watu mbalimbali wakati wa utumishi
wake serikalini. Uso wake wenye tabasamu muda wote ulimjengea kupendwa na Watanzania
wengi, na hilo pia lilirahisisha kuaminika kwake, hususan kwenye kauli mbiu ya Maisha Bora
kwa Kila Mtanzania.

Kama ilivyotarajiwa, Kikwete aliibuka na ushindi mnono katika uchaguzi huo ambapo alipata
jumla ya kura 9,123,952 (sawa na asilimia 80.28) huku mpinzani wake wa karibu, mgombea wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiambulia kura 1,327,125 (sawa na asilimia 11.68). Ukiweka
kando mgombea wa Chadema, Freeman Mbowe aliyepata jumla ya kura 668,756 (sawa na asilimia
5.88), wagombea wengine saba kutoka vyama vya TLP (Augustine Mrema), NCCR- Mageuzi
(Dokta Sengodo Mvungi), DP (Christopher Mtikila), NLD (Emmanuel Makaidi), TPP- Maendeleo
(Anna Senkoro), Demokrasia Makini (Leonard Shayo) na SAU (Paul Kyara) waliambuliwa chini
ya kura laki moja kila mmoja.

Kwa matokeo hayo, hata kama vyama vya upinzani vilivyoshiriki uchaguzi huo vingeunganisha
jumla ya kura zao, bado CCM kupitia mgombea wake Kikwete ingeibuka na ushindi huo mkubwa.
Hata hivyo ni muhimu kupigia mstari matokeo ya mgombea wa Chadema, Mbowe, kwani
yatarejewa tena katika sura zijazo ili kulinganisha na matokeo yake katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010. Kadhalika matokeo ya wagombea wa CUF, NCCR- Mageuzi na NLD yatafuatiliwa
kutoka katika uchaguzi huo wa mwaka 2005 na kulinganishwa na mwaka 2010, kwa minajili ya
kupata taswira ya ushirika wa vyama hivyo UKAWA- katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Baada ya kuingiza madarakani, Rais Kikwete alianza na tahadhari kuwa tabasamu lake lilitafsiriwe
vibaya, na kuahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wala rushwa. Kikwete alikwenda mbali zaidi
ambapo licha ya kutoa deadline kwa wala rushwa, pia alibainisha kuwa anawafahamu wala
rushwa kwa majina, na wasimlaumu iwapo hawatobadilika. Kwa vile aliendesha kampeni zake
33

akihubiri kuhusu maisha bora kwa kila Mtanzania, baadhi ya wananchi waliamini onyo hilo la
Kikwete wakitarajia hatua kali zingefuata kwa wala rushwa watakaogoma kubadilika.

Kilichofuata baada ya mwanzo huo mzuri (angalau kwa kutoa kauli tu inayoonyesha kuwa sio tu
Rais anauchukia rushwa bali pia ana dhamira ya kupambana nayo kwa dhati) ni hadithi ya
kusikitisha. Chini ya mwaka mmoja tangu Rais Kikwete aingie madarakani, utawala wake ukaanza
kuandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi, na neno UFISADI likatokea kujipatia umaarufu
mkubwa katika miaka 10 ya utawala wake.

Kimsingi, Kikwete aliingia madarakani akiwa amebeba kashfa ya EPA iliyojiri katika utawala
wa mtangulizi wake, Mkapa. Japo sababu hii haiwezi kuwa utetezi kwake lakini kiuhalisia alijikuta
akiingia madarakani na kashfa hiyo pasipo kuitengeneza akiwa madarakani kama rais. Hata hivyo,
maelezo mbalimbali kuhusu kashfa hiyo yanamhusisha Kikwete kupitia Mtandao wake,
unaodaiwa kuwa ndio ulioshinikiza kutolewa kwa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu, fedha
zinazodaiwa kutumika katika kampeni za CCM kumwingiza Kikwete madarakani.

Moja ya sababu kuu zilizoufanya utawala wa Kikwete ugubikwe na tuhuma mfululizo za ufisadi
ni kile kinachoelezwa kama udhaifu wake katika kutumia madaraka aliyopewa na Katiba,
kuchukua hatua stahili dhidi ya wahusika bila kujali ukaribu aliokuwa nao. Hapa ninamaanisha
kwamba laiti Kikwete angeweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi yake binafsi au ya watu
wake wa karibu, angeweza kabisa kuwageuka.

Siasa za uchaguzi katika nchi nyingi duniani huambatana na jitihada za taasisi au watu wenye
maslahi binafsi kukisaidia chama au mgombea kwa matarajio ya kurejeshewa fadhila pindi chama
au mgombea husika akiingia madarakani. Yayumkinika kuamini kuwa wengi wa waliojihusisha
na Mtandao wa Kikwete hawakufanya hivyo kwa maslahi ya taifa au ya CCM au Kikwete
mwenyewe bali walikuwa na matarajio kuwa nao wangenufaika pindi mwanasiasa huyo akiingia
madarakani.

Licha ya onyo alilotoa mara baada ya kuingiza madarakani kuwa asingekuwa na huruma kwa wala
rushwa, na kutahadharisha kuwa tabasamu lake lisitafsiriwe vibaya, kuzungukwa na watu wengi
waliokuwa wakitarajia fadhila kutoka kwake kulichangia kumkwamisha kuchukua hatua zozote
34

za maana dhidi ya wahusika katika kashfa mbalimbali. Ukaribu wake na wahusika hao sio tu
ulionekana kama kinga kwao lakini pia ulichafua taswira yake kwa jamii, hususan katika
kujengeka hisia kama kwa vyovyote Bwana Mkubwa (Rais Kikwete) anafahamu kuhusu suala
hili au labda mhusika katumwa na Bwana Mkubwa.

Mlolongo wa tuhuma za ufisadi zilizouandama utawala wa Kikwete ulianza na kashfa ya kihistoria


ya Richmond ambayo ilimhusisha pia aliyekuwa Waziri Mkuu (wakati huo) na mshirika wa
Kikwete, Lowassa. Licha ya kuwa kashfa kubwa ya kwanza kwa utawala wa Kikwete (tukiweka
kando kashfa ya EPA ambayo haikuuhusisha utawala wake moja kwa moja), kashfa hiyo pia
ilipelekea msukosuko mkubwa ambao ulikaribia kupelekea Bunge la Muungano kuvunjika. Lakini
pia, madhara makubwa ya kashfa hiyo ni mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM ambao hatimaye
ulipelekea jina la Lowassa kukatwa katika azma yake ya kuomba ridhaa ya kuwa mgombea urais
kwa tiketi ya chama hicho. Kimsingi, upinzani mkali unaoikabili CCM wakati huu wa kampeni
unaweza kuhusishwa na suala hilo la Richmond.

Kama ilivyoonyeshwa awali, Lowassa na Kikwete walikuwa marafiki wakubwa, na wawili hao
pamoja na Rostam waliunganisha nguvu zao zilizomwezesha Kikwete kupata urais mwaka 2005.
Taarifa zinaelezwa kwamba wakati Kikwete anaingia madarakani, kulikuwa na makubaliano
yasiyo rasmi kuwa akimaliza muda wake ampishe rafiki yake Lowassa. Hata hivyo, inadaiwa
kuwa sakata la Richmond liliathiri mahusiano ya wanasiasa hao ambao inaelezwa walikuwa
marafiki hata nje ya maisha yao ya kisiasa.

Maelezo yasiyo rasmi yanadai kuwa kilichosababisha mfarakano baina ya wanasiasa hao ni hisia
kwamba Kikwetealimtosa Lowassa wakati Waziri Mkuu huyo wa zamani alipobanwa na
Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza suala la Richmond, na kupendekeza Lowassa achukue
hatua stahili, na yeye kuamua kujiuzulu mwezi Februari 2008, chini ya miaka mawili tangu
ateuliwe kushika wadhifa huo.

Kama ni kweli kuwa Kikwete hakumsaidia rafiki yake vya kutosha au la, ni vigumu kuthibitishwa
kwa sababu hakujawahi kupatikana taarifa rasmi kuhusu suala hilo ukiachia mbali taarifa za
Kamati Teule ya Bunge, maarufu kama Kamati ya Mwakyembe ambayo kwa kiasi kikubwa
35

ilimbembesha Lowassa mzigo wa lawama. Katika utetezi wake, Lowassa alidai chanzo cha sakata
hilo ni watu walitamani nafasi yake ya Uwaziri Mkuu, na hadi muda huu ameendelea kusisitiza
kuwa maagizo ya kuipa zabuni kampeni feki ya Richmond PLC ya Marekani yalitoka ngazi za
juu. Kadhalika, mwanasiasa huyo ameendelea kujitetea kuwa aliamua kujiuzulu kwa sababu tu
ya kuwajibika kisiasa lakini si kuashiria kuwa yeye ndio mhusika.

Kama ilivyobainishwa hapo juu, kashfa hiyo na kujiuzulu kwa Lowassa kulizua mgawanyiko
ndani ya CCM, ambapo licha ya kujiuzulu kwake, Lowassa alijitokeza kuwa mwanasiasa mwenye
nguvu kubwa ndani ya chama hicho. Wajuzi wa siasa za Tanzania wanadai kuwa nguvu ya
mwanasiasa huyo ilichangiwa zaidi ni misaada yake kwa viongozi mbalimbali wa CCM kwenye
chaguzi za ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, kuibuka kwa wanasiasa vijana kama vile Nape Nnauye kulimsababishia matatizo
Lowassa, hususan katika ajenda ya kujivua magamba, zoezi lililotarajiwa kuisafisha CCM baada
ya kwa kuwachukulia hatua makada wake mbalimbali waliokuwa wakiandamwa na kashfa za
ufisadi. Japo zoezi hilo halikufanikiwa kwa kiasi kikubwa, inaelezwa kuwa miongoni mwa
wahanga wake ni Rostam aliyeamua kujiuzulu ubunge na nyadhifa zake ndani ya chama hicho
tawala. Hata hivyo, inaelezwa pia kuwa mahusiano katika ya mwanasiasa huyo na Lowassa
yameendelea kuwa imara japo haifahamiki vizuri kuhusu uhusiano wake na Kikwete.

Kashfa ya Richmond sio tu iliibuliwa na vyama vya upinzani, hususan Chadema, lakini pia
iligeuka kuwa ajenda kuu ya Wapinzani dhidi ya CCM, kama ilivyojitokeza kwa kashfa nyingine
zilizoibuka baadaye. Yayumkinika kuhitimisha pasi shaka kuwa kuimarika kwa vyama vya
upinzani Tanzania Bara kumechangiwa zaidi na mapungufu ya CCM kuliko uimara wa vyama
hivyo. Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilishuhudia siri za ndani za CCM zikiwekwa hadharani
na wanasiasa wa vyama vya upinzani. Kubwa zaidi ilikuwa Orodha ya Aibu (List of Shame)
iliyotangazwa na viongozi wa Chadema, ikiwataja wanasiasa kadhaa wa CCM, akiwemo Kikwete
na Lowassa. Msimamo thabiti wa vyama hivyo, hususan Chadema, sambamba na serikali ya
Kikwete kuendelea kuandamwa na kashfa za ufisadi, kulichangia kuwafanya wananchi waanze sio
tu kupoteza imani na chama hicho tawala bali pia kupata matarajio mapya kutoka kwa vyama vya
upinzani, ambavyo kimsingi vilionekana kuyaelewa zaidi matatizo ya wananchi kuliko CCM.
36

Kadhalika, chama hicho tawala kilijikuta kikitumia muda mwingi kujitetea kuliko kujivunia rekodi
yake ya kuwa madarakani kwa muda mrefu kuliko chama kingine chochote kile cha siasa nchini.
Vilevile, chini ya miaka mawili baada ya kuingiza madarakani, Rais Kikwete alilazimika kufanya
mabadiliko ya kwanza ya baraza lake la mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri
Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Hata hivyo, kungoka kwa Lowassa kutoka katika nafasi yake ya Uwaziri Mkuu kulipelekea CCM
kumzalisha Frankenstein wa kisiasa ndani ya chama hicho. Katika mazingira ya kushangaza
lakini yanayoeleweka, Lowassa aliibuka kuwa mwanasiasa mwenye nguvu kubwa kabisa katika
chama hicho, nguvu inayoweza kulinganishwa kuwa karibu na aliyokuwa nayo Nyerere. Labda
tofauti pekee kati ya Lowassa na Nyerere ni kwamba mwanzilishi huyo wa TANU na CCM
aliheshimika kwa matendo yake kwa taifa na chama, sambamba na kutokuwa na upinzani wowote
ule ndani ya chama hicho hadi alipojiuzulu, ilhali licha ya Lowassa kuangaliwa na vyama vya
upinzani kama mfano hai wa ufisadi ndani ya CCM (hasa kwa vile baadhi waliona kuwa kujiuzulu
kwake tu kulikuwa hakutoshi na alipaswa kuchukuliwa hatua kali zaidi) lakini pia alipata upinzani
kwa baadhi ya wana-CCM wenzake kama vile Nape Nnauye, upinzani ambao miaka 7 baadaye
uliua ndoto yake ya kumrithi Kikwete kuwa rais, na hatimaye kulazimika kujiunga na Chadema
kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA.

Wakati suala hilo la Richmond halikuweza kumalizika kwa kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri
kadhaa pekee, kwani limeendelea kugusa vichwa vya Watanzania hadi muda huu, na kwa sasa
limegeuka kuwa ajenda muhimu dhidi ya Lowassa katika harakati zake za kusaka urais, pia
lilipelekea sintofahamu nyingine inayohusu kampeni ya Dowans. Lakini, kama nilivyoeleza
awali, ufisadi wa Richmond ulikuwa mwanzo tu wa mlolongo wa kashfa mbalimbali
zilizouandama utawala wa Kikwete.

Mwaka 2008 , kashfa ya EPA iliibuka kwa kasi na kuitingisha serikali ya Kikwete kwa kiasi
kikubwa. Katika kashfa hiyo, jumla ya shilingi bilioni 133 zilikwapuliwa kutoka akaunti ya madeni
ya kigeni (EPA) huko Benki Kuu. Licha ya serikali kuunda tume ya uchunguzi, sambamba na
Wapinzani, hususan Chadema kulivalia njuga suala hilo, hadi sasa hakuna hatua za maana
zilizochukuliwa dhidi ya wahusika. Kadhalika, mmiliki wa kampuni ya Kagoda, inayodaiwa
37

kufaidika zaidi na mgao huo, amaeendelea kutotajwa hadharani licha ya taarifa mbalimbali zisizo
rasmi kuihusisha na mfanyabiashara mmoja maarufu ambaye pia alikuwa kiongozi wa CCM kabla
ya kujiuzulu.

Utata kuhusu ufisadi wa EPA umeendelezwa pia na mkanganyiko kuhusu kifo cha aliyekuwa
Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali. Wakati taarifa rasmi za serikali zikidai kuwa gavana huyo
alifariki akiwa nchini Marekani, tetesi mitaani zimekuwa zikidai kuwa gavana huyo bado yupo
hai. Ballali ni mtu muhimu sana katika suala hilo, na inaaminika kuwa alikuwa akiwafahamu
wahusika wa ufisadi huo kwa majina.

Kama ilivyokuwa kwa ufisadi wa Richmond, ufisadi wa EPA umeendelea kuwa suala linaloumiza
vichwa vya wananchi wengi hasa kutokana na usiri mkubwa unaolizunguka. Lakini matukio hayo
mawili makubwa ya ufisadi hayakuwa ya mwisho, kwani utawala wa Kikwete ulijikuta
ukikabiliwa tena na kashfa nyingine mbili kubwa, yaani Operesheni Tokomeza Ujangili na
akaunti ya Tegeta Escrow.

Kufuatia kushamiri kwa ujangili, serikali iliamua kufanya Operesheni maalum katika mikoa ya
Manyara, Singida, Arusha, Dodoma na Tabora kukabiliana na uhalifu huo kuanzia Oktoba 2013
huo lakini ilibidi kusitishwa takriban mwezi mmoja baadaye kufuatia madai ya ukiukwaji mkubwa
wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na vifo vya raia 13 na askari 6, utesaji wa kutisha wa
watuhumiwa, ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi. Taarifa ya uchunguzi kuhusus
kashfa hiyo ilipelekea Rais Kikwete kuwatimua mawaziri kadhaa na hatimaye kufanya mabadiliko
katika baraza lake la mawaziri. Mawaziri waliongolewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo
iliyoongezewa shinikizo la wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David Mathayo.

Mwaka jana, 2014, serikali ya Kikwete ilijikuta ikikabiliwa na kashfa nyingine kubwa kufuatia
taarifa za kuibiwa mabilioni ya fedha za umma kutoka akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki
Kuu ya Tanzania, iliyofunguliwa baada ya mgogoro na kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL na
38

Tanesco. Kashfa hiyo iliyovuta hisia za wananchi wengi iliweka historia ya aina yake kutokana na
wabunge wengi wa CCM kuungana na wabunge wa vyama vya upinzani kudai hwahusika katika
kashfa hiyo wachulkuliwe hatua.

Licha ya wizi huo, taarifa mbalimbali zilibainisha majina ya watendaji kadhaa wa serikali,
wanasiasa, viongozi wa dini na watu wengine mbalimbali kuwa wanufaika wa mgao uliotolewa
na mfanyabiashara James Rugemalira wa IPTL na mwenzie Herbinder Seth Singh. Kufuatia
mapendekezo ya kamati ya bunge iliyochunguza suala hilo, Rais Kikwete alilazimika kumtimua
Waziri wake Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa mmoja wa wanufaika wa mgao huo, sambamba
na kukubali kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema na
baadaye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo. Kadhalika, viongozi
kadhaa wa CCM walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao katika kamati za bunge kutokana na suala
hilo.

Kwa ujumla, pamoja na mambo mbalimbali aliyoifanyia Tanzania, Kikwete atakumbukwa zaidi
kwa utawala wake uliogubikwa na ufisadi mfululizo ambao mara kadhaa ulimlazimisha kufanya
mabadiliko ya baraza lake la mawaziri, na anaingia katika historia kama rais wa Tanzania
aliyefanya mabadiliko ya mawaziri mara nyingi zaidi kutokana na kashfa zilizowahusu baadhi yao.

Kimsingi, yayumkinika kuhitimisha kuwa ombwe lililojitokeza katika tasnia ya ungozi wa kitaifa
mara baada ya Nyerere kujiuzulu limechangiwa zaidi na kosa la Nyerere kutoandaa vema
uongozi baada ya yeye kutoka madarakani. Tangu alipojiuzulu na hatimaye kufariki, nchi yetu
imeshindwa kabisa kupata kiongozi wa aina ya Nyerere aliyeweka mbele maslahi ya taifa kuliko
yake binafsi. Kadhalika, uzalendo umekuwa ukididimia kwa kasi hususan kutokana na kujengeka
kwa hisia kuwa utumishi kwa umma ni fursa ya ulaji. Ni katika mazingira hayo, siasa imegeuka
kuwa kama ajira huku wasomi kutoka kada mbalimbali wakikimbilia kwenye siasa kwa kutambua
kuwa huko ndipo kwenye 'ulaji.'

Sura hii imefanya uchambuzi wa jumla kuhusu miaka 10 ya utawala wa rais Kikwete ambao
utahitimishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Lengo la uchambuzi huo ni kupata picha ya
mazingira ambayo nchi yetu inaingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kadhalika, kwa
39

kuangalia utawala uliopo madarakani, inatarajiwa kuwa sura zijazo zitakuwa katika fursa nzuri
kubainisha fursa na nafasi zinazokikabili chama tawala CCM na mgombea wake, Magufuli, kwa
upande mmoja, na vyama vya upinzani, hususan UKAWA na mgombea wao, Lowassa, kwa
upande mwingine. Yeyote atakayeingia madarakani atakuwa na jukumu kubwa la kuibadilisha
Tanzania yetu hasa kwa kuzingatia yaliyojiri katika miaka 30 baada ya Nyerere kungatuka.
40

SURA YA TATU: Mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais

Sura hii inajadili kwa undani mchakato wa chama tawala CCM kumpata mgombea wake kwa tiketi
ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Tofauti na chaguzi zilizopita, kwa mara ya kwanza tangu Tanzania iingie kwenye mfumo wa
vyama vingi, CCM ilikuwa na jina la kada mmoja lililozungumwa mno kuwa na uwezekano wa
kugombea urais mwaka huu. Jina hilo si jingine bali la kada wa siku nyingi wa chama hicho
aliyeshika nyadhifa mbalimbali katika awamu tofauti, na hatimaye kuwa Waziri Mkuu, Edward
Lowassa. Licha ya utumishi wake wa muda mrefu serikalini, na kama ilivyoelezwa katika sura
zilizopita, mwanasiasa huyo alikuwa sehemu muhimu ya kampeni za Rais Kikwete kuingiza
madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005. Pamoja na mfanyabiashara Rostam Aziz, Lowassa
na Kikwete walifahamika kama viongozi wa kinachoitwa Mtandao wa Kikwete, kikundi kisicho
rasmi kilichojumuisha watu kutoka kada mbalimbali, kikiwa na lengo la kumwingiza Kikwete
madarakani kumrithi Raia wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa Mtandao huo uliundwa mara baada ya Kikwete na
Lowassa kushindwa azma ya mmoja wao kuingiza Ikulu katika uchaguzi wa mwaka 1995, ambapo
inaelezwa kuwa Nyerere alitumia nguvu zake kubwa kisiasa kuwazuwia wanasiasa hao na papo
hapo kumbemba mwanasiasa chaguo lake, yaani Mkapa.

Taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa kulikuwa na makubaliano kati ya Kikwete na Lowassa
kupokezana urais aidha baada ya miaka mitano ya Kikwete madarakani aua atakapomaliza mihula
yote miwli. Hata hivyo, kashfa ya Richmond iliyopelekea Lowassa kujiuzulu ilionekana kujenga
mpasuko sio tu katika makubaliano hayo bali pia katika kinachoelezwa kuwa urafiki wa muda
mrefu kati yao.

Tetesi kuwa Lowassa angewania urais zilianza kitambo, lakini zilipata nguvu zaidi wakati CCM
ikijiandaa kwa uchaguzi wa mwaka 2010 ambao kwa mujibu wa taratibu zisizo rasmi ndani ya
chama hicho, rais aliyekuwa madarakani alistahili kupitishwa kugombea tena ili amalizie awamu
yake ya pili. Wakati huo, kulikuwa na tetesi zisizo rasmi kuhusu uwezekano wa Lowassa kuachana
na Kikwete ili nae agombee, lakini tetesi hizo zilipotea haraka kama zilivyozuka.
41

Hata hivyo, dalili za Lowassa kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka zilijidhihirisha
zaidi katika chaguzi za ndani za CCM mwaka 2012, ambapo makada waliokuwa wakimuunga
mkono walifanikiwa kushinda nyadhifa mbalimbali, huku ikidaiwa kuwa wengi wao walisaidiwa
kifedha na Lowassa na washirika wake. Ushindi huo ulionekana kama mwanzo wa kilichokuja
kufahamika kama kambi ya Lowassa ndani ya CCM.

Kadri siku zilivyokwenda ndivyo tetesi za Lowassa kuwania urais zilivyozidi kupamba moto. Hata
hivyo, kadri tetesi hizo zilivyopamba moto ndivyo upinzani dhidi yake, hususan ndani ya CCM ,
ulivyozidi kujitokeza, kubwa zaidi likiwa wazo la CCM kujivua magamba, lilishikiliwa kwa
nguvu kubwa na kada kijana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. Wazo hilo lilionekana
kuwavutia sio wana-CCM tu bali hata wananchi wengine wasiojihusisha na chama hicho tawala.
Kimsingi, ilionekana kuwa chama hicho kimetambua makosa yake na kina nia ya kujirekebisha.
Kadhalika, hatua hiyo ilonekana kutambua jinsi ajenda ya ufisadi ilivyokuwa ikivipaisha vyama
vya upinzani hususan Chadema, huko CCM ikitumia muda mwingi kujitetea.

Kujivua gamba ilikuwa moja ya fursa adimu na muhimu kwa chama hicho tawala kurejesha
imani kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla. Yayumkinika kuhitimisha kuwa laiti
mpango huo ungefanikiwa, CCM isingekuwa inapitia wakati mgumu kwenye kampeni za kuwania
uraia wakati huu ninapoandika kitabu hiki. Urahisi katika utekelezaji wa mpango huo ulikuwa
kwenye ukweli kwamba kuna wana-CCM wengi waliokuwa wakiuafiki, na wananchi kwa ujumla
walikuwa na mtizamo chanya.

Lakini licha ya mpango huo kufanikiwa kiasi kwa kupelekea mmoja ya wanasiasa waliokuwa na
nguvu kubwa ndani ya CCM, Rostam Aziz, kuamua kujiuzulu ubunge na nyadhifa zake ndani ya
chama hicho, kwa kiasi kikubwa kinachotajwa kama nguvu ya Lowassa kilifanikiwa kuuzima.
Kikwazo kingine kwa mpango huo kilikuwa Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Taifa, kuonekana kumtumia Nape kufanikisha mkakati huo pasipo ushiriki wake yeye (Kikwete)
mwenyewe.

Hoja kubwa dhidi ya kujivua gamba zilikuwa ni pamoja na kuushutumu mpango huo kuwa
ungepelekea kuigawa CCM, sambamba na kumtuhumu Nape kuwa anamwandama Lowassa kwa
42

sababu binafsi. Kwa ujumla, wazo hilo zuri liligeuzwageuzwa hadi kuonekana kuwa lingekuwa
na athari zaidi kuliko faida kwa chama hicho.

Kipenga cha mbio za kuwania urais kwa tiketi ya CCM kilipulizwa na rasmi na kada kijana,Naibu
Waziri Wa Sayansi na Teknolojia na msaidizi wa zamani wa Rais Kikwete, January Makamba,
kutangaza nia ya kuwania urais, takriban mwaka mmoja kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato
kamili wa CCM. Tangazo hilo la January liliingiza CCM kwenye zama mpya kwani huko nyuma
suala la kuwania urais lilifanywa kwa siri hadi ulipokaribia muda kwa chama hicho kuanza
mchakato wake.

Licha ya hofu kuwa kwa kutangaza nia ya kuwania urais mapema hivyo January angeweza kuwapa
silaha maadui zake kisiasa, Watanzania wengi walilipokea vema tamko lake huku wengi wakiona
kuwa ni vema kwa wanasiasa wanaotaka kuwania urais kujitokeza hadharani mapema ili wananchi
wawafahamu vema. Kwa upande mwingine, tangazo hilo la January lilikuwa changamoto kubwa
kwa Lowassa ambaye jina lake lilikuwa likihusishwa na urais kwa miaka kadhaa.

Pamoja na kuulizwa mara kadhaa iwapo atawania urais, Lowassa aliendelea kukaa kimya, hatua
inayoweza kuwa ilichangia kutofanikiwa kwa dhamira yake ya kuwa mrithi wa rafiki yake wa
zamani, Kikwete. Katika mazingira ya kawaida tu, ilionekana kuwa iwapo mwanasiasa kijana
kama January anapata ujasiri kuwatangazia Watanzania kuwa anataka kuwania urais, kwanini
mkongwe kama Lowassa ashindwe kuwa muwazi kwa wananchi? Yawezekana alikuwa hajaamua
kwa dhati kuchukua hatua hiyo au huenda ulikuwa ni mkakati wenye lengo la kuwashtukiza watu,
lakini vyovyote ilivyokuwa, safari yake ya muda mrefu kutaka urais kupitia CCM iliisha baada ya
jina lake kukatwa na vikao vya mchujo.

Uamuzi wa January kutangaza mapema kuwa atawania urais hatimaye ulipelekea wanasiasa
wengine nao kuanza kuzungumzia hadharani kuwa wana nia ya kufanya hivyo japo hawakuwa
wawazi sana. Pengine kutokana na ugeni wa utaratibu wa wanasiasa kutangaza nia ya urais
kitambo kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza, au pengine kwa sababu za kihafidhina tu, tangazo
la January lilikumbana na vikwazo ndani ya chama chake ambapo ziliibuka tuhuma kuwa
mwanasiasa huyo, na baadaye makada wenzie watano, Lowassa, Bernard Membe, Stephen
43

Wassira, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye, na William Ngeleja, kukaripiwa na chama
hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukiuka taratibu na kanuni za CCM za uchaguzi. Pamoja na
kukaripiwa, makada hao walihukumiwa kifungo cha miezi kadhaa, japo kiuhalisia takriban wote
waliendelea kujinadi wakati wa kifungo hicho.

Mara baada ya chama hicho kufungua rasmi mchakato wa kuomba ridhaa ya kuwania urais kwa
tiketi ya chama hicho, Juni 6, 2015, makada kadhaa walijitokeza kuchukua fomu. Kwa mara ya
kwanza katika historia ya CCM, na ya Tanzania kwa ujumla, makada 43 walichukua fomu. Orodha
ya makada hao ni kama ifuatavyo:

1. Amos Robert Siyatemi

2. Augustine Ramadhani.

3. Balozi Ali Karume

4. Balozi Amina Salum Ali

5. Bernard Membe

6. Boniface Ndengo

7. Charles Makongoro Nyerere

8. Dk. Asha Rose Migiro

9. Dk. Augustine Mahiga

10. Dk. Harrison Mwakyembe

11. Dk. John Magufuli

12. Dk. Khamis Kigwangallah


44

13. Dk. Mwele Malecela

14. Dk. Titus Kamani

15. Dk.Mohamed Gharib Bilal

16. Dk.Muzzamil Kalokola

17. Edward Lowassa

18. Frederick Sumaye

19. Hassy Kitine

20. Hellen Elinawinga

21. January Makamba.

22. Lazaro Nyalandu

23. Leonce Mulenda

24. Lidephonce Bilohe

25. Luhaga Mpina

26. Maliki Marupu

27. Mathias Chikawe

28. Mizengo Pinda

29. Mohamed Gharib Bilal

30. Monica Mbega.

31. Musa Mwapango


45

32. Mwigulu Nchemba

33. Patrick Chokala

34. Peter Isaiah Nyalali

35. Peter Nyalali.

36. Prof Mark Mwandosya

37. Prof. Sospeter Muhongo

38. Ritha Ngowi

39. Samuel Sitta

40. Samwel John

41. Stephen Wassira

42. Veronica Kazimoto

43. William Ngeleja

Hata hivyo, kati ya wagombea hao 43, wanne kati yao hawakurejesha fomu na hivyo kufanya
majina yaliyopelekwa kwenye vikao vya mchujo vya CCM kubaki 38 tu. Wagombea hao
walioshindwa kurejesha fomu ni Dkt Kalokola, Elinawinga, Chalamila na Nyalali.

Zoezi hilo la kuchukua na kurejesha fomu lilishuhudia sehemu kubwa ya watendaji wa serikali
wakiwania kumrithi Rais Kikwete, ambapo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri 10 na
Manaibu Waziri wawili, sambamba na Jaji Mkuu Mstaafu mmoja, Wakurugenzi wakuu wawili wa
zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, na wengineo.

Wingi huo wa makada ulizua mjadala wa aina yake. Kwa upande mmoja, kuna waliotafsiri idadi
hiyo kubwa kuwa ni dalili za kushamiri kwa demokrasia ndani ya chama hicho, wakirejea historia
46

ya zama za chama kimoja ambapo jina moja tu la mwanachama mmoja tu liliwasilishwa kwa ajili
ya kupigiwa kura katika vikao vya CCM.

Hata hivyo, baadhi ya watu walitafsiri wingi huo kuwa ni athari ya wazi ya miaka 10 ya Kikwete
madarakani. Wenye mtizamo huo walidai kuwa urais wa Kikwete ulishusha hadhi ya taasisi ya
urais kiasi kwamba kila mtu alidhani anaweza kuwa rais.

Tukirejea kwenye jitihada binafsi za makada kuwania nafasi hiyo, kuna mambo kadhaa
yaliyojitokeza yanayopaswa kugusiwa hapa. Kubwa zaidi lilikuwa jinsi Lowassa alivyoonekana
kupata ufuasi mkubwa, mara baada ya kutangaza nia na katika muda wote aliopita maeneo
mbalimbali kusaka wadhamini. Na japo kanuni za chama hicho zilimtaka mgombea kupata
wadhamini 450 katika mikoa 15, mwanasiasa huyo alipata wadhamini 1,600,000. Kwa jinsi hali
ilivyokuwa wakati huo, isingekuwa jambo la kushangaza kuhisi kuwa kilichokuwa kikisuburiwa
ni Lowassa kuapiashwa tu na kuwa rais.

Hata hivyo, pamoja na dalili hizo za kukubalika na wengi, ndani ya CCM kulikuwa na sauti kadhaa
za upinzani dhidi yake. Kwa mfano, mara kadhaa, hasimu wake wa muda mrefu, Nape, alitoa
matamshi yalioashiria kuwa kuna jitihada za kumzuwia Lowassa kuteuliwa kuwa mgombea urais
kwa tiketi ya CCM. Kadhalika, baadhi ya wagombea, kwa mfano Makongoro Nyerere, Waziri
Mkuu wa zamani Sumaye, na Waziri Sitta, walitumia hotuba zao mbalimbali zilizoashiria kuwa
na ujumbe kuwa Lowassa hafai.

Katika muda wote huo Rais Kikwete hakuonyesha dalili yoyote iwapo anamuunga mkono
Lowassa au la. Hilo lilichangia kwa kiasi kikubwa kuugeuza mchakato huo kuwa kama
referendum kwa wanasiasa hao, ambapo kwa upande mmoja, swali lilikuwa, Je Kikwete
atamtosa rafiki yake au atambemba? Na kwa upande mwingine, swali kuhusu Lowassa
lilikuwa, atakatwa (katika vikao vya mchujo vya CCM) au hatokatwa?

Pengine moja ya dalili za awali kuwa licha ya ufuasi mkubwa alioupata wakati anasaka wadhamini
sehemu mbalimbali, na licha ya kutajwa kwa muda mrefu kuwa angegombea urais, Lowassa
hakuwa na hakika iwapo Kikwete atamuunga mkono, ni katika kurejea mara kwa mara katika
mikutano yake kauli kwamba anaamini rafiki yake huyo atamsapoti kama yeye alivyomsapoti
47

mwaka 2005. Haihitaji uelewa mkubwa wa jinsi urafiki unavykuwa kutambua kuwa marafiki
walioshibana hawahitaji kukumbushana fadhila walizofanyiana huko nyuma. Kwamba kama
kweli urafiki wa wawili hao ni wa dhati basi watasaidiana tu pasi haja ya Lowassa kukumbushia
msaada wake kwa Kikwete miaka 10 iliyopita.

Kwa upande mwingine, ukimya wa Kikwete tangu rafiki yake huyo alipotangaza nia ya kuwania
urais, na kurejea kauli kwamba hana mgombea wake, ilianza kujenga hisia kuwa huenda tetesi
kuwa urafiki kati ya wanasiasa hao wawili si mzuri zina ukweli. Hata hivyo, kwa vile kwa kiasi
kikubwa urafiki kati yao umekuwa ni suala la kuhisiwa zaidi kuliko kuthibitishwa nao hadharani,
baadhi ya watu waliamini sio rahisi kwa Kikwete kumtosa Lowassa, na kinachotajwa kama
tofauti kati yao ni sehemu tu ya mkakati wao.

Wakati safari ya urais wa Lowassa ilichangiwa zaidi na jina lake kutajwa kuwa mrithi wa
Kikwete kwa muda mrefu kuliko mwanasiasa mwingine yeyote yule, kada aliyeendesha kampeni
zake kwa umahiri mkubwa ni January. Awali, alipotangaza nia, takriban mwaka mmoja kabla ya
CCM kuanza rasmi mchakato wa kumpata mgombea wake, baadhi ya watu walidhani kuwa
hakuna na dhamira ya dhati, na pengine anamsafishia njia mgombea mwingine. Hata hivyo, kadri
siku zilivyokwenda, na licha ya kebehi za mara kwa mara alizokumbana nazo, mwanasiasa huyo
kijana alionekana kutotetereka katika dhamira yake.

Baadaye, January alichapisha visheni yake aliyoiita Tanzania mpya, ambayo kwa kiwango
kikubwa ilibainisha matatizo yanayoikabili nchi yetu na namna ya kuyatatua. Kampeni ya
January ilifanikiwa zaidi kutokana na mambo makuu mawili, kwanza, ukaribu aliojenga na vijana
hususan katika mitandao ya kijamii, na pili, kuwa mtu anayefikika (approachable) na wengi. Licha
ya sababu hizo mbili, mwanasiasa huyo kijana amejaaliwa kipaji cha kuongea lugha inayoeleweka
kirahisi kwa mtu wa rika na kada yoyote. Jinsi alivyouza ajenda yake ya Tanzania mpya
iliwafanya watu wengi kumwelewa na pia kumsaidia kupata ufuasi mkubwa. Sambamba na hilo,
wasanii kadhaa walionekana kumuunga mkono na hiyo ilisadia kuwavuta wafuasi wa wasanii hao
kumkubali mwanasiasa huyo, msaidizi wa zamani wa Rais Kikwete na mtoto wa Katibu Mkuu wa
zamani wa CCM.
48

Lakini mchakato huo wa CCM kumpata mgombea wake uliambatana na vituko pia, kikubwa
kikiwa uamuzi wa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwania
nafasi hiyo. Miezi machache tu kabla, jina la mwanasiasa huyo msomo lilivuma mno kufuatia
kashfa ya Tegeta Escrow ambayo hatimaye ilipelekea kujiuzulu licha ya awali kudai kuwa
asingefanya hivyo. Lakini pengine hata kama Profesa Muhongo asingehusishwa na kashfa hiyo,
Watanzania wengi walikuwa wanamkumbuka kwa kauli yake kuwa uwezo wa Watanzania
kuwekeza unaishia kwenye juisi na matunda. Alisema hayo alipoombwa na taasisi moja asitishe
zoezi la kutoa vitalu vya gesi asilia kwa wageni hadi sera ya gesi na mafuta iwe tayari ili kuwezesha
Watanzania nao kuingia ubia au kushiriki umiliki wa uchumi wa gesi. Wengi walijiuliza, hivi
huyu mtu ambaye majuzi tu kulazimika kujiuzulu kwa kashfa ya Tegeta Escrow, amepata wapi
ujasiri wa kuwania urais? Ni katika mazingira kama hayo, hoja kwamba kujitokeza kwa wana-
CCM wengi kuwania urais imechangiwa na thamani ya urais kushuka ilionekana kupata nguvu.

Kingine kilichojitokeza wakati wa kampeni za makada mbalimbali wa CCM kuwania urais ni


matumizi ya mitandao ya kijamii. Kama kuna suala moja litakaloingia kwenye historia ya uchaguzi
mkuu nchini Tanzania basi ni hili la jinsi matumizi ya teknolojia ya kisasa, hsusan mitandao ya
kijamii, yalivyowezesha ushirikishwaji wa kisiasa kwa wananchi wengi, wanasiasa waliokuwa
wakiwania kuteuliwa kuwa wagombea urais na wananchi wa kawaida kwa ujumla.

Kwa mara ya kwanza, wananchi waliokuwa mtandaoni walipata fursa ya kuwahoji wanasiasa hao,
sambamba na wao kutumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania mikakati yao iwapo wangepewa
ridhaa na chama hicho kuwa wagombea. Kwa bahati mbaya, kwa kiasi kikubwa suala hili
halijapewa uzito mkubwa, labda pengine kutokana na ukweli kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa
mitandao ya kijamii hawachukulii mambo ya mtandaoni kwa uzito mkubwa. Hisia kuwa
Watanzania wanaotumia mtandaoni ni asilimia ndogo tu ya Watanzania wote imekuwa kigezo
muhimu kwa watu wengi kutoyachukulia yanayojiri mtandaoni kwa uzito unaostahili. Hata hivyo,
ukweli kwamba wanasiasa kadhaa walitambua umuhimu wa teknolojia hiyo kuwasiliana na
wananchi unaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua ya kuridhisha katika matumizi ya teknolojia
ya mawasiliano.
49

Suala jingine muhimu kabisa ni idadi ya wanawake waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM kuwania
urais, ambapo makada sita wa kike walijitokeza. Makada hao ni Dkt Mwele ,Malecela, Dkt Asha-
Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, Monica Mbega, Ritha Ngowi na Hellena Elinawinga.
Kujitokeza kwa idadi hiyo ya kuridhisha ya wanawake kulijenga hisia kuwa iwapo Tanzania
haitopata Rais mwanamke basi kuna uwezekano mkubwa wa kupata mgombea mwenza, na
pengine hatimaye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa umakamu wa rais.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kwamba kwa kiasi kikubwa makada hao hawakupewa sapoti
ya kutosha na wanawake wenzao, kwenye chama chao na hata mtaani. Hii ni changamoto kubwa
kwa wanawake nchini Tanzania kwa sababu licha ya ukweli kwamba uongozi ni suala la uwezo
lakini jamii nyingi duniani, hususan Barani Afrika, zimekuwa zikikandamiza nafasi za wanawake
katika uongozi, na hii ilikuwa fursa nzuri kwa wanawake wa Tanzania kuwasapoti wanawake
wenzao.

Hatimaye, Julai 2,2015 zoezi la kusaka wadhamini na kurejesha fomu za kuwania ridhaa ya CCM
kumteua mgombea wake wa urais lilifikia ukingoni na makada walioweza kurejesha fomu
walifanya hivyo. Kilichosubiriwa kwa hamu kilikuwa uamuzi wa vikao vya chama hicho tawala
kuchuja wagombea wake na hatimaye kumpata mmoja atakayekiwakilisha chama hicho katika
uchaguzi mkuu.

Mara baada ya kikao cha kwanza, cha Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM kumaliza kikao
chake, kulisikika uvumi kuwa jina na Lowassa halikupitishwa. Uthibitisho sahihi kuhusu tetesi
hizo ulipatikana Julai 11, 2015 baada ya chama hicho kutangaza rasmi majina matano ya makada
wake waliopitishwa, na ambayo yangepigiwa kura katika Mkutano Mkuu wa CCM. Taarifa za
kukatwa kwa jina la Lowassa zilizokelewa kwa mshtuko mkubwa, na wakati fulani zilisikika tetesi
kuwa wafuasi wa Lowassa walipanga kufanya mapinduzi ya kumngoa Kikwete na Kamati Kuu
ya Chama hicho. Baadhi ya wafuasi hao, walijitokeza hadharani kupinga maamuzi ya chama
chao kukata jina la mwanasiasa huyo.

Taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa marais wa zamani, Mwinyi na Mkapa walifanya kazi kubwa
kumnusuru Kikwete na uhai wa chama hicho kwa ujumla kwa maelezo kwamba kanuani na
50

taratibu za chama hizo ziwekwe mbele ya maslahi ya mtu mtu binafsi (Lowassa). Inadaiwa Mkapa
alikwenda mbali na kuwatakia wajumbe wa vikao hivyo wanaodhani kuwa Lowassa hakutendewa
haki aidha warejeshe kadi zao za uanachama wa CCM, kwa maana ya kujiondoa wenyewe kwenye
chama hicho, au waafiki maamuzi ya vikao hivyo.

Makada watano waliopitishwa ni pamoja na Magufuli, Membe, January, Dkt Asha-Rose na


Balozi. Katika hatua ya kwanza ya kura kwa wagombea hao ili kupata majina matatu, Magufuli,
Balozi Amina na Dkt Asha-Rose waliibuka na ushindi. Tetesi zinaeleza kuwa kwa vile kambi ya
Lowassa iliamini kuwa Membe ndio chaguo la Kikwete, na January alionyesha upinzani mkubwa
kwa mgombea wao, kura zao nyingi zilielekezwa kwa Magufuli, Dkt Asha-Rose na Balozi
Amina. Katika duru la mwisho, Magufuli aliibuka mshindi kwa kura 1560, akifuatiwa na Dkt
Asha-Rose alaiyepata kura 70 na Balozi Amina kuambulia kura 349.

Awali kulikuwa na hisia kuwa kwa vile tatu bora ilikuwa na makada wawili wa kike basi huenda
mshindi angekuwa mwanamke pia. Hata hivyo, wachunguzi wa siasa wanadai wakati Dkt Asha-
Rose hakuwa na ushawishi mkubwa wa kumwezesha kusinda nafasi hiyo, kilichomwangusha
Balozi Amina ni hotuba yake ya kuomba kura ambapo alionekana kama anayetaka kura za huruma
kutoka kambi ya Lowassa, sambamba na dalili kuwa huenda angamvuta Lowassa kuwa nae
kama mgombea mwenza endapo mwanamama huyo angeshinda katika kinyanganyiro hicho.

Yayumkinika kuhitimisha kuwa mafanikio ya Magufuli hadi kuteuliwa kuwa mgombea rasmi wa
chama hicho yalichangiwa zaidi na siasa za kumzuwia Lowassa kwa upande mmoja, na hasira
za kambi ya Lowassa dhidi ya Membe. Hata hivyo, kwa kumchagua Magufuli, CCM iliweza
kumpata mgombea ambaye angalau kwa kiasi kikubwa ni mmoja wa watendaji wachache katika
chama hicho wenye kusifika kwa uchapakazi. Tangu jina lake lilipotangazwa rasmi, sambamba na
kada aliyemteua kuwa mgombea mwenza, Samia Suluhu, taswira iliyojitokeza mtaani iliashiria
kuwa chama hicho tawala kisingekuwa na kazi ngumu kumnadi mgombea huyo ambaye licha ya
kusifika kwa uchapakazi, ana kipaji cha kujielezxa kwa ufasaha.

Kwa upande mwingine, sintofahamu ilijitokeza kuhusu hatma ya Lowassa, kada ambaye sio tu
jina lake lilianza kusikika mapema kuwa angewania nafasi hiyo na kujizolea ufuasi mkubwa lakini
51

pia hadi muda huo alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu zaidi ndani na nje ya chama hicho. Swali
kubwa lililotawala vichwa vya Watanzania liligeuka kutoka atakatwa au hatakatwa (na vikao vya
mchujo vya CCM) na kuwa atahama CCM au atabaki katika chama hicho (hasa ikirejewa kauli
zake za awali kuwa wanaomtaka atoke katika chama hicho watoke wao na sio yeye).

Hatimaye, Julai 28, 2015, takriban wiki mbili baada ya jina lake kukatwa na vikao vya CCM,
Lowassa alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema. Siku chache baadaye, vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vilimpitisha Lowassa kuwa mgombea
wao wa nafasi ya urais.

Katika kuhitimisha sura hii, ni muhimu kupigia mstari jinsi ushindi wa Magufuli, na kushindwa
kwa Lowassa, kulivyoenda kinyume na ubashiri wa wachambuzi mbalimbali wa siasa za Tanzania,
ikiwa ni pamoja nami mwandishi wa kitabu hiki. Kwa upande wangu, nilibashiri uwepo wa
makundi makuu matatu ambayo yangeweza kuzaa mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Makundi
hayo ni, kwanza, makada wenye nafasi kubwa, ya kati na wenye nafasi ndogo.

Katika kundi la kwanza Katika kundi la kwanza ninawaweka Jaji Ramadhan, Lowassa, January,
Makongoro, Dkt Bilal, Pinda na makada watatu wanawake, yaani Dkt Mwele, Dkt Asha-Rose na
Balozi Amina.

Jaji Ramadhani aliingia kundi hilo kutokana na sababu za wazi. Ushahidi wa kimazingira wakati
huo ulionyesha kama ndio alikuwa mgombea turufu kwa CCM, hasa katika kile kilichotajwa
kama kumdhibiti Lowassa. Pia kulionekana dalili kuwa Jaji huyo Mkuu mstaafu alikuwa chaguo
la Kikwete kwa kurejea baadhi matamshi yake huko nyuma. Kadhalika, uhaba wa makada wa
CCM wenye rekodi ya kupendeza japo kidogo ulimfanya Jaji Ramadhani kuonekana mwenye na
nafasi ya juu zaidi.

Kuhusu Lowassa, sababu mbili zilizopelekea kuingizwa kundi hilo la kwanza ni, kwanza, historia
yake na Kikwete, angalau hadi wakati huo. Mtizamo maarufu wakati huo ulikuwa kwamba laiti
sakata la Richmond lisingetokea na Lowassa kulazimika kujiuzulu, basi muda huo ingekuwa
inasubiriwa kutawazwa kwake tu, yaani kupasisha utawala kwa mtu pasi haja ya uchaguzi.
52

Mengi ya yalikuwa yakisemwa kuhusu uhusiano wake na Kikwete hayakuwahi kuthibitishwa,


lakini iliyumkinika kuhisi kuwa kadri Lowassa alivyomsaidia Rais Kikwete mwaka 2005 ndivyo
Kikwete alivyotarajiwa kulipa fadhila mwaka huu.

Sababu ya pili ilikuwa uwezo wake mkubwa kifedha ambao kwa kiasi kikubwa ulichangia kile
kilichoonekana kama kukubalika kwake kwa wananchi wengi. Ilikuwa muhimu sana kutopuuza
nafasi ya fedha katika kinyanganyiro hicho hasa kwa kuwa chaguzi nyingi za CCM hutawaliwa
mno na nguvu ya fedha kiasi hata uchaguzi wa viongozi wa chipukizi wa chama hicho uliwahi
kuhusishwa na matumizi makubwa ya fedha.

Kwa upande wa January, aliingia katika kundi hili kwa sababu kuu mbili. Kwanza, alikuwa kada
wa kwanza kutangaza hadharani nia yake ya kuwania urais. Hatua hii ilionekana kumsaidia sana
kutambulika kwa watu wengi hususani miongoni mwa vijana wanaotumia mitandao ya kijamii.
Sambamba na hilo, kada huyo kijana alijizolea ufuasi mkubwa miongoni mwa wasanii maarufu
na wenye mashabiki wengi ambao licha ya kumsapoti pia walikuwa wakimnadi hushusan katika
mitandao ya kijamii.

Sababu ya pili ilikuwa nguvu kubwa mno aliyotumia kujinadi. Licha ya kuandika kitabu
kinachoelezea ajenda yake ya Tanzania Mpya, mwanasiasa huyo alifanya kazi kubwa ya
kujinadi, huku akisaidiwa na wasanii kadhaa wenye majina makubwa. Kimsingi, kada mwingine
pekee anayelingana na Makamba kwa kampeni kubwa alikuwa Lowassa, ambaye hata hivyo,
tofauti na Makamba, alikuwa akifanyiwa zaidi kampeni hizo na wapambe kuliko yeye
mwenyewe.

Kuhusu Makongoro, kikubwa kinachomwingiza Makongoro katika kundi hili ni ukweli kwamba
yeye ni mtoto wa Nyerere, na takribani kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu bado anamlilia
Mwalimu Nyerere. Kwa kuwa mtoto wa Baba wa Taifa, kulikuwa na hisia kwamba tunaweza
kumpata Nyerere mwingine, jambo ambalo ilikuwa kama ndoto njema ya Watanzania wengi.

Lakini kingine ni ukweli kuwa Makongoro alikuwa muwazi mno katika kuikosoa CCM, na
alijitahidi sana kutotoa ahadi kwa kigezo kuwa ahadi za mgombea wa chama hicho shurti ziendane
na ilani ya uchaguzi ya chama hicho ambayo ilikuwa haijatolewa hadi muda huo.
53

Kuhusu Bilal na Pinda, kitu pekee kilichofanya waingie katika kundi hilo ni ukweli kwamba
walikuwa wasaidizi wa karibu wa Rais Kikwete katika miaka 10 iliyopita. Kwa taratibu zisizo
rasmi katika siasa za Afrika, hakuna Rais anayemaliza muda wake atakayethubutu kumkabidhi
madaraka kwa mtu asiyemjua, na Kikwete na makada hao walikuwa wakijiuana vizuri kutokana
na ukaribu wao kikazi. Kadhalika, Uzanzibari wa Bilal ulitarajiwa kuwa mtaji kwake pia iwapo
ingeamuliwa na CCM kuwa mgombea wake ajaye wa urais ajaye Zanzibar.

Kwa Pinda, mara kadhaa alionekana kubebeshwa lawama katika masuala ambayo pengine
lawama zilipaswa kwenda kwa bosi wake, yaani Rais Kikwete. Ilidhaniwa kwamba kwa kukubali
kurushiwa risasi ili kumkinga Rais wake, huenda Kikwete angelipa fadhila kwa kumnadi awe
mrithi wake.

Kwa upande wa makada watatu wanawake, niliwapa nafasi sawa Dkt Mwele, Dkt Asha-Rose na
Balozi Amina kutokana na kila mmoja kuwa na turufu zake. Kwa Dkt Mwele, licha ya
kuendesha kampeni yake kistaarabu sana, alikuwa na faida ya kuwa mgeni katika siasa, kwa
maana isingikuwa rahisi kuhusishwa na mapungufu yaliyoelekezwa kwa makada wengine
waliokwishashika nyadhifa katika chama hicho. Kwa Migiro, ilitarajiwa kuwa wasifu wake kama
mmoja wa wanawake wachache wenye nguvu katika ngazi za juu za chama hicho, na wadhifa
wake wa zamani kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ungeweza kumsaidia.

Kwa Balozi Amina, turufu zake ilitarajiwa kuwa Uzanzibari wake, utumishi wake wa muda
mrefu katika taasisi za kimataifa, na ukweli kwamba hilo lilikuwa jaribio lake la pili kwania fursa
hiyo.

Kundi la pili lilijumuisha makada walioonekana kuwa na nafasi ya kati. Binafsi, nilibashiri kuwa
kundi hilo lingeweza kutoa surprise candidate angalau kuingiza kwenye tano bora, na nilikuwa
sahihi kwani Magufuli alitoka kwenye kundi hilo, kada ambaye licha ya kutanguliza maslahi ya
taifa mbele ya itikadi za kisiasa, alikuwa akisifika kwa uchapakazi. Pamoja na Magufuli, kada
mwingine katika kundi hilo alikuwa na Membe, ambaye tetesi zilikuwa zikidai kuwa alikuwa
akiungwa mkono na familia ya Kikwete, sambamba na ukweli kuwa nafasi yake ya Uwaziri wa
Mambo na Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilimweka karibu sana na mkuu huyo wa nchi. Hata
54

hivyo, licha ya awali kupewa nafasi ya kutoa upinzani mkali kwa Lowassa, kauli zake angalau
mara mbili kuwa angekuwa tayari kumuunga mgombea mwingine endapo yeye asingepitishwa
zilitoa taswira kuwa huenda alishajikatia tamaa.

Mwigulu aliingia katika kundi hilo kutokana na ukweli kwamba kulinganisha na watangaza nia
wengine, alikuwa na rekodi ya kipekee katika kupambana na vyama vya upinzani..

Kada wingine alikuwa Balozi Mahiga, ambaye licha ya kuwa mwanadiplomasia wa kimataifa kwa
muda mrefu aliwahi pia kuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Tatizo kwa Balozi Mahiga
lilikuwa kutojulikana sana katika medani za siasa za Tanzania, na japo ukweli kuwa aliwahi kuwa
bosi wa mashushushu ulitarajiwa kumsaidia kama mgombea mwenye uwezo wa kukabiliana na
tatizo la ufisadi, lakini pia ilidhaniwa kuwa sifa hiyo ingeweza kumkwamishwa na waliohofia
kuwa na rais shushushu.

Mwingine katika kundi hilo alikuwa Profesa Mwandosya, mmoja wa makada waliojaribu bila
mafanikio kuchuana na Kikwete katika kinyangaanyiro cha CCM kumpata mgombea wake
mwaka 2005. Hata hivyo, nguvu aliyokuwa nayo wakati huo ilikuwa imepungua sana kulinganisha
na mwaka huu.

Kundi la tatu lilijumuisha makada wengine wote waliochukua fomu kuwania ridhaa ya chama
hicho tawala kuwateua kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Katika kundi
hili kulikuwa na wanasiasa kama Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye ambaye aliingia kundi hili
kwa sababu tayari alikuwa na maadui wengi ndani ya CCM, hivyo ni ingekuwa vigumu mno
kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho. Baadaye Sumaye alitangaza kuhama chama hicho na
kujiunga na UKAWA, na suala hilo litajadiliwa kwa kirefu katika sura ijayo.

Makada wengine, kama Ngeleja na Profesa Muhongo, waliingia katika kundi hilo la wagombea
wenye nafasi finyu kutokana na ukweli kwamba hadi muda huo majina yao yalikuwa
yakifahamika zaidi kuhusiana na skandali kuliko utendaji kazi wao. Kwa upande wa Dk.
Mwakyembe na Sitta, nafasi zao zilionekana kuwa finyu kutokana na kilichotajwa mara kadhaa
kuwa na uhasama wake na Lowassa ambao ulitarajiwa ungepelekea upinzani mkali dhidi yao.
55

Moja ya mambo ambayo hadi leo hjayajapatiwa majibu ni jinsi Jaji Ramadhan alivyoishia
kukatwa jina lake licha ya kupewa nafasi kubwa kama mtu pekee anayeweza kupambana na
Lowassa. Kimsingi, uamuzi wake wa kutangaza nia ya kugombea urais uliwashtua wengi hasa
ikizingatiwa kuwa rekodi yake safi kama Jaji Mkuu wa zamani, afisa wa zamani wa ngazi ya juu
jeshini, na kiongozi wa kidini, ingeweza aidha kuchafuliwa wakati wa kampeni au kuingiza doa
iwapo jina lake lingeishia kukatwa. Kwa bahati mbaya, Jaji Ramadhan anaweza kukumbukwa
zaidi kwa kutamani urais lakini jina lake halikupitishwa, kuliko rekodi yake ya kuvutia.

Kwa hitimisho, sura hii imezungumzia kwa undani mchakato wa Chama cha Mapinduzi CCM
kumpata mgombea wake, masuala kadhaa yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya chama hicho
kuruhusu makada wake kuwania nafasi hiyo, na jinsi vikao vya chama hicho vilivyowexza
kumpitisha mgombea wao, Magufuli. Vilevile, suura hii, imetengeneza mazingira mazuri ya
kuzungumzia mchakato wa UKAWA kumpata mgombea wao, Lowassa, ambaye kujiunga nao
kulitokea baada ya jina la mwanasiasa huyo kuchujwa na vikao vya CCM, na hatimaye kuamua
kuhama.
56

SURA YA NNE: Mchakato wa UKAWA kupata mgombea wake wa kiti cha urais

Sura hii inazungumzia mchakato wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), unaoundwa na


Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kupata mgombea wake. Kama ilivyokuwa katika sura
iliyotangulia iliyojadili mchakato wa CCM kupata mgombea wake, inatarajiwa kuwa uchambuzi
unaofanyika katika sura hizi mbili utawezesha sura ijayo kuwa katika nafasi nzuri ya kujadili fursa
na na vikwazo kwa CCM na UKAWA kushinda uchaguzi mkuu ujao.

Mwishoni mwa mwezi Februari, mwaka jana 2014 viongozi wa vyama vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD walitangaza kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananichi, kwa kifupi
UKAWA, lengo likiwa kudhibiti kile vyama vya Upinzani walichokiita jitaihada za CCM
kuchakachua rasimu ya Katiba Mpya.

Akieleza malengo ya umoja hu, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba
alieleza chombo hicho kingesaidia kukabiliana na misimamo ya CCM na matamshi ya serikali
katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya uliokuwa ukiendelea katika Bunge Maalum la Katiba,
jijini Dodoma. Alieleza kuwa umoja huo unaundwa na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na wajumbe wa
Bunge hilo Maalum la Katiba walioteuliwa na Rais kutoka taasisi na makundi mbalimbali.
Alibainisha kuwa malengo ya kuundwa kwa umoja huo ni pamoja na kutetea rasimu ya katiba
kama ilivyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, sambamba na kuiboresha rasimu hiyo
kwa kuzingatia maoni ya wananchi na si kuchakachuliwa na CCM na makundi mengine.

Kwahiyo, kimsingi, asili ya UKAWA haikuwa ushirikiano kwenye uchaguzi mkuu, japokuwa
suala hilo limekuwa likitajwa mara kadhaa kuwa ndio kikwazo kikuu cha uwezekano wa vyama
vya upinzani kuingoa CCM madarakani. Hata hivyo, pamoja na ushirikiano wao, uchache wao
kwenye Bunge hilo Maalum la Katiba, na wingi wa wajumbe wa CCM na washirika wake
ulipelekea Umoja huo kutofanikiwa kuizuwia CCM kutekelezwa matakwa yake. April, 2014,
takriban miezi mawili baada ya kuundwa, wajumbe zaidi ya 200 wa UKAWA katika Bunge hilo
walilazimika kususisia vikao vya Bunge hilo, katika kile kilichoelezwa na Profesa Lipumba kuwa
wasingeweza kuendelea na dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba iliyo kinyume na
57

matakwa yao. Hadi Bunge hilo lilipovunjwa rasmi Oktoba mwaka huo, hakukuwa na mwafaka
uliopatikana katika ya UKAWA na CCM, na chama hicho tawala kikitumia wingi wa idadi ya
wajumbe wake kilifanikiwa kutimiza akidi iliyowezesha kuapatikana kwa Katiba Pendekezwa.

Oktoba 26, 2014, vyama vinavyounda umoja huo viliandika historia mpya baada ya kusaini
makubaliano ya kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na
kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia wakati huo. Makubaliano
hayo ni kama ifuatavyo:

1. Kuhusisha sera za vyama hivyo.

2. Kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi.

3. Vyama husika kutoa utaratibu wa jinsi vitashirikiana katika Uchaguzi wa Serikali za


Mitaa na vijiji mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015.

4. Vyama hivyo kushirikiana kuelimisha umma kuifahamu na kuipigia kura ya hapana


Katiba Pendekezwa.

5. Kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye
masilahi kwa Watanzania.

6. Kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya maslahi.

7. Kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja baina ya vyama hivyo na asasi na


makundi mbalimbali ya Watanzania.

Wakati hatua hiyo ilipokelewa vizuri na wengi waliokuwa na kiu ya kuona upinzani imara wenye
uwezo wa kuingoa CCM, baadhi walidhani kuwa uwezekano wa vyama hivyo kusimama imara
hadi wakati wa uchaguzi mkuu ni hafifu, sababu kubwa zikitajwa kuwa hujuma zilizozoeleka za
CCM dhidi ya vyama hivyo, sambamba na tofauti za kimsingi kisera na kimaslahi baina ya vyama
hivyo.
58

Kwa mfano, kwa muda mrefu kumekuwa na hisia, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa
zikitafsiriwa kama hujuma za CCM dhidi ya vyama vya upinzani, kwamba CUF ni chama cha
kidini (Kiislamu) na Chadema ni chama cha kidini (Kikristo). Kadhalika, tuhuma nyingine dhidi
ya vyama hivyo ni ukabila au ukanda, ambapo tuhuma dhidi ya CUF zimekuwa ni chama cha
Wapemba, ilhali Chadema ikituhumiwa kuwa chama cha Wachagga.

Kwa bahati mbaya, taswira potofu dhidi ya chama cha siasa, hata kama sio za kweli, zinaweza
kujenga mwonekano wa aina hiyohiyo (potofu) kwa jamii. Japo tuhuma hizo za udini na
ukanda/ukabila hazina uzito mkubwa miongoni mwa Watanzania wengi, yayumkinika kuhitimisha
kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyodhaniwa kuwa vikwazo kwa UKAWA kufanikiwa katika
malengo yake.

Lakini kinyume na matarajio ya baadhi ya watu kuwa umoja huo ulikuwa ni moto wa karatasi
tu, kwa maana kwamba usingedumu hadi kipindi cha uchaguzi mkuu, UKAWA ilifanikiwa
kuunganisha nguvu nje ya ajenda iliyowaunganisha ya kudai Katiba mpya.

Mtihani wa kwanza kwa UKAWA ulikuwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014
ambapo vyama hivyo vinne vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja mmoja. Kwa mujibu wa
matokeo, vyama vya upinzani vilipata viti zaidi ya 3,200 huko CCM ikipata viti 9,400. Licha ya
matokeo ya vyama vya upinzani kujumisha vyama ambavyo havimo UKAWA, kama vile TLP na
ACT- Wazalendo, kwa ujumla Upinzani ulipata ongezeko la zaidi ya viti 1,900 kulinganisha na
viti 1,230 vilivypatikana katika uchaguzi wa mwaka 2009. Kwa upande mwingine, CCM ilipoteza
zaidi ya viti 2,600.

Japo hakuna aliyetarajia UKAWA kuibuka mshindi wa jumla dhidi ya CCM lakini mafanikio
yaliyopatikana katika uchaguzi huo sio tu yaliashiria umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa
vyama vyama vya upinzani katika azma yao ya kuingoa CCM bali pia yaliashiria kuingia kwa
zama mpya za siasa za upinzani dhidi ya chama tawala CCM, na pengine ishara ya jinsi hali
ingekuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
59

Kwahiyo, yayumkinika kuhitimisha kwamba UKAWA ilifanikiwa kufaulu mtihani wake wa


kwanza, ambao licha ya kuwa muhimu kuthibitisha kuwa ushirikiano wao ulikuwa wa dhati lakini
pia ungewasaidia kupata imani ya Watanzania kuwa umoja huo unaweza kuwa mbadala wa CCM.

Hata hivyo, badala ya kutumia mafanikio hayo kama chachu ya kushirikiana kwa upana zaidi,
moja ya mapungufu makubwa yaliyojitokeza baada ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa, na
ambayo yanaweza kuugharimu umoja huo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni kile
kilichoonekana kama kila chama kuonekana kuendelea na shughuli zake za kisiasa peke yake
badala ya shughuli hiyo kufanywa kwa pamoja. Japo kulikuwa na nyakati ambapo viongozi wa
vyama hivyo walipanda pamoja majukwaani, ushirikiano wao ulionekana kuwa baina ya viongozi
wakuu zaidi kuliko vyama hivyo na wanachama wake wa kawaida.

Japo hoja mbadala ilikuwa haja ya vyama hivyo kuendelea kujiimarisha kimoja kimoja ili
hatimaye viweze kuimarisha ushirikiano wao, baadhi ya wachunguzi wa siasa za Tanzania
walidhani kuwa mazingira yaliruhusu vyama hivyo kufanya mambo yote mawili kwa wakati
mmoja: kujijenga kama vyama binafsi na wakati Huohuo kujijenga kama UKAWA.

Mapungufu mengine ni ukweli kwamba maamuzi ya ushirikiano huo yalifanywa na viongozi


wakuu wa vyama hivyo pasi kuwashirikisha kwa kiasi kikubwa wanachama wa kawaida. Japo
suala hilo halikupelekea vurugu au upinzani ndani ya vyama husika, baadhi ya wachambuzi
walipatwa na hofu kwa kigezo cha umoja wowote wa vyama unaoonekana kuwa wa viongozi tu
pasi ushiriki wa wanachama wa kawaida unaweza kuwa na matatizo mbeleni. Hata hivyo, hadi
muda huu wakati ninaandika kitabu hiki, hakujakuwa na upinzani mkali ndani ya vyama husika
dhidi ya wazo hilo. Zaidi, wanachama wengi wameonekana kuunga mkono wazo hilo na kwa kiasi
kikubwa limewapa matumaini ya kuona umoja huo ukiingoa CCM.

Kwa upande mwingine, wakati Watanzania wengi wakiwa na kiu ya kusikia kuhusu maandalizi
ya UKAWA kwa ajili ya uchaguzi mkuu, umoja huo ulihamishia nguvu zake kwenye kutoa
elimu ya uraia sambamba na kusimamia uandikishwaji kwenye daftari la wapigakura, na kwa
wengi, umoja huo ulionekana kama unapuuzia kujinadi, hasa ikizingatiwa bado kulikuwa na
mkanganyiko kuhusu mchakato wao wa kupata wagombea katika nafasi mbalimbali katika
60

uchaguzi mkuu. Sambamba na hilo, UKAWA ilipaswa kufanya kazi ya ziada kuwaelimisha
Watanzania kuhusu umoja wao ili kuepuka mkanganyiko kwa wapiga kura, ambao ungeinufaisha
CCM.

Kimsingi, vyama vyote vinne vilikuwa vikitambua fika kuwa nafasi pekee waliyonayo ya
kujitengenezea mazingira mzuri ya kuipiku CCM ni kipindi ambacho chama hicho tawala
kitakuwa vitani katika mchakato wake wa kupata mgombea wake. Lakini, kadri siku zilivyokuwa
zinazidi kupita ndivyo shutuma zilivyozidi kuanza kujitokeza dhidi ya UKAWA kwa ukimya wao
kuhusu mikakati yao ya ushiriki katika uchaguzi mkuu, hususan kushindwa kutangaza mgombea
wao wa nafasi ya urais.

Kwa vile kulikuwa na uwezekano mkubwa wa UKAWA kutokuwa na idadi kubwa ya wanachama
wanaotaka kuwania nafasi ya urais, hasa kwa kuzingatia historia ya vyama vya upinzani nchini
Tanzania ambapo katiak chaguzi zote zilizotangulia kulikuwa na idadi ndogo tu ya wanachama
waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama husika, ilitarajiwa
kuwa zoezi la umoja huo kumpata mgombea wake lingechukua muda mfupi, na muda uliosalia
ungetumika kumnadi mgombea huyo, sambamba na kuutangaza vema Umoja huo hasa katika
maeneo ya vijijini.

Badala yake kila chama kilionekana kama kinaendelea na ajenda binafsi, na suala la umoja huo
kuja na mgombea wake mmoja kuonekana kama kitendawili. Hata hivyo, matarajio makubwa
yalikuwa kwa umoja huo kumpitisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Willbrord Slaa,
kuwa mgombea urais, kwa kuzingatia matokeo yake ya kuridhisha katika uchaguzi mkuu uliopita
ambapo alishika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa CCM, Rais Kikwete.

Baada ya kimya kirefu, Profesa Lipumba alitangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya UKAWA
kupitia chama chake cha CUF, akiwafuatia Mwenyekiti wa NLD Emmanuel Makaidi na Dkt
George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi waliotangaza nia zao awali. Suala hilo lilionekana kuzua
mkanganyiko kwa waliokuwa wakifuatilia maendeleo ya UKAWA, kwani awali ilitarajiwa kuwa
badala ya kila chama kutangaza mgombea wake, Umoja huo ungemtangaza mgombea mmoja
kutoka miongoni mwao. Lakini wakati viongozi hao wa CUF, NLD na NCCR-Mageuzi
61

wakitangaza nia, ukimya mkubwa uliigubika Chadema, chama kikuu cha upinzani kwa kuzingatia
matokeo yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Lakini pamoja na ukimya huo, tetesi
ziliendelea kuonyesha uwezekano mkubwa wa chama hicho kumpitisha tena mgombea wake
katika uchaguzi mkuu uliopita, Katibu wake Mkuu, Dkt Slaa.

Wakati Watanzania wengi wakidhani ukimya huo wa UKAWA ulikuwa dalili za awali kwamba
vyama vinavyounda umoja umoja huo haviwezi kuafikiana kumsimamisha mgombea mmoja
katika nafasi ya urais kwa vile kila kimoja kina maslahi binafsi na kinataka urais, ukweli
uliofahamika baadaye ulibainisha hali tofauti kabisa. Kwa mujibu wa taarifa, wakati vyama
vinavyounda umoja huo vikiendelea na majadiliano ili kumpata mgombea mmoja, kulikuwa na
harakati za chinichini kati ya viongozi Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, na Lowassa,
kuhusu uwezekano wa mwanasiasa huyo wa CCM (wakati huo) kujiunga na umoja huo na
kupatiwa nafasi ya kugombea urais, endapo jina lake lisingepitishwa katika vikao vya mchujo vya
CCM.

Taarifa za kiuchunguzi zilieleza kuwa awali, kulikuwa na mwafaka kuwa Dkt Slaa ndiye awe
mgombea wa UKAWA, baada ya kikwazo kikubwa cha ugombea wake, kutoka CUF, kufanikiwa
kurukwa. Taarifa hizo zilidai kuwa mwanzoni CUF walitaka Profesa Lipumba ndie awe mgombea
wa umoja huo, lakini baada ya majadiliano ya muda mrefu, iliafikiwa kuwa Dkt Slaa alikuwa
katika nafasi ya kufanya vizuri zaidi laiti angeteuliwa kuwa mgombea urais wa UKAWA kwa
tiketi ya Chadema.

Dkt Slaa, mwanasiasa aliyejijengea heshima kubwa kutokana na misimamo yake thabiti
sambamba na uwezo mkubwa wa kujenga hoja zenye mantiki, alionekana angeweza kutoa
upinzani mkali kwa mgombea wa CCM hasa ikizingatiwa kuwa sio tu aliibuka mshindi wa pili
nyuma ya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 lakini ugombea wake uliisaida
Chadema kuipiku CUF kama chama kikuu cha upinzani, na kukiwezesha chama chake
kujiongezea idadi ya wabunge kutoka watano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 (ambapo
mgombea wake katika nafasi ya urais alikuwa Mbowe) hadi 23, ongezeko la asilimia 460.
62

Kadhalika, kura mbalimbali za maoni zilionyesha kuwa Dkt Slaa alikuwa akifanya vizuri kuliko
wanasiasa wengine, ndani na nje ya vyama vya upinzani, huku angalau kura moja ya maoni
ikimwonyesha kuwa mbele ya Lowassa ambaye takriban kila kura ya maoni ilionyesha anaongoza
katika kipengele cha nani anafaa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015.

Taarifa zaidi zinaelezwa kuwa mara baada ya maafikiano kuwa Dkt Slaa ndiye awe mgombea wa
UKAWA, Mbowe alishauri taarifa hiyo kutotangazwa rasmi kwa madai kuwa kulikuwa na
mwanasiasa mwenye jina kubwa kutoka CCM aliyekuwa anatarajia kujiunga na umoja huo. Hadi
wakati huo, haikuwekwa rasmi kuwa mwanasiasa huyo kutoka CCM ni Lowassa, na kwamba
ndiye angekuja kuteuliwa kuwa mgombea wa umoja huo badala ya Dkt Slaa.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa baadaye na Dkt Slaa baada ya kujitenga na Chadema, hata
ilipowekwa bayana kuwa Lowassa angejiunga na UKAWA, maafikiano yalikuwa apitie taratibu
zinazoongoza vyama hivyo kabla ya kumfikiria kuwa mgombea urais, jambo ambalo
halikutekelezwa.

Julai 28, 2015 Lowassa alitambulishwa rasmi kwenye mikutano na waandishi wa habari
uliohudhuriwa na viongozi wakuu wa UKAWA (lakini Dkt Slaa hakuwepo), na baadaye alipatiwa
kadi ya uanachama wa Chadema. Siku chache baadaye, Lowassa alipitishwa na chama hicho kuwa
mgombea wake wa kiti cha urais akiwakilisha UKAWA., na Juma Haji Duni alilazimika kuhamia
Chadema kutoka CUF ili awe mgombea mwenza.

Wakati uamuzi huo wa Chadema kumpokea Lowassa na kumpitisha kuwa mgombea wake kwa
tiketi ya UKAWA ulipokelewa kwa shangwe kubwa na wafuasi wengi wa chama hicho, kundi
dogo lilionekana kutoafikiana na hatua hiyo, ikiwa ni pamoja na Dkt Slaa. Katika mazingira ya
kawaida tu, ilionekana kama kichekesho kwa chama hicho kumpokea mwanasiasa ambaye
walikuwa wakimwandama tangu ilipoibuliwa kashfa ya Richmond mwaka 2006. Baadhi ya watu
walihoji Chadema itawezaje kumnadi Lowassa baada ya kumchafua kwa muda mrefu
wakimtuhumu kwa ufisadi.

Lakini licha ya upinzani huo kutoka ndani ya Chadema, baadhi ya wananchi wasiojihusisha na
chama hicho walioanza kupata matumaini kuwa chama hicho sio tu msemaji wao sahihi wa kero
63

mbalimbali zinazowakabili, hususan ufisadi, walitafsiri hatua ya kumpokea Lowassa kama usaliti
kwa sababu ilikuwa ni wazi kuwa chama hicho kisingeweza kusimamia ajenda yake kuu ya
kupinga ufisadi ambayo ilikisaidia mno kupata umaarufu, kukubalika na kuaminiwa na
Watanzania wengi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, baada ya kimya kirefu na taarifa za kukanganya kuhusu ukimya wake,
Dkt Slaa aliongea na vyombo vya habari na kubainisha kuwa aliamua kujiweka kando kutokana
na kutoridhishwa na mchakato mzima wa kumpokea Lowassa na baadaye kumpitisha kuwa
mgombea urais. Katika maelezo yake yaliyovuta hisia za wengi, Dkt Slaa alikiri kushiriki katika
mchakato wa kumpokea Lowassa, lakini alibainisha kwamba kuna masuala kadhaa ambayo
yalikiukwa katika makubaliano ya awali. Miongoni mwa makubaliano hayo ni Lowassa kutoa
maelezo ya kuridhisha kuhusu uhusika wake katika kashfa ya Richmond, sambamba na uthibitisho
wa ahadi ya ujio wa viongozi kadhaa kutoka CCM kujiunga na Chadema. Katibu huyo Mkuu wa
Chadema alieleza kwamba hadi Lowassa anapitishwa kuwa mgombea urais, ahadi ya ujio wa
viongozi kutoka CCM ilionekana kuwa kama ahadi hewa kwani makada wachache waliohama
CCM na kumfuata Chadema hawakuwa mtaji wa maana kwa chama hicho kikuu cha upinzani.

Kilichofuatia baada ya mikutano huo wa Dkt Slaa ni mlolongo wa vituko ambavyo wiki chache tu
kabla ingekuwa vigumu kuamini vingeweza kutokea. Uongozi wa Chadema na UKAWA kwa
ujumla, pamoja na wanachama na mashabiki wao mbalimbali, walifanya kila jitihada kujenga
taswira kwamba Dkt Slaa ni mnafiki kwa vile alishiriki mchakato wa kumpokea Lowassa, na
sababu kuu ya yeye kujiweka kando ni uroho wa madaraka uliochochewa zaidi na mwenza wake,
Josephine Mushumbusi.

Lakini kwa vile sakata hilo lilionekana kuwa habari njema kwa CCM huku baadhi ya viongozi
na wafuasi wake wakimpongeza Dkt Slaa kwa kuwa mkweli, wana-Chadema na UKAWA
walitumia hali hiyo kudai kuwa kiongozi huyo wa zamani ni kibaraka anayetumiwa na CCM.
Kwa takriban wiki nzima tangu aongee na vyombo vya habari, Dkt Slaa alikumbwa na mafuriko
ya pongezi na shutuma, pongezi kutoka kwa viongozi na wafuasi wa CCM na watu wengine
waliomwona kama mwanasiasa mwenye msimamo thabiti, na shutuma kutoka kwa viongozi na
64

wafuasi wa Chadema na UKAWA waliomwona kama kibaraka anayetumiwa na CCM kukwaza


dhamira ya kuingoa CCM madarakani.

Siku chache baadaye, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba, naye alitangaza kujiuzulu wadhifa
huo huku akiahidi kubaki mwanachama wa kawaida wa chama hicho. Mwanasiasa huyo alieleza
kuwa alilazimika kujiuzulu kutokana na kukerwa na UKAWA kushindwa kusimamia makubaliano
yalivyopelekea kuundwa kwa umoja huo. Alitanabaisha kuwa umoja huo uliundwa kwa ajili ya
kutetea maslahi ya wananchi katika rasimu ya Katiba mpya yaliyowasilishwa kwenye Bunge
Maalum la Katiba, lakini nafsi yake ilikuwa inamsuta kuona watu waliopinga rasimu hiyo na
jitihada za UKAWA wakikaribishwa kugombea uongozi kupitia umoja huo (akimaanisha
Lowassa, ambaye rekodi zinaonyesha alikuwa mpinzani wa rasimu hiyo.)

Kama ilivyokuwa kwa Dkt Slaa alipotangaza kujiweka kando na shughuli za Chadema, Profesa
Lipumba nae alijikuta akiandamwa na shutuma kali kutoka kwa wafuasi wa UKAWA
wakimshutumua kuwa kibaraka wa CCM mwenye lengo la kukwamisha safari ya mabadiliko ya
kuingoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakati hali haijatulia, akajitokeza Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josphat Gwajima, na
kuongea na wanahabari, ambapo alitumia hotuba yake nzima kumshambulia Dkt Slaa, na
kukanusha tuhuma zake (Slaa) kuwa yeye Gwajima ni miongoni mwa maaskofu waliohongwa
fedha na Lowassa ili wamsaidie katika dhamira yake ya kupata urais. Kiongozi huyo wa kanisa
alikwenda mbali zaidi na kumtuhumu Dkt Slaa na mwenza wake, Josephine, kuwa wanatumika ili
kumkwaza Lowassa na UKAWA.

Hata hivyo, pamoja na sintofahamu hiyo ya Dkt Slaa kujiweka kando na Prof Lipumba kujiuzulu,
hatimaye UKAWA ilifanikiwa kuzindua rasmi kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani jijini
Dar es Salaam na kuhudhuriwa na umati mkubwa, baada ya kulazimika kuahirisha uzinduzi huo
kutokana na mamlaka kuukatalia umoja huo kuutumia Uwanja wa Taifa, hatua iliyotafsiriwa na
wengi kuwa ilikuwa ni hujuma ya CCM dhidi ya UKAWA.

Tangu wakati huo, Lowassa na viongozi wenzie wa UKAWA wamekuwa wakipata maeneo
mbalimbali kuomba ridhaa ya kuingiza Ikulu, huku ujumbe mkuu ukiwa ni mabadiliko. Pamoja
65

na dhana hiyo ya mabadiliko kutobainishwa kwa undani, mtaji mkubwa kwa Lowassa na
UKAWA umekuwa kwenye ukweli kuwa kuna baadhi ya Watanzania wanaotamani kuoina CCM
inangolewa madarakani kwa njia yoyote ile, hata kama ni kwa kumtumia mwana-CCM wa
zamani kama Lowassa, ambaye huko nyuma vyama vya upinzani vilimwandama mno na kumuita
fisadi. Ni katika mantiki hii, hoja kuwa Lowassa ni fisadi iliyotumiwa kwa muda mrefu na
Chadema, na ambayo ilidhaniwa ingeweza kuwa kipingamizi kikubwa kwa mgombea huyo,
imekosa mvuto wa kutosha miongoni mwa wafuasi wa UKAWA, ambao baadhi wamekuwa
wakieleza bayana kuwa bora kumpigia kura shetani achilia mbali mtuhumiwa wa ufisadi
Lowassa kuliko kuipigia kura CCM.

Kadhalika, katika hali inayoweza kuonekana kama mchezo wa kuingiza, makada mbalimbali wa
Chadema ambao huko nyuma walikuwa mwiba mkali dhidi ya Lowassa kuhusu tuhuma za
ufisadi, kwa mfano Tundu Lissu, wamjitokeza hadharani kumtetea mgombea wao huyo wa urais
wakidai kuwa amewaambia ukweli kuhusu Richmondyeye alitolewa kafara tu...na ndio maana
serikali imeshindwa kumchukulia hatua za kisheria.

Ukweli mchungu kwa CCM ni kwamba Lowassa ni zao la mfumo walioulea kwa muda mrefu.
Laiti chama hicho kingetilia mkazo mkakati wake wa kujivua magamba, na kumngoa Lowassa
muda huo (endapo tuhuma dhidi yake zingethibitishwa), basi ni wazi muda huu wasingekuwa na
wakati mgumu kupambana nae. Ni wazi kuwa endapo Lowassa na UKAWA watafanikiwa
kushinda katika uchaguzi huu, basi CCM hawatakuwa na wa kumlaumu isipokuwa kujilaumu wao
wenyewe.

Kwa upande mwingine, bila kujali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakuwaje, ukweli kwamba
UKAWA wamemudu kufikia muda huu wakiwa pamoja, kwa maana ya vyama vyote vinne
vilivyosaini makubaliano kushirikiana, tena kinyume cha matarajio ya wengi waliodhani tmaa na
maslahi binafsi vingefanya ushirikiano wao kuwa ndoto, si tu ni jambo la kupongezwa bali pia ni
ishara ya kukua kwa demokrasia nchini Tanzania. Ni muhimu kutambua nafasi ya vyama vya
upinzani katika mfumo wa siasa, kwa kwa hakika, vyama vya upinzani nchini vimemfanya kazi
kubwa kuiamsha CCM na serikali, sambamba na kupigania maslahi ya wananchi.
66

Kwamba UKAWA ikishinda, kila baya la CCM litaondoka ni kujidanganya. Umoja huo
umekuwa ukiendesha kampeni zake kwa kauli-mbiu ya mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko ni
mchakato wa muda mrefu, wenye kuhitaji kiwango kikubwa cha kujitolea na kujitoa mhanga. Si
kwamba hilo haliwezekani iwapo UKAWA itashinda, lakini ni vema kujiandaa kisaikolojia kwa
kutambua kuwa hata kama kweli dhamira ya mabadiliko itakuwepo iwapo umoja huo utashinda,
halitakuwa jambo la hapo kwa hapo, hasa ikizingatiwa uwepo wa lundo la matatizo ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii.

Kwa hitimisho, sura hii imechambua kwa undani mchakato wa UKAWA kumpata mgombea
wake, kada wa zamani wa CCM, Lowassa, na kutengeneza msingi mzuri wa uchambuzi kuhusu
nafasi na vikwazo kwa umoja huo, kwa upande mmoja, na CCM, kwa upande mwingine, kufanya
vizuri katika uchaguzi mkuu, mada ya sura inayofuata.
67

SURA YA TANO: Nafasi na vikwazo kwa kila upande

Baada ya sura zilizopita kuchambua kwa kina jinsi Tanzania inavyoingia katika uchaguzi mkuu
wa mwaka huu, na jinsi wapinzani wawili wakuu CCM na UKAWA walivyoweza kupata
wagombea wao, sura hii inachambua nafasi na vikwazo kwa wagombea, Magufuli na Lowassa, na
vyama vyao kwa ujumla.

CCM inaingia kwenye uchaguzi huu ikiwa chama tawala, na kanuni isiyo rasmi kuhusu siasa za
Afrika ni kwamba chama tawala huwa hakishindwi uchaguzi, na kikishindwa basi ni matokeo ya
matatizo yake ya ndani kuliko nguvu ya wapinzani wake. Ni kanuni isiyo rasmi kwa sababu si
kweli kwamba katika chaguzi zote za Afrika ni lazima chama tawala kishindo. Hata hivyo, chaguzi
katika nchi nyingi za bara hilo hufanyika katika mazingira yanayovipa vyama tawala nafasi nzuri
ya kuendelea kuwa madarakani.

Moja ya sababu zinazoweza kupelekea chama tawala kushindwa uchaguzi ni uteuzi mbovu wa
mgombea wake. Iwapo chama kitampitisha mgombea asiyekubalika kwa wingi ndani ya chama
husika, kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wafuasi wa chama hicho kumpigia kura mgombea
wa chama kingine, katika kile kinachofahamika katika chaguzi kama kura za chuki. Japo ni
vigumu kubainisha kwa hakika kukubalika kwa mgombea wa chama hicho, Magufuli, kwa kiasi
kikubwa, na angalau kwa mwonekano wa nje tu, anaonekana kupewa sapoti kubwa na viongozi
waandamizi na wa kawaida wa chama hicho pamoja na wanachama na wafuasi wa CCM.

Hata hivyo, kutojitokeza waziwazi kwa Makamu wa Rais, Dkt Billal na Waziri Mkuu, Pinda,
kumezua maswali kwa wanaofuatilia mwenendo wa uchaguzi huo. Kadhalika, kumekuwepo na
tetesi za uwepo wa wasaliti ambao mchana ni mashabiki wa Magufuli/CCM lakini usiku ni
mashabiki wa Lowassa/UKAWA.

Uwezekano pekee kwa CCM na/au Magufuli kupigiwa kura za chuki ni kutoka kwa makada na
wanachama wanaoendelea kumsapoti Lowassa wakiwa ndani ya chama hicho. Ikumbukwe kuwa
hadi alipoamua kuhama chama hicho na kujiunga na Chadema, Lowassa alikuwa mwanasiasa
mwenye nguvu kubwa zaidi ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Kikwete, na wakati fulani, ilielezwa
kuwa anaungwa mkono na idadi kubwa ya viongozi wa chama hicho katika ngazi za mikoa na
68

wilaya, hususan kutokana na kilichoelezwa kuwa misaada yake kwao kushinda katika chaguzi za
ndani za chama hicho.

Jambo jingine linaloweza kukiathiri chama tawala kutomudu kutetea nafasi yake ni mshikamano
hafifu, hasa pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya chama au mgombea wake.
Hili laweza kujitokeza kutokana na mchakato usio huru na haki wa kumpata mgombea wa chama
husika. Mgombea anayesimama mwenyewe ana nafasi ndogo ya kufanya vizuri, angalau katika
mazingira ambayo ni vigumu kumtenganisha chama na mgombea wake. Chama kinachoingia
katika uchaguzi huku baadhi ya viongozi wake wakiweka nguvu kubwa kufikirika hatma zao za
kisiasa badala ya kumuunga mkono mkombea wao kinaweza kushindwa uchaguzi kirahisi. Kwa
kifupi, ili chama kishinde uchaguzi ni lazima kiwe na umoja na mshikamano.

Katika hilo, kumekuwa na tetesi kuwa baadhi ya makada waliopewa jukumu la kusimamia
kampeni za Magufuli na chama kwa ujumla wamekuwa bize zaidi na kuangalia mustakabali wao
baada ya uchaguzi kuliko kuhakikisha chama na mgombea wao wa urais anashinda. Taarifa
zilizopatikana wakati ninaandika kitabu hiki ziliashiria kuwa suala hilo lilikuwa likifanyiwa kazi
na uongozi wa juu wa CCM, japo hakukuwa na uthibitisho wa uwepo wa tatizo hilo au jitihada za
kulishughulikia.

Kwa upande wa CCM, uwepo wake madarakani muda mrefu na uzoefu wake wa kushinda chaguzi
zote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa vyaweza kuwa mitaji muhimu
lakini pasipo umakini vyaweza pia kuwa vikwazo. Kwa kuwepo madarakani muda mrefu,
yayumkinika kuamini kuwa kuna idadi kubwa tu ya wapigakura ambao hawaamini kabisa kuwa
kuna maisha bila CCM. Kwa hao Tanzania ni CCM, na CCM ni Tanzania. Wapigakura wa aina
hiyo hawahitaji kampeni kubwa kushawishiwa waendelee kuipigia kura CCM.

Wengi wa wapigakura wanaoiunga mkono CCM wapo vijijini, ambako pia ndiko kwenye idadi
kubwa ya Watanzania. Katika baadhi ya maeneo, neno chama tu maana yake ni CCM. Na mengi
ya maoneo hayo, tofauti kati ya chama na serikali ni kama haipo. Kwahiyo ni vigumu kwa
wapigakura katika maeneo kama hayo japo kufikiri uwezekano wa uwepo wa nchi yao bila CCM.
69

Lakini mtaji huo wa uwepo wa muda mrefu wa chama hicho tawala una upande wa pili ambao
ni hasi, hususan kukihusisha chama hicho na matatizo lukuki yanayoikabili Tanzania. Mara nyingi,
yanapozungumzwa matatizo ya nchi yetu, CCM imekuwa mhanga mkubwa wa lawama kuhusu
sababu za matatizo hayo.

Japo mabadiliko ya mfumo wa siasa za Tanzania yana umri wa zaidi ya miaka 20 sasa lakini
kimsingi hayajajipenyeza kila kona ya taifa letu, hususan katika maeneo ya vijijini. Katika mengi
ya maoneo hayo, bado kuna vitu vingi vinavyohusiana na CCM, na ambavyo katika nyakati kama
hizi za uchaguzi, vinaweza kuwa na manufaa kwa chama hicho tawala. Kwa mfano, kuna viwanja
na kumbi za burudani ambavyo sio tu vinamilikiwa na chama hicho bali pia vinahusishwa na
uwepo wake. Na katika mazingira yaliyopo ambapo uchaguzi mkuu wa mwaka huu una ushindani
ambao haijawahi kutokea katika historia za chaguzi nchini, kila kitu bila kujali udogo au
umuhimu wake kinachoweza kumkumbusha mpirakura kuhusu chama au mgombea, kina
umuhimu wa kipekee.

CCM na mgombea wake Magufuli wana faida ya wazi ya mfumo uliopo, ambapo chama kina
hatamu zaidi ya serikali. Japo mabadiliko ya sheria iliyoruhusu vyama vingi iliharamisha masuala
ya siasa katika ofisi na taasisi za serikali, kwa kiwango kikubwa hali imeendelea kuwa hivyo, hasa
kutokana na muundo wenyewe wa serikali. Kwa upande mmoja, Rais kama mkuu wa serikali
ndiye pia mwenyekiti wa CCM. Kwa lugha nyingine, madaraka na nguvu zote za rais kama mkuu
wa serikali zinaweza kutumika kwa maslahi ya chama, hasa kwa vile ni vigumu kuchora mstari
unaotenganisha uraia na uenyekiti wa CCM Taifa.

Kwa mfano hai, Rais ndio mlaji (consumer) wa ripoti za kila siku kutoka Idara yya Usalama wa
Taifa. Lakini kwa vile rais huyohuyo ni mwenyekiti wa CCM, ni wazi kuwa anaweza kuzitumia
taarifa hizo, ambazo baadhi zinaelezea mikakati na shughuli za vyama vya upinzani, kwa manufaa
ya chama chake. Tukibaki kwenye taasisi hiyo, Rais ndiye mkuu halisi (sponsor) wa Idara hiyo.
Nafasi hiyo inamruhusu kutoa malelekezo kwa Idara hiyo kuhusu masuala mbalimbali, na anaweza
kutumia fursa hiyo, kwa mfano kuagiza Operesheni fulani, kwa manufaa ya chama chake.
70

Kwa upande mwingine, Rais ana madaraka ya kuwateua wakuu mbalimbali wa taasisi za dola,
akiwa kama Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Katika mazingira ya kawaida tu,
viongozi wa majeshi hayo wana deni la aina flani kutokana na uamuzi wa Rais kuwateua kushika
nyadhifa hizo. Hii inajenga uhusiano binafsi kati ya Rais na watendaji hao, na anaweza kutumia
uhusiano huo kwa manufaa ya chama chake.

Moja ya shutuma za vyama vya upinzani dhidi ya serikali imekuwa ni jinsi taasisi za dola, hususan
jeshi la polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, zinavyotumika kwa maslahi ya chama hicho tawala.
Kwa upande wa jeshi la polisi, mara kadhaa limeonekana bayana kutumia nguvu kubwa
kuwadhibiti viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani huku likiwaonea aibu viongozi na
wafuasi wa CCM. Ni katika mazingira haya, inaaminika kuwa baadhi ya wafanyabiashara
wachafu wameziona CCM kama sehemu inayowapatia kinga, kwa maana ya kutobughudhiwa na
vyombo vya dola.

CCM pia ina faida ya upendeleo katika vyombo vya habari vya umma. Tangu enzi za Radio
Tanzania hadi zama hizi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), vyombo vya habari vya umma
vimeshindwa kabisa kuficha upendeleo wao kwa chama tawala. Pengine kinachopelekea
uepndeleo huo ni gumu wa kutenganisha kofia za kiutendaji, yaani kwa mfano Rais anapofanya
shughuli ya chama kama mwenyekiti wa taifa wa chama tawala bado anabaki kuwa Rais, na
chombo cha habari husika kinawajibika kumhudumia.

Licha ya kuwa na magazeti yake ya Uhuru na Mzalendo, CCM imekuwa ikinufaika pia kutokana
na kile kinachoonekana machoni mwa wengi kama upendeleo katika magazeti ya serikali, Daily
News na Habari Leo, ambayo kimsingi yalipaswa kutoelemea upande wowote.

Kimsingi, muundo wa serikali ambapo Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu, Manaibu Waziri, na
baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ni makada wa chama tawala, unaifanya serikali kuwa na
uhusiano wa kutegemeana na chama tawala. Na hata kama watendaji hao wa serikali wakiamua
kutoingizwa siasa katika majukumu yao, bado kuna uwezekano wa walio chini yao kudhani
utumishi wao serikalini unahusiana na chama tawala.
71

Kwenye suala zima la uchaguzi, licha ya Wakurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteuliwa
na Rais, suala ambalo kwa namna fulani linaweza kujenga mahusiano binafsi kati ya Rais na
watumishi hao, utendaji kazi wa taasisi hiyo unatoa mwanya kwa chama tawala kupandikiza
matakwa yake. Kwa muda mrefu, vyama vya upinzani vimekuwa vikiilalamikia Tume hiyo kwa
mdai kuwa inaibeba CCM, madai ambayo ni vigumu kuyathibitisha japo ushahidi wa kimazingira
unaashiria hivyo.

Moja ya mapendekezo ya Katiba mpya yalikuwa haja ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi, lakini
kwa vile Katiba mpya haijapatikana, UKAWA na vyama vingine vya upinzani vimelazimika
kushiriki uchaguzi huu amba o kwa mara nyingine unasimamiwa na taasisi wasiyo na imani kubwa
kwake.

CCM inanufaika pia na muundo wake imara. Chama hicho kimesambaa Tanzania nzima, huku
mahusiano yake ya karibu na serikali yakiwezesha muundo huo kufanya kazi kwa ufanisi.
Sambamba na hilo, kwa vile viongozi wengi wa serikali ni watendaji wa chama hicho, raslimali
za serikali zimekuwa zikitumika kukiimarisha chama hicho hususan maeneo ya vijijini, ambako
kama ilivyobainishwa hapo awali, ndipo kwenye Watanzania wengi, kama hilo halitoshi,vyama
vya upinzani katika uchanga wao havijafanikiwa kwa kiasi kikubwa kujipenyeza au kujiiimarisha.

Kadhalika, CCM inajivunia idadi kubwa ya wanachama wake. Hali hii imechangiwa na sababu za
kihistoria, ambapo kabla ya ujio wa mfumo wa vyama vingi, katika mazingira fdulani ilikuwa ni
lazima kwa Mtanzania kuwa mwanachama wa chama hicho. Kwahiyo, wakati kukua kwa idadi ya
wanachama wa vyama vya upinzani kunategemea wanachama wa chama hicho tawala kuhamia
kwao, CCM kwa upande wake ina kazi moja tu: kuhakikisha wanachama wake hawahami, huku
ikijaribu kuwavuta wachache wanaohamia vyama vya upinzani. Kwa takwimu za hivi karibuni,
CCM ina wanachama takriban milioni 8, huku takwimu za wanachama wa vyama vya upinzani
zikiwa hazifahamiki vizuri japo yayumkinika kuhisi kuwa chama hicho tawala ndicho
kinachoongoza kwa idadi ya wanachama. Kwa mantiki hiyo, tukichukulia kuwa kila mwanachama
wa CCM atampigia kura Magufuli, chama hicho kinaingia katika uchaguzi huo kikiwa na kura
milioni 8 kibindoni (japo hilo ni suala la kufikirika zaidi kuliko uhalisia).
72

Uimara wa CCM katika maeneo mengi unachangiwa pia na uwezo wake mkubwa kifedha
unaotokana na miradi yake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na umiliki wa viwanja na majengo ya
burudani katika sehemu mbalimbali nchini. Pamoja na wito wa muda mrefu kutaka chama hicho
kisalimishe mali hizo kwa kigezo kwamba nyingi zilipatikana wakati wa mfumo wa chama
kimoja, Kwahiyo ni za Watanzania wote na sio CCM pekee, jitihada za mali hizo kurejeshwa kwa
umma zimekuwa hafifu. Uwezo wake huo kifedha umekiwezesha chama hicho kuwa na
mawasiliano rahisi kutoka ngazi ya taifa hadi mtaa. Yayumkinika kuhitimisha kuwa ni rahisi kwa
ujumbe kutoka CCM taifa kufika kwa uongozi wa chama hicho ngazi ya mtaa kuliko hali ilivyo
kwa vyama vya upinzani, na hali hiyo ina msaada mkubwa kwa chama hicho katika kipindi hiki
cha uchaguzi.

CCM pia imekuwa kimbilio kubwa la wafanyabiashara, wasafi na wachafu. Katika kipindi
flaini, ili kuepuka usumbufu wa vyombo vya dola, hususan askari wa jeshi la mgambo,
wafanyabiashara waliamua kuanzisha matawi ya CCM kwenye maeneo yao ya biashara ili
wasibughudhiwe, na mbinu hiyo ilikuwa na mafanikio. Kwa cjama tawala, hiyo ilikuwa mbinu
rahisi ya kupata wanachama wapya sambamba na kuikiimarisha chama hicho mitaani.

Kwa wafanyabiashara wakubwa, ukaribu wao na CCM unatafsiriwa kama kinga dhidi ya
unyanyasaji kutoka taasisi mbalimbali, iwe ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au taasisi
nyingine za serikali. Kanuni siyo rasmi kwa wafanyabiashara wengi, wakubwa kwa wadogo, ni
kuwa karibu na CCM ili biashara yako iendelee vema bila matatizo. Lakini si kila
mfanyabiashara anayeisapoti CCM anafanya hivyo kwa minajili ya kupata hifadhi kutoka kwa
chama hicho bali ukweli kwamba uhusiano katika ya chama hicho na wafanyabiashara ni wa muda
mrefu, tangu enzi za TANU ambapo baadhi ya wafanyabiashara enzi hizo walichangia harakati za
kumngoa mkoloni.

CCM na Magufuli wanaingia kwenye uchaguzi huu wakiwa na kitu cha kuwaonyesha Watanzania.
Ndio, nchi yetu inakabiliwa na matatizo mengi lakini itakuwa ukosefu wa shukrani kudai kuwa
hakuna maendeleo yoyote yaliyoletwa na chama tawala na serikali yake. Bila kujali maendeleo
hayo ni jitihada za ndani au za wafadhili wa nje, chama hicho kina vitu kadhaa vya kuwaonyesha
wananchi na ambavyo inaweza kujigamba hadharani kuwa ni matunda ya utawala wake. Kw
73

aupande wa UKAWA na vyama vingine vya upinzani, hilo ni gumu wao kwa sababuhawajawahi
kuwa madarakani, na nafasi yao katika mfumo wa siasa ni ya kukosoa zaidi, na pengine kupigania
maslahi ya wananchi kuliko kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Na katika hilo, CCM ina turufu ya mgombea ambaye Wizara yake inaigusa kila sehemu ya
Tanzania. Magufuli, anayesifika kwa uchapakazi ni Waziri wa Ujenzi, wizara inayohusika na
miundombinu inayoiunganisha Tanzania. Kwa bahati nzuri, sekta ya ujenzi ni moja ya chache
zilizofanya vizuri katika Awamu mbalimbali za utawala wa CCM, na Magufuli, kama Waziri
katika Awamu mbili tofauti, ana rekodi ndefu anayoweza kuitumia kujinadi vema. Ujenzi wa
barabara kwa kiwango cha lami, nyingi zikiwa zinaunganisha mikoa mbalimbali, madaraja na
vivuko katika maeneo ambayo awali yalikuwa vigumu kupitika, ni miongoni mwa turufu
alizonazo mgombea huyo na chama chake, huku UKAWA na vyama vingine vya upinzani vikiwa
na uwezekano mdogo wa kukosoa mafanikio hayo.

Tanzania, kwa muda mrefu, imekuwa ikionekana machoni mwa dunia kama kisiwa cha amani na
utulivu. Japo amani na utulivu ni misamiati relative (kwa maana ya kuwa na tafsiri pana), si
vigumu kwa mtu kulinganisha hali ilivyo nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
Tanzania na kubaini ipi yenye amani zaidi ya mwenzie. Lakini licha ya kuwa nchi yenye amani,
Tanzania pia imekuwa mahiri katika jitihada za kusaka amani katika nchi mbalimbali, hususan
majirani wake katika Ukanda wa Maziwa Makuu. CCM na Magufuli wana cha kujivunia katika
hili ilhali wapinzani watakuwa na wakati mgumu kukosoa mafanikio hayo.

Chama hicho tawala pia kinanufaina na uhusiano wake mzuri na taasisi mbalimbali zisizo za
kiserikali, za kitaifa na kimataifa. Licha ya kuwa chama tawala, ukongwe wake umepelekea aina
ya imani flani kwa taasisi hizo, sambamba na ukweli kwamba pasipo mahusiano mazuri, ni
vigumu kwa taasisi hizo kuweza kutimiza majukumu yake kwa ufanisi. Kadhalika, kwa vile
shughuli mbalimbali za taasisi hizo huhusisha viognzoi mbalimbali wa serikali, ambao wengi wao
pia ni viongozi wa CCM, mafanikio yanayotokana na taasisi hinzo ni rahisi kuhusishwa na chama
hicho tawala. Kwa mfano, uzinduzi wa mradi wa maji kijiji uliofadhiliwa na NGO ya kimataifa
lakini mgeni ramsi akawa Waziri ambaye pia ni mbunge wa jimbo hsika kwa tiketi ya CCM,
waweza kutafsiriwa kirahisi kuwa ni mafanikio ya chama hicho tawala.
74

Kama ambavyo watu wa kada mbalimbali wamependela zaidi kuwa karibu na CCM kuliko vyama
vya upinzani, chama hicho tawala kinaingia katika uchaguzi huu kikiwa na endorsements kadhaa
kutoka kwa wasanii mbalimbali. Japo wengi wa wasanii hao sio watu wanaojihusisha na siasa,
uwepo wao kwenye kampeni za Magufuli na CCM kwa ujumla unaleta mvuto na ushawishi kwa
wapiga kura.

Kwa upande mwingine, UKAWA na baadhi ya vyama vingine vya upinzani nao wamefanikiwa
kupata wasanii kadhaa kuwaunga mkono, na wamekuwa wakipata sehemu mbalimbali
kumkampenia Lowassa na wagombea wa umoja huo. Hata hivyo, kama idadi ya endorsements
hizo ina umuhimu wowote, basi CCM ina faida katika eneo hilo kwani wasanii wengi maarufu
wanamuunga mkono Magufuli na chama hicho kwa ujumla.

Wakati ujio wa Lowassa katika UKAWA, na hatimaye kuwa mgombea wake kwa tiketi ya urais
ni moja ya vitu vinavyoupa nguvu na mvuto umoja huo, ukweli kwamba mwanasiasa huyo
ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ndani ya CCM, na hata kuhama kwake n ni kutokana na
jina lake kukatwa na vikao vya mchujo vya chama hicho tawala, unaipa CCM nafasi nzuri sio tu
ya kumfahamu vema Lowassa, na pengine mapungufu yake, bali pia hata fursa ya kumdhibiti.

Na kama ilivyotarajiwa, lawama za Lowassa, akisaidiwa na Waziri Mkuu wenzie wa zamani,


Sumaye, dhidi ya CCM kuwa ndiyo chanzo cha matatizo yote yanayoikabili Tanzania, zimekuwa
zikijibiwa kirahisi na viongozi na wafuasi wa chama hicho tawala kwa kukumbushia tu kuwa
Lowassa na Sumaye pia walikuwa wana-CCM ambayo leo wanaishutumu. Ukweli kwamba mengi
wa yanayoahidiwa na wanasiasa hao hayakufanyika wakati walipokuwa Mawaziri Wakuu,
unaongezea nguvu ya hoha inayotumiwa na CCM kuwa wanasiasa hao ni waroho wa madaraka,
waliokatwa na CCM kutokana na kutokuwa na rekodi nzuri ya kiutendaji.

Hata hivyo, Lowassa, Sumaye na makada wengine waliohama kutoka CCM wanaweza pia
kunufaika na uelewa wao wa chama hicho tawala, na hilo linaweza kuwa jambo muhimu kwa
UKAWA katika kutafuta mbinu za kuingoa CCM madarakani. Kikwazo ksischo wazi dhidi ya
wanasiasa hao ni uwezekano wa CCM kuwa na taarifa zao za siri zinazohifadhiwa na Idara ya
Usalama wa Taifa, na ambazo chama hicho tawala inaweza kuzitumia kuwabomoa.
75

Kingine kinachoweza kuwa na msaada kwa CCM ni uzoefu wake katika kushinda chaguzi
mbalimbali. Kuna imani isiyo rasmi miongoni mwa wanasiasa na wafuasi wa vyama vya
upinzani kuwa CCM ni wazuri sana katika kuchakachua matokeo ya uchaguzi, zoezi
linalohusihwa na wizi wa kura. Ni vigumu kuthibitishwa hili lakini kwa kuangalia mahusiano ya
karibu kati ya chama hicho tawala na taasisi mbalimbali za umma zinazohusika na masuala ya
uchaguzi, yayumkinika kuhisi kuwa CCM ipo katika nafasi nzuri kuwahujumu UKAWA kwa
mbinu chafu kuliko uwezekano kwa umoja huo kufanya hivyo.

Hata hivyo, kuna faraja, japo kidogo, kwa UKAWA kuwa kwa kuwapata watu kama Lowassa na
Sumaye, wanaojua kwa undani mbinu chafu za CCM katika chaguzi mbalimbali inaweza
kuwasaidia kudhibiti mbinu hizo. Taarifa ambazo haziwajawahi kuthibithswa wala kukanushwa
za uwepo wa mmoja wa wakurugenzi wakuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa katika
kambi ya Lowassa atangu alipokuwa akiwania urais kupitia CCM, na baadaye kuhamia naye
UKAWA, zinaweza kutoa matumaini kwa umoja huo kwamba wana mtu anayejua tasnia ya
mbinu chafu katika Nyakati za uchaguzi. Hili ni la kufikirika zaidi kuliko uhalisia kwani hakujawa
na uthibitisho wa wazi.

Hata kabla ya ujio wa Lowassa na Sumaye, vyama viwili vinavyounda UKAWA, CUF na
Chadema vilikuwa vikiandamwa na tuhuma za ukanda na udini. Japo tuhuma hizo zimekuwa
zikichochewa zaidi na CCM kama mbinu ya kuvishushia hadhi vyama hivyo ambavyo kwa nyakati
mbili tofauti vimekuwa vyama vikuu vya upinzani, kwa kiasi fulani zimejenga mwonekano hasi
wa ina flani. Wakati CUF imekuwa ikituhumiwa kuwa ni chama cha Kiislamu na cha Wapemba,
Chadema kwa upande wake imekuwa ikituhumiwa kuwa ni chama cha Knda ya Kaskazini na cha
Kilutheir.

Wakati tuhuma hizo hazijaigusa sana CUF katika uchaguzi huu, ukweli kwamba Lowassa na
Sumaye, sio tu wanataka mkoa mmoja, Arusha, ulio Kanda ya Kaskazini, bali pia ni Walutheri,
lakini wakati huohuo CCM ikionekana chama cha kitaifa zaidi, kwa maana ni vigumu
kukuonyesha kama cha kidini au kikanda, inaweza kuwa turufu kwa chama hicho tawala
kuwatahadharisha wapigakura juu ya hatari ya kumchagua Lowassa na UKAWA kwa ujumla.
Udini na ukanda ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili Tanzania japo si kwa kiasi kikubwa,
76

lakini kwa kujenga uthibitisho, CCM inaweza kujitengenezea mazingira mazuri dhidi ya
UKAWA, ambayo kwa upande mwingine inaweza pia kuthiriwa na uhusiano wa karibu kati ya
Lowassa na Askofu Gwajima.

Kwa CCM, kushinda uchaguzi huu sio suala tu la kubaki madarakani bali kwa wengi wa viongozi
wake ni suala la 'kufa na kupona.' Chama hicho kina idadi kubwa tu ya viongozi ambao wamekuwa
wanufaika wakubwa wa uwepo wake madarakani. Kwa vile ni jambo la kawaida kwa familia ya
kiongozi wa kisiasa kuvutia wanafamilia wengine kuingiza kwenye siasa, CCM ina idadi kubwa
ya wanasiasa, wazee kwa vijana, ambao chama hicho sio tu kimekuwa ni sehemu muhimu ya
maisha yao bali pia ndiyo kinachowawezesha kupelekea mikono vinywani. Katika mazingira
kama haya, inatarajiwa kuwa viongozi wengi wa chama hicho hawatokuwa tu wanapigani ushindi
wa Magufuli na CCM bali pia uhai wao binafsi. Kwa CCM kuondolea madarakani na UKAWA,
wanasiasa hao watakuwa kama wamekatwa mikono, au kuzaliwa katika zama mpya ambayo
baadhi yao hawajawahi hata kuifikiria.

Kadhalika, Kikwete na viongozi wengine wanaostaafu baada ya uchaguzi huu wanatarajiwa


kuitumia kila nguvu na raslimali waliyonayo kuhakikisha CCM na mgombea wake, Magufuli,
wanashinda, ili kujitengenezea mazingira ya kustaafu kwa amani. Kimsingi, iwapo tashinda
uchaguzi, uwezekano wa Magufuli kuchukua hatua dhidi ya wastaafu pale itapobainika
walifanya makosa wakati wa utawala wa Kikwete, ni mdogo, kulinganisha na uwezekano mkubwa
wa hilo kutokea iwapo UKAWA wataingia madarakani. Ni wazi, Kikwete angependa kumkabidhi
urais Magufuli kuliko Lowassa kwani mwana-CCM mwenzie anamhakikishia kustaafu kwa
amani zaidi kuliko rais kutoka chama cha upinzani.

Tangu Lowassa aingie Chadema na kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA,
miongoni mwa lawama imekuwa kwamba Chadema sasa ni Lowassa, na UKAWA pia ni
Lowassa. Ni kile kwa kimombo wanaita a one-man party. Tofauti na hali hiyo, Magufuli
anaonekana kuwa mgombea wa chama si kwa vile tu ni kweli ndiye mgombea wa chama hicho
bali pia kampeni yake inaendeshwa katika hali inayotofa taswira ya kichama zaidi kuliko kibinafsi.
77

Lakini tatizo hilo ambalo si la kufikirika, kwa vile lipo na linaonekana bayana, laweza kuwa na
madhara mengine kwa UKAWA, kwamba kwa kuwekeza nguvu kubwa kumnadi Lowassa, vyama
vinavyounda umoja huo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vinaweza kujikuta
vikipoteza nafasi kadhaa za ubunge na udiwani, huku CCM ambayo mgombea wake Magufuli
licha ya kunadiwa kichama zaidi, haathiri kampeni za chama hicho katika ngazi za ubunge na
udiwani, ikaishia kunyakuwa viti vingi zaidi.

Pamoja na fursa hizo nyingi zinazoweza kuitengenezea CCM na mgombea wake Magufuli
mazingira mazuri ya ushindi, chama hicho kinakabiliwa na vikwazo kadhaa. Kikwazo kikubwa
zaidi ni kuhusishwa kwake na kila baya linaloihusu Tanzania. Orodha ni ndefu, lakini kama kuna
tuhuma inayoitafuna zaidi CCM ni suala la ufisadi. Na licha ya tuhuma hizo za ufisadi kuiandama
CCM katika awamu zake mbalimbali, hali katika awamu mbili za Rais Kikwete imekuwa mbaya
mno. Tuhuma mbalimbali zilizouandama utawala huo zimeelezewa kwa kirefu katika sura ya tatu
ya kitabu hiki. Mtihani mkubwa kwa chama hicho tawala ni kuwaaminisha wapigakura kuwa kuna
uwezekano kwa chama hicho kuweza kuwa hai pasipo kujihusisha na ufisadi. Hali ni mbaya mno
kiasi kwamba wakati chama hicho kilipokuja na mkakati wa kujIvua magamba, watu wengi
walidai jaribio hilo lingekiuwa chama hicho katika namna ileile ya kumuua kobe ukijaribu
kumngoa gamba.

Kama kuna ajenda moja inayoweza kuinyima CCM ushindi ni suala hilo la ufisadi. Na licha ya
Lowassa kuandamwa na tuhuma za ufisadi alipokuwa CCM, chama hicho tawala kinapata wakati
mgumu kuzungumzia ufisadi mmoja tu huku chenyewe kikiandamwa na lundo la tuhuma za
ufisadi. Na kwa upande mwingine, ufisadi wa Lowassa si usafi wa CCM.

Tatizo linalopelekea ufisadi kuwa kama sehemu ya uhai wa CCM ni kulindana. Kimsingi, laiti
sera ya kulindana isingekuwepo, basi leo hii CCM isingehangaishwa na Lowassa kwa sabau
ingeweza kuchukua hatua katika nyakati mbalimbali dhidi yake kutokana na kuhusishwa na
tuhuma za ufisadi.

Kushindwa kwa chama hicho na serikali yake kuchukua hatua dhidi ya ufisadi kunatajwa kuwa ni
moja ya sababu za kukua kwa tatizo hilo, kwa sababu mafisadi watarajiwa hawana cha
78

kuwaogopesha kufanya majaribio ya ufisadi mpya, kwa kuzingatia kuwa wengi wa


waliokwishafanya hivyo hawakuchukuliwa hatua zozote.

Kibaya zaidi, CCM inaingia kwenye uchaguzi huu huku tuhuma nyingi za ufisadi zikiwa
hazijapatiwa majibu wala hatua kuchukuliwa. Licha ya suala la Richmond kujitokeza mwaka
2006, taarifa mbalimbali kuhusu suala hizo hazijaweza kutoa majibu ya maswali kadhaa
yanayowasumbua Watanzania wengi. Kwa mfano, wakati Lowassa akituhumiwa kuwa mhusika
mkuu katika kashfa hiyo, je bosi wake, yaani Rais Kikwete, hakuwa na ufahamu wowote
kuhusiana na suala hilo?

Kwa upande wa kashfa ya EPA, hadi leo serikali ya CCM imegoma katakata kuwajulisha
Watanzania kuhusu mmiliki wa kampeni ya Kagoda, inayotajwa kuwa mnufaika mkubwa wa
ufisadi huo. Kwenye kashfa ya Escrow, bado kuna lundo la maswali kuhusu, kwa mfano, wakati
majina ya waliopewa mgao kupitia Benki ya Mwananchi yalifahamika, wanufaika wa mgao
unaotajwa kuwa mkubwa zaidi kupitia benki ya Standard Chartered hawajatajwa hadharani.
Katika kashfa ya Opereheni Tokomeza, Serikali ilifanya kioja cha mwaka kwa kuwasafisha
wahusika pasipo kutoa maelezo ya kuridhisha.

Kushamiri kwa ufisadi, sambamba na kutokuwepo jitihada za dhati kupambana na tatizo hilo
kunaweza kuwashawishi wapiga kura, hata walio wanachama wa CCM, kukinyima kura chama
hicho tawala. Licha ya mgombea wa chama hicho, Magufuli, kuahidi kuanzishwa kwa mahakama
maalumu za kushughulikia kesi za ufisadi, kuna hisia miongoni mwa wananchi wengi kuwa ahadi
hiyo ni porojo tu kwani tatizo si ukosefu wa mahakama bali dhamira ya kupambana na ufisadi.

Licha ya ufisadi wa EPA, Richmond, Escrow na kashfa ya Operesheni Tokomeza, kuna kashfa
nyingine kama ya Meremeta, Tangold, Mwananchi, mgodfi wa Kiwra, na nyinginezo ambazo
zimezikwa kienyeji bila serikali ya CCM kubainisha majina ya wahusika wala kuchukua hatua
stahili dhidi yao. Tatizo hapa sio tu kashfa hizo zinaweza kuiathiri CCM katika uchaguzi huu bali
pia ni uwezekano wa kuibuka upya huko mbeleni iwapo chama hicho kitashinda.

Tukiweka kando kashfa za ufisadi, tangu kustaafu kwa Nyerere, Tanzania imeendelea kushuhudia
ongezeko la uhalifu mkubwa, hasa tatizo sugu la biashara ya madawa ya kulevya, biashara ya
79

usafirishaji binadamu, uatakatishaji fedha na ujangili. Matatizo haya ambayo yalikuwepo hata
kabla ya Kikwete kuingiza madarakani, yameshamiri zaidi katika utawala wake, ambapo kuna
licha ya kuchafua jina la Tanzania kimataifa, nchi yetu imefikia hatua ya kuonekana kama ina-
export uhalifu (kwa mfano, kuna idadi kubwa tu ya Watanzania waliofungwa katika magereza ya
nchi mbalimbali duniani kwa makosa ya madawa yakulevya)

Kana kwamba matatizo hayo si mabaya kwa hadhi ya nchi yetu, kwa muda mrefu sasa Tanzania
imejikuta ikipata sifa mbaya kutokana na mauaji ya albino, ambapo vyombo vya habari
mbalimbali vya kimataifa vimekuwa vikifuatilia unyama uhalifu huo wa kinyama kwa karibu.
Jitihada za serikali kupambana na tatizo hilo zimekuwa hafifu, huku tuhuma zikielekezwa kwa
wanasiasa ambao baadhi yao wanatuhumiwa kuwa wateja wa waganga wa kineyji wanaotumia
viuongo vya albino kutengeneza dawa za asili. Japo CCM haiwezi kuhusishwa moja kwa moja na
tatizo hili, ukweli kwamba limejiri wakati wa utawala wake unaweza kuwapa nguvu UKAWA
kukibana chama hicho, kwa hoja kwamba kimeshindwa kuwalinda maalbino.

Licha ya kuonekana kama kisiwa chama amani na utulivu, Tanzania chini ya utawala wa CCM
imekuwa na rekodi isiyopendeza kuhusu haki za binadamu. Wakati uhalifu wa mauaji ya albino
unaangukia katika eneo hilo, jeshi la polisi limekuwa likilaumiwa mara kwa mara, hususan na
vyama vya upinzani, kwa kutumia nguvu kubwa zaidi ya akili katika matukio kadhaa
yalivyopelekea vifo na majeraha. Kwa vile CCM imekuwa kama ina kinga dhidi ya vitendo hivyo
vya polisi, haikufanya jitihada za kutosha kupambana na ukiukwaji huo wa haki za binadamu.
Kimsingi, chama hicho tawala kimekuwa kikionekana kama kinafurahia mwenendo wa jeshi la
polisi, ambapo wakati fulani, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa ruhusa kwa polisi kuwapiga raia
badala ya kusisitiza haja ya kuzingatia haki za binadamu.

Yayumkinika kuhitimisha kuwa moja ya sababu za uhusiano hafifu kati ya wananchi wengi na
jeshi la polisi ni kwa chombo hicho cha dola kupuuzia haki za binadamu hususan pale maslahi ya
chama tawala yanapoguswa. Ni katika mazingira hayo, jeshi hilo limebandikwa jina la poli-CCM
likimaanisha polisi wa CCM. Chuki za wananchi dhidi ya jeshi hilo linaloonekana kuipendelea
CCM zaweza kukiathiri chama hicho kwenye uchaguzi huu.
80

Kiuchumi, wakati CCM inaweza kujinadi kwa kutumia takwimu mbalimbali zinazoonyesha kuwa
Tanzania imekuwa ikipiga hatua kubwa kuboresha uchumi wake, hali halisi mtaani ni tofauti
kabisa. Ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei, kiapto kisichoendana na hali halisi ya maisha pamoja
na matatizo mengine kama hayo yamepelekea kushamiri kwa rushwa na uhalifu mwingine. Tofauti
za kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho sio tu imezidi kukua mwaka hadi mwaka lakini
pia imeongeza hamasa kwa wasio nacho kutafuta njia za kuweza kumudu maisha yao, ambapo
mara nyingi kimbilio limekuwa kwenye uhalifu, ufisadi na rushwa.

Wakati mgombea wa CCM, Magufuli anasifika kwa uchapakazi, hana rekodi inayoashiria ni
mpambanaji dhidi ya ufisadi, suala linaloweza kutumiwa na UKAWA kuonyesha udhaifu wake.
Lakini tatizo kubwa linaloweza kumkabili mgombea huyo wa CCM laiti akishindwa ni mfumo
unaoendesha siasa za chama hicho ambao kwa kiasi kikubwa sio tu unatoa fursa ya kufanyika
ufisadi bali pia chama hicho ni mnufaika wa fursa hiyo. Ili Magufuli aweze kukabiliana na tatizo
la ufisadi itamlazimu atengeneze maadui wengi ndani ya CCM, kwa sababu wengi wa
wanaomzunguka ni wanufaika wa ufisadi.

Utawala wa CCM umeshuhudia watu kutoka kada mbalimbali katika jamii wakikimbilia kwenye
siasa, kutona ana siasa kugeuka kuwa ajira ya uhakika zaidi kuliko zote. Wasomi mbalimbali
wameacha kazi za taaluma na kuingiza kwenye siasa, na kinyume cha matarajioya wengi kuwa
ujio huo wa wasomi ungechochea maendeleo, wengi wao wameishia kukumbwa na kashfa za
ufisadi kiasi cha kushamiri kwa hisia miongoni mwa Watanzania kuwa wasomi wetu ni miongoni
mwa wanaomchangia matatizo katika nchi yetu. UKAWA yaweza kuinyooshea kidole CCM
ikiituhumu kwa kuzalisha ukame wa wanataaluma na kisha kuwaharibu wanataaluma
wanaoingia katika siasa kupita chama hicho, kwa kuweka kando eilu yao na kukumbatia ufisadi.

Japo tangu kuanza rasmi kwa kampeni za CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu,
mgombea Magufuli ameonekana kutoa ahdi mbalimbali zenye mwelekeo wa kurekebisha kasoro
mbalimbali zilizopo, kwa kiasi kikubwa, yeye na chama chake wameshindwa kuwa wawazi kwa
Watanzania. Kinachohitajika ni kwa CCM kukiri makosa na mapungufu yake bila aibu, na
kutanabaisha jinsi gani itayarekebisha iwapo itapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi. Kama
kuna msaada mkubwa kwa Magufuli kufanya hilo, chapisho la January Makmba la Tanzania
81

mpya lingeweza kumsaidia sana mgombea huyo kuyaeleza matatizo mbalimbali yanayoikabili
nchi yetu, na kukiri uhusika wa CCM, na jinsi ya kuyashughulikia. Kukiri kosa sio udhaifu bali ni
sehemu ya hatua za kutatua kosa husika, kwani kwa kukiri kosa fulani, yaashiria mhusika
anafahamu tatizo lipo wapi.

Hatua zisizo madhubuti za kushughulikia baadhi ya matatizo yanayoikabili Tanzania kwa sasa
kunaweza pia kuwa kikwazo kwa CCM. Na moja ya matatizo hayo sugu ni mgao wa kudumu wa
umeme. Tatizo hilo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na ufisadi mfululizo linawakera
Watanzania wengi. Kibaya zaidi, badala ya utawala wa CCM kuwekeza nguvu kumaliza tatizo
hilo, jitihada za baadhi ya watendaji wake zimeelemea zaidi katika kutumia tatizo hilo kama njia
ya kufisadi zaidi. Kimsingi, Shirila la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa kama ngombe
asiye na lishe lakini anakamuliwa maziwa mfululizo hadi anatoa damu badala ya maziwa.
Hujumam mfululizo dhidi ya Shirika hilo, katika wamu mbalimbali za utawala wa CCM
zimechangia sana kufanya mgao wa umeme kuwa stahili ya Watanzania. Si jambo la kushangaza
kukutana na bandiko mtandaoni, wakati huu wa kampeni, likieleza bayana nitainyima kura CCM
kwa sababu ya mgao wa umeme.

Wakati wa kampeni za kuwania urais mwaka 2005, moja ya hadi za CCM na Kikwete ilikuwa
kuzalisha ajira milioni mbili. Kama lengo hilo lilifikiwa au la, kinachoonekana mtaani ni
kuzalishwa kwa ajira nyingi za uhalifu kuliko ajira halali. Kumekuwa na ongezeko la idadi ya
waliojiingiza katika siasa na kugeuka mamilionea kutokana na marupurupu makubwa kwenye
ubunge, ongezeko la wauza unga, majangili, mafisadi, na wahalifu wengine kwa ujumla. Ugumu
wa maisha na ukosefu wa ajira umepelekea uhalifu kuwa kama ajira halali na njia halali ya
kutengeneza kipato.

Kama ilivyoelezwa katika sura zilizotangulia, uchaguzi mkuu huu utaingia kwenye kumbukumbu
kama uliohusisha matumizi makubwa ya teknolojia, hususan mitandao ya kijamii. Wakati
maendeleo hayo yana faida takriba sawa kwa CCM na UKAWA, inatarajiwa kuwa umoja huo wa
Wapinzani unaweza kunufaika zaidi kwa sababu mitandao hiyo ya kijamii inatumika kama nyenzo
muhimu ya mawasiliano kati ya viongozi na wanachama, na miongoni mwa wanachama, na hivyo
kukabiliana na kikwazo cha vyombo vya habari vya umma kuelemea CCM,.
82

CCM inakwazwa pia na kile Waingereza wanaita guilty by association, yaani kuhusishwa na
kosa kutokana na kuhusiana na mtenda kosa. Katika hilo, uawala wa CCM unaweza kubebeshwa
lawama za ubadhirifu mkubwa unaofanywa kwenye taasisi mbalimbali, hususan vyama vya
ushirka ambavyo baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakilindwa na CCM kutokana na
michango yao ya fedha kwa chama hicho tawala. Tatizo la ubadhirifu katika vyama vya ushirka
sio tu linawaathiri sana wakulima vijijini bali pia lina athari kwa uchumi wa taifa letu ambalo
linategemea kilimo kama uti wa mgongo. Vyama vingi vya ushirika vinaonekana huko vijijini
kama taasisi za CCM, na ni rahisi makosa yanayofanywa na vyama hivyo kuhusishwa na chama
hicho tawala.

Licha ya vyama vya ushirika, uendeshaji wa serikali za mitaa umegubikwa na tuhuma mbalimbali
za ufisadi, sambamba na watendaji wa serikali hizo kujiona kama miungu-watu, na kutokuwa na
msaada wa kutosha kwa wananchi. Ni wazi kuwa chuki za wananchi dhidi ya watendaji wa serikali
za mitaa wenye tuhuma za ubadhirifu au wasio na utendaji kazi bora zinaweza kuiathiri CCM pia,
hasa ikizingatiwa kuwa ni vigumu kuchora mstari unaotenganisha chama hicho tawala na serikali
za mitaa.

Tatizo la umungu-mtu lipo pia ndani ya CCM yenyewe na katika serikali yake. Kw aupande mmoja
tatizo hili linachangiwa na ufisadi ambapo jeuri ya fedha inawapa kiburi watendaji wakiamini
kuwa fedha walizonazo ni kinga dhidi ya kuchukuliwa hatua. Kwa upande mwingine, utoaji ajira
kwa misingi ya undugu au urafiki unawajengea kiburi baadhi ya watendaji wanaoamini kuwa hata
wakiboronga watalindwa na aliyewaweka hapo. Sababu kama hizi zinaweza kuwafanya baadhi
ya wapigakura waamue kufanya majaribio kwa utawala wa UKAWA hasa kutokana na
kutapakaa kwa hisia kuwa ni vigumu kwa CCM kupambana na mengi ya matatizo yanayoikabili
yenyewe kama chama, na nchi kwa ujumla.

Umungu-mtu na viongozi kuwa mbali na wananchi pia ni matokeo ya mfumo uliorithiwa kutoka
zama za chama kimoja. Wakati huo, kauli ya kiongozi ilikuwa kama amri ya mungu, ni sahihi
na isiyoweza kupingwa. Ujio wa mfumo wa vyama vingi haijafanikiwa kuondoa kasumba hiyo,
ambayo pia inachangia viongozi kutofahamu fika matatizo ya wananchi kutokana na kutokuwa
karibu nao.
83

Kadhalika, mabadiliko yaliyoitoa CCM kutoka chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwa
chama cha wafanyabiashara na wasomi yanaweza kutoa fursa kwa vyama vya upinzani, hususan
UKAWA, kuwaunganisha wakulima na wafanyakazi waliotelekezwa na CCM, na kupata kura
kutoka kwa makundi hayo mawili yenye asilimia kubwa ya Watanzania.

Ukweli kwamba huu ni uchaguzi mkuu wa kwanza kwa CCM kukumbana na muungano imara wa
upinzani, unaoongozwa na Lowassa, mwanasiasa aliyekuwa na nguvu kubwa alipokuwa ndani ya
CCM, unaweza kukifanya chama hicho tawala kisijue jinsi ya kuukabili upinzani huo wa aina
mpya. Kwa kiasi fulani, ushindi wa CCM dhidi ya vyama vya upinzani katika chaguzi mbalimbali
huko nyuma ulichangiwa na mazingira ya chama kikongwe na imara kuchuana na upinzani
dhaifu na uliogawanyika. Mbinu zilizotumiwa na CCM katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005
na 2010 zinaweza zisifanikiwe kwenye uchaguzi wa mwaka huu kutokana ushirikiano wa vyama
vya upinzani vinavyounda UKAWA.

Lakini kwa upande mwingine, mazowea ya kushinda kila uchaguzi mkuu yanaweza kuijengea
CCM hali ya kujiamini kupita kiasi, na hivyo kuzembea, na kutofa fursa kwa UKAWA kushinda
uchaguzi huo. Hadi wakati ninaandika makala hii kulikuwa na tuhuma za chinichini kuwa
maandalizi ya chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu huu si ya kuridhisha, aidha kutokana na
imani kuwa ushindi ni lazima au kutoelewa jinsi ya kukabiliana na UKAWA.

Licha ya tuhuma za mara kwa mara za ufisadi zilizouandama utawala wa Kikwete, moja ya
matatizo yaliwagusa wengi ni ombwe la uongozi wa taifa. Wakati Wapinzani walimtuhumu Rais
Kikwete kuwa ni dhaifu, wananchi wengi walimwona kama mpole kupita kiasi, japo wakati
anaingia madarakani kwa mara ya kwanza, mwaka 2005 alitahadharisha kuwa tabasamu lake
lisieleweke vibaya. Ombwe hilo la uongozi ambalo lilijitokeza mara baada ya Nyerere kustaafu
na hatimaye kufariki, limezidi kukua, awamu moja baada ya nyingine. Kuna Nyakati mabpo nchi
huonekana kama inajiendesha kwa auto-pilot, aidha kwa vile Rais alikuwa kwenye safari zake
mfululizo nje ya nchi au watendaji wa serikali walikuwa wamebanwa na jukumu la kuvuna
shamba la bibi, kula keki ya taifa, yaani kufanya ufisadi. UKAWA wanaweza kunufaika katika
hili iwapo wataweza kuonyesha mlolongo wa kukua kwa ombwe la uongozi, na kujenga hisia
kuwa Magufuli atakuja kupendeza ombwe hilo badala ya kuliondoa.
84

Kwa upande wa UKAWA, turufu yao kubwa ni Lowassa, mwanasiasa ambaye mwenye
umaarufu mkubwa tangu alipokuwa CCM na sasa akiwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA
kupitia Chadema, alikojiunga baada ya jina lake kukatwa katika vikao vya mchujo vya CCM.
Umaarufu wake ndani ya chama tawala ulishuhudia maelfu kwa maelfu ya wananchi wakijitkeza
kwenye shughuli zake wakati anaowania kugombea urais kwa tiketi ya CCM. Umaarufu huo
umeendelea kuonekana baada ya kujiunga na Upinzani.

Tukiweka kando makada kadhaa waliohama CCM na kumfuata Lowassa UKAWA, hakuna
takwimu sahihi kuhusu idadi ya wana-CCM waliojiunga na umoja huo wa wapinzani kumfuata
mwanasiasa huyo. Kipimo pekee kimekuwa idadi ya watu wanaojitokeza kwenye mikutano ya
kampeni za UKAWA na Lowassa wao. Kama umati ni kipimo cha kura, basi yayumkinika kuhisi
kuwa umoja huo na mgombewa wake utafanya vizuri.

Licha ya umaarufu wake, Lowassa amekuwa akielezwa kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa
kifedha, na mwenye marafiki matajiri. Uhaba wa fedha ulikuwa kikwazo kikubwa kwa vyama vya
upinzani katika chaguzi za nyuma, lakini fedha za Lowassa na marafiki zake zinaweza kuondoa
tatizo hilo na kuitengenezea UKAWA nafasi nzuri kuchuana na CCM kikamilifu.

Ni muhimu pia kutambua kuwa kama kuna mtu mmoja aliyechangia mno Kikwete kuingiza
madarakani mwaka 2005 ni Lowassa (pamoja na Rostam). Inaelezwa kuwa Mtandao wa Kikwete
ulikuwa na muundo wa namna hii: Mgombea: Kikwete; Mpanga mikakati ya kisiasa: Lowassa;
Bwana Fedha: Rostam. Inaelezwa kuwa wakati uhusiano kati ya Kikwete na Lowassa sio mzuri,
Lowassa na Rostam bado ni marafiki. Yayumkinika kuhisi kuwa wanasiasa hao wawili wanaweza
kutumia mbinu zilezile zilizowezesha Kikwete kuingiza madarakani mwaka 2005 ili zimsaidie
Lowassa kuingiza Ikulu. Na kwa vile wawili hao wanaojua vema CCM, wanaweza kutumia uelewa
huop kutengeneza mikakati imara ya ushindi kwa Lowassa.

Kwa upande mwingine, UKAWA iliwekeza nguvu kubwa katika kusambaza elimu kwa wapiga
kura na usimamizi wa uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa kompyuta (BVR). Japo umoja
huo ulilaumiwa huko nyuma kwa kutumia muda mwingi katika masuala hayo badala ya kufanya
maandalizi ya uchaguzi, kwa mfano kumpata na kumnadi mgombea wake wa kiti cha urais kabla
85

CCM hawajafanya hivyo kwa mgombea wao, masuala hayo pia yanaweza kuwa yaliwaweka
karibu zaidi na wapigakura, hasa katika mikutano yao mbalimbali ya uhamasishaji.

Kadhalika, uamuzi wa vyama hivyo vinne kuungana kupigania maslahi ya wananchi katika Katiba
Pendekezwa, sambamba na jitihada za awali za Chadema kuibua kashfa mbalimbali za ufisadi
zilizouandama utawala wa CCM, vinaweza kuwa vigezo muhimu kwa wananchi kuwa na imani
na UKAWA. Kadhalika, kuweka kando maslahi binafsi ya kila chama na kufanya ushirikiano kwa
kusimamiasha mgombea mmoja kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, na katika
uchaguzi huu mku, kunaweza kuwapa matumaini wananchi kuwa vyama hivyo vina nia ya dhati
ya kushika dola na kuutumikia umma.

Hata hivyo, ujio wa Lowassa, mwanasiasa aliyeandamwa na wapinzani kwa takriban miaka tisa,
akituhumiwa kwa ufisadi, na kupewa fursa ya kuwa mgombea urais wa umoja huo, kunaweza
kutia doa wasifu wa vyama hivyo, hususan Chadema, ambayo ilijijengea umaarufu mkubwa
kutokana na msimamo wake thabiti dhidi ya ufisadi. Hili litajadiliwa kwa kirefu katika kipengele
kinachohusu vikwazo kwa UKAWA.

Suala jingine linaloweza kuisaidia UKAWA kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao ni ukweli
kwamba imefika hapo ilipo against all odds, yaani kwa kuruka vihunzi vingi. Awali, ilitarajiwa
umoja huo ungesambaratika mapema kama ulivyoundwa, hukohuko Dodoma wakati wa Bunge
Maalum la Katiba. Hilo halikutokea, na sio tu umoja huo ulisimama kidete lakini baadaye
ulikubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye
katika uchaguzi mkuu. Awali, wengi walidhani suala hilo lingekuwa kama miujiza, kwamba
vyama hivyo vilikuwa na tofauti nyingi za msingi na isingewezekana kushirikiana katika uchaguzi
wowote ule. Kinyume na matarajio ya wengi, vyama hivyo vinavyounda UKAWA sio tu viliweza
kushirikiana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, bali pia umoja huo ulipata matokeo ya
kuridhisha. Kusuasua umoja huo kumtangaza mapema mgombea wake wa urais kulirejesha tena
hisia kuwa uhai nwa UKAWA umefikia kikomo. Kwa mara nyingine, umoja huo ulifanikiwa
kuruka kihunzi hicho, na hatimaye kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wao. Hizi sio hatua ndogo
hata kidogo, na zinaweza kuwa zimejenga picha nzuri kwa Watanzania kiasi cha baadhi yao
kuwapatia kura za kutosha kuingiza Ikulu.
86

Kinyume na CCM inayoonekana kama klabu maalum kwa watu maalum (exclusive mambers
club), uongozi wa vyama vinavyounda UKAWA umekuwa rahisi kufikiwa na wananchi, na kwa
kiasi kikubwa unajumuisha watu wa kawaida. Ukawaida wa viongozi hao unachangiwa zaidi na
vyama hivyo kuwa karibu na wananchi, na kongea lugha ya wananchi wa kawaida, ilhali
viongozi wengi wa CCM honekana kama wanaongea llugha ya watawala. Kwa vile kujiunga na
vyama hivyo sio njia ya mkato ya mafanikio katika maisha au kupata kinga dhidi ya taasisi za
dola (sababu zinazotajwa kuwavutia watu wengi kujiunga na CCM), kwa kiasi kikubwa,
UKAWA ina wanasiasa wa kawaida, watu wanaofahamu fika athari za kuwa mpinzani wa
chama tawala. Hali hii inawafanya wanasiasa hao kutotofautiana sana na wananchi wa kawaida,
na hili linaweza kuwasaidia wagombea wa UKAWA katika kampeni zao.

Mtaji mkubwa zaidi wa UKAWA ni ajenda yao ya mabadiliko. Sio siri kwamba kuna idadi kubwa
tu ya Watanzania wanaohitaji mabadiliko ya haraka. Wengi wamechoshwa na CCM inayoonekana
imeziba masikio kuhusu haja ya kubadilika. Huku wanaohama CCM wakimnukuu Nyerere
katika angalizo lake kwamba wana-CCM wasipoata mabadiliko ndani ya chama hicho
watayatafuta nje, na kuhalalisha sababu zao za kuihama CCM na kujiunga na UKAWA, vyama
vinavyounda umoja huo vimekuwa na rekodi ya kudai mabadiliko mbalimbali, ikiwa ni pamoja
na wazo la Katiba mpya. Kwa vile UKAWA inaonekana kuwa mmiliki halali wa ajenda ya
mabadiliko, CCM inaweza kupata wakati mgumu kuwashawishi wapiga kura kuwa nayo inaweza
kuleta mabadiliko, hasa ikizingatiwa kuwa chama hicho tawala kimekuwa kikwazo kikubwa cha
mabadiliko kusudiwa.

Suala jingine linaloweza kuwasaidia UKAWA ni ukweli kwamba mengi ya mabaya ya CCM
yanaonekana hadharani. Kwa mfano, tatizo la mgao wa umeme sio jambo linahitaji uchunguzi,
lipo bayana na linawaathiri Watanzania wengi. Kadhalika, tuhuma dhidi ya CCM kuhusu ufisadi
zipo hadharani, na baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakieleza waziwazi kuwa
mwelekeo wa chama hicho sio mzuri. Hali hii inaweza kuwasaidia UKAWA kujenga hoja ya
umuhimu wa kuingoa CCM kwa manufaa ya wananchi.

Vikwazo walivyopitia UKAWA hadi kufika hapa ambapo wamemudu kusimamisha mgombea
mmoja wa urais vinaweza kuwapa hamasa na kuona ndoto yao ya kuingoa CCM sio tu
87

inawezekana bali pia ipo karibu. Hamasa hiyo ikiambatana na mikakati thabiti, yaweza kuusaidia
umoja huo kufanya vizuri dhidi ya CCM katika uchaguzi huo. Hata hivyo, kuwa na dhamira ni
kitu kimoja, kuitimiza ni kitu kingine kabisa. Kosa linaloweza kuigharimu UKAWA ni iwapo
itapuuzia uimra wa CCM, na dhamira ya chama hicho tawala kutaka kuendelea kuwa madarakani.

Pamoja na ukweli kuwa hakuna takwimu za wazi kuhusu idadi ya wanachama wa kila chama
kinachounda umoja huo, ni dhahiri kuwa uamuzi wao wa kushirikiana umewaongezea idadi ya
wapigakura. Ukichanganya na wana-CCM waliomfuata Lowassa, umoja huo unaweza kupata kura
za kutosha za kuingoa CCM madarakani. Kadhalika, uwezekano wa baadhi ya wana-CCM kupiga
kura za chuki kutokana na Lowassa kukatwa, unaweza pia kuwa na manufaa kwa UKAWA.

Chaguzi katika nchi mbalimbali, kama vile Nigeria, Kenya, na kwingineko ambako vyama vya
upinzani vilifanikiwa kuviondoa madarakani vyama tawala, kunaweza kutoa hamasa kubwa kwa
UKAWA na kuwapa imani kuwa kukiondoa chama tawala madarakani ni jambo linalowezekana
kama ilivyotokea sehemu hii au ile.

Kingine kinachoweza kuwavutia wapigakura kwa UKAWA, sio tu ukweli kwamba vyama
vinavyounda umoja huo vilijumuika pamoja kutetea mapendekezo ya Katiba ambayo, pamojamna
mambo mengine ilishauri uwepo wa serikali tatu, bali pia sera ya umoja huo kuhusu muungano ni
muundo huo wa serikali tatu, ambao kama ilivyokuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba,
inapingwa na CCM. Ni ukweli usiofichika kuwa idadi kubwa ya Wanzibari wanaelekea kutaka
muundo wa muungano wa serikali tatu, na suala hilo linaweza kuinufaisha UKAWA.

Kadhalika, licha ya lowassa kupinga wazo hilo alipokuwa CCM, ameshatamka bayana kuwa
akishinda urais, sio tu atashughulikia suala la mabadiliko ya kKatiba, bali pia atapigania
upatikanaji wa serikali tatu. Hata hivyo, mabadiliko hayo katika msimamo wake yametafsiriwa na
CCM kuwa ni 'ulaghai unaochangiwa na tamaa ya madaraka.'

Lakini pamoja na fursa hizo zinaweza kuisadia UKAWA kuishinda CCM, umoja huo unakabiliwa
na vikwazo kadhaa. Kikubwa zaidi ni ujuio wa Lowassa. Katika mazingira ya kawaida tu, ni
vigumu kwa vyama vilivyomshutumu Lowassa kwa takriban miaka tisa kuwa ni fisadi, na
88

kuwaaminisha wananchi kuwa huo ndiyo ukweli, kumudu kumsafisha katika kipindi cha miezi
mitatu tu tangu ajiunga nao.

Sambamba na hilo, kitendo cha UKAWA kuchelewa kutangaza mgombea wake, na baadaye
kufahamika kuwa walikuwa wanamsubiri mgombea atoke CCM, kinaweza kuwapunguzia imani
wapiga kura kwa umoja huo. Kadhalika, taarifa kuwa tayari viongozi wanauounda umoja huo
walishaafikiana kuwa mgombea wao awe Dkt Slaa, lakini wakabadili baada ya ujio wa Lowaasa
kinaweza kujenga picha kuwa vyama hivyo havina uwezo wao binafsi bali kutegemea makombo
ya CCM. Na kimsingi, CCM imekuwa ikitumia hoja hiyo majukwaani kuwakejeli wanachama
wake wa zamani waliohamia UKAWA, hususan Lowassa na Sumaye, kuwa ni makombo yenye
uroho wa madaraka.

Uamuzi wa kumtelekeza Dkt Slaa, mwanasiasa mwenye msimamo usioyumba na mwenye uwezo
mkubwa wa kujenga hoja na kueleweka, na ambaye alitoa mchango mkubwa kwa Chadema
kumudu kufika ilipo leo, haukuwa jambo la kiungwana. Lakini Kibaya zaidi ni jinsi viongozi na
wafuasi wa UKAWA walivyomdhalilisha Dkt Slaa mara baada ya kueleza kwanini aliamua
kujiweka kando. Hoja zake zilikuwa na msingi, hususan katika kipengele cha Lowassa kushindwa
kutekeleza ahadi kadhaa alizowapatia UKAWA kabla hajajiunga nao, kwa mfano lundo la
viongozi wa CCM waliotarajiwa kumfuata katika umoja huo.

Kadhalika, uhusika wa Askofu Gwajima katika suala zima la Lowassa kujiunga na UKAWA,
ukaribu katika ya mtumishi huyo wa Mungu na mwanasiasa huyo, na matamshi yake dhidi ya Dkt
Slaa, vyote vyaweza kuwa na madhara kwa UKAWA japo ni vigumu kutambua kwa kiasi gani.
Ukweli kwamba idadi kubwa ya wanachama wa CUF ni Waislamu, waweza kupelekea baadhi yao
kuutafsiri urafiki wa Lowassa na Gwajima kama mkakati wa kanisa kuingiza mtu wake Ikulu,
na japo Magufuli ni Mkristo pia, lakini kwa kiasi kikubwa chama chake kinaonekana miongoni
mwa wengi kuwa kisichokumbatia udini.

Wakati kampeni zikiendelea, zilipatikana video zilizowaonyesha Lowassa na Gwajima wakihubiri


kile kinachoweza tu kuelezwa kuwa ni kuhubiri udini. Lowassa alionyeshwa akizungumza
kanisani akidai kuwa Tanzania haijawahi kupata rais Mlutheri, na kupelekea shutuma kali dhidi
89

yake, hoja ikiwa nchi yetu inahitaji rais mwadilifu bila kujali madhehebu yake. Kana kwamba hiyo
haitoshi, siku chache baadaye, kulijitokeza video inayoonyesha mahubiri ya Gwajima yaliyoeleza
ndoto zake kuona misikiti ikigeuka kuwa Sunday Schools, Yayumkinika kuhitimisha kuwa
uhusiano kati ya kiongozi huyo wa dini na mwanasiasa huyo ni liability na unaweza kuipoteza
UKAWA kura kadhaa.

Kwa upande mwingine, tofauti na CCM yenye mtandao mpana na uwezo mkubwa wa kifedha,
UKAWA haina mtandao mpana, na kwa kiasi kikubwa ipo maeneo ya mijini zaidi kuliko vijijini
ambako licha ya CCM kuwa na ufuasi mkubwa katika maeneo hayo, ndiko kwenye wapigakura
wengi.

Kadhalika, ukweli kwamba katika maeneo mengi ya vijijini ni vigumu kutenganisha utumishi wa
umma na ufuasi kwa chama tawala. Ni rahisi kwa mtumishi wa umma kuipigia kura CCM akidhani
anafanya hivyo kwa maslahi yake kiajira kuliko kuhatarisha ajira yake kwa kukipigia kura chama
cha upinzani. Hili ni suala ambalo vyama vya upinzani vinapaswa kuwekeza nguvu nyingi huko
mbeleni ili kuliondoa.

Wakati CCM ikijinadi kwa uzoefu wake wa muda mrefu, UKAWA ina mtihani wa kuwaaminisha
wananchi kuwa inaweza kufanya vema zaidi ya chama hicho tawala. Tatizo ni kwamba, UKAWA
haijawahi kujaribiwa katika uongozi wa nchi. Katika mazingira ya kawaida, mpigakura
akikabiliwa na uchaguzi katik ya chama chenye uzoefu na kingine kisicho na uzoefu, uwezekano
mkubwa ni kukipigia kura chenye uzoefu.

Tatizo jingine linaloweza kuiathiri UKAWA ni uwezekano wa kuwepo mamluki wa CCM


mingoni mwa wahamiaji wapya walimfuata Lowassa baada ya kuhama chama hicho tawala. Sio
siri kuwa CCM haiitakii mema UKAWA, na kama ina uwezo wa kujaza mamluki wake kwenye
umaja huo, haitosita kufanya hivyo. Na kwa bahati nzuri kwa CCM, umoja huo wa wapinzani
umewapatia fursa ya bure kwa kupokea wana-CCM lukuki waliomfuata Lowassa. Hadi wakati
ninaandika kitabu hiki, bado kuna hisia kuwa baadhi ya wana-CCM hao (ikiwa ni pamoja na
Lowassa mwenyewe na hata Sumaye) wanaweza kuitosa UKAWA siku chache kabla ya
uchaguzi, na kuitengenezea CCM mazingira mazuri ya ushindi.
90

Vilevile, ujio wa wana-CCM hao unaweza kuwa na athari kwa UKAWA hasa katika maeneo
ambapo wanachama waliotoka mbali na vyama hivyo wamejikuta wakipoteza umuhimu kwa
wanachama wapya waliokuja na Lowassa. Mara baada ya umoja huo kutangaza majina ya
wagombea wake katika nafasi za ubunge na udiwani, kulijitokeza malalamiko katika maeneo
kudhaa kupinga kitendo cha umoja huo kupitisha wagombea wapya badala ya wanachama asili
wa vyama hivyo.

Japo ni hoja inayoweza kutokuwa na uzito mkubwa lakini ukweli kwamba Lowassa ni Mlutheri
kutoka Kanda ya Kaskazini kama ilivyo kwa Mbowe na Sumaye, unaweza kutumiwa na CCM
kujenga picha kuwa urais wa Lowassa ni wa ukanda na udini, hasa kwa kuzingatia athari
zinazoweza kutokana na kujiingiza kwa Askofu Gwajima katika mchakato wa Lowassa kujiunga
na Chadema na baadaye kuwa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA. Ukichanganya tatizo hilo
na tuhuma za Uislamu na Upemba dhidi ya CUF, yayumkika kuhisi kuwa CCM inaweza kuwa
na risasi za kutosha dhidi ya UKAWA.

Kama ilivyoelezwa awali, ujio wa Lowassa ndani ya UKAWA umejenga picha ya chama cha
mtu-mmoja tofauti na ugombea wa Magufuli ambao unaoonekana kwa kiasi kikubwa ni
ugombea wa kuwakilisha chama. Hadi muda huu, kampeni za uchaguzi huu zimechukua
mwelekeo wa CCM+Magufuli vs Lowassa, badala ya kuwa CCM+Magufuli vs
UKAWA+Lowassa. Kimsingi suala la ugombea urais wa Magufuli linaonekana kama ni CCM na
mgombea wake ilhali kwa upande wa UKAWA suala hilo linatoa taswira ya urais wa Lowassa.

Hata hivyo, hali hiyo inaweza kuwa inachangiwa na ukweli kwamba licha ya Lowassa kugombea
kwa tiketi ya UKAWA, kimsingi ni mwanachama wa Chadema, chama ambacho ni sehemu ya
ushirikiano wa vyama vinne, ilhali Magufuli ni mgombea wa chama kimoja tu, yaani CCM.

Kuhusu ajenda ya mabadiliko, sio tu kwamba ipo jumlajumla (vague) sana lakini uwasilishwaji
wake kwa umma umeambatana na upungufu mmoja mkubwa: hotuba za Lowassa kwenye
mikutano zimekuwa fupi mno. Haiyumkiniki kwa mgombea anayejaza maelfu kwa maelfu ya watu
kwenye mikutano yake akaishia kuongea kwa dakika chache tu. Sawa, hotuba ndefu sio ishara ya
91

uongozi bora lakini kampeni za uchaguzi ni fursa nzuri kwa vyama na wagombea wake kuelezea
kwa undani kuhusu ilani za vyama zao.

Hadi muda huu, ajenda ya mabadiliko inaonekana kuwa na lengo moja tu; kuingoa CCM. Lakini
japo kuiondoa CCM madarakani ni mabadiliko, lakini mabadiliko yenye manufaa kwa Watanzania
hayawezi kuishia kwa kukibadili chama pekee. Kwa kiasi kikubwa Lowassa ana viongozi wenzie
wa UKAWA wamekuwa wakisema tu tutafanya hili au lile bila kuingiza kwa undani kuwa
wataweza vipi kufanya hivyo.

Umuhimu wa hotuba zenye maelezo ya kutosha kuhusu sera za umoja huo unasababishwa na
ukweli kwamba idadi kubwa tu ya Watanzania sio wanachama wa chama chochote cha siasa.
Wakati takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa CCM ina wanachama takriban milioni nane,
idadi ya wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA haifahamiki vizuri. Kuna uwezekano
mkubwa kuwa miongoni mwa Watanzania waliojiandikisha kupiga kura, idadi ya wananchi wasio
wanachama wa vyama vya siasa ni kubwa zaidi ya walio na vyama. Kimsingi, ni kundi hili ndilo
linalotarajiwa kuamua ushindi kwa chama au mgombea. Kutokana na hali hiyo, ni muhimu mno
kwa kundi hili kushawishiwa vya kutosha kwa kuelezwa mipango tarajiawa ya Lowassa na
UKAWA kwa ujumla endapo watapatiwa ridhaa ya kuchaguliwa.

Ukweli kwamba Lowassa alijiunga na UKAWA miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi mkuu unaweza
kuwa na athari za kimaandalizi kwa muungano huo. Japo ujio huo unaoonekana kuongeza nguvu
na mvuto kwa UKAWA lakini hali inaweza kuwa tofauti katika maeneo ya vijijini ambayo baadhi
yao yanaweza kuwa na wananchi wasioelewa lolote kuhusu umoja huo wala mgombea wake.

Sambamba na hilo ni ukweli kwamba baadhi ya vyama vinavyounda umoja huo, hususan
Chadema, vilitumia muda mwingi kumchafua Lowassa alipokuwa CCM, na inahitajika kazi ya
ziada kumsafisha ndani ya miezi mitatu mtu aliyechafuliwa kwa mtakriban miaka tisa. Na hata
kama muda ungekuwa unatosha, jitihada za kumsafisha Lowassa zina uwezekano mkubwa tu wa
kuiumiza Chadema, na UKAWA kwa ujumla kuliko kuisaidia, kwani linagusa suala muhimu la
chama kuaminika machoni mwa wapigakura.
92

Japo hazina ushawishi wa kutosha, kuna hisia kwamba uamuzi wa Lowassa kujiunga na Chadema,
na hatimaye kupewa fursa ya kugombea urais, ni mkakati wa mwanasiasa huyo, kwa upande
mmoja, kulipa kisasi dhidi ya wanasiasa hususan wa Chadema waliotumia muda mwingi
kumchafua kwa kumwita fisadi, na kwa upande mwingine, ni fursa dhidi ya Kikwete, aliyemtosa
katika jaribio lake la kuwania urais kupitia CCM. Hisia hizo zinadai kuwa yawezekana Lowassa
anafarijika kuona watu walewale waliotumia miaka kibao kumchafua, kama vile Mbowe na Lissu,
sasa wanapata huku na kule kumsafisha. Kadhalika, inadaiwa kuwa, kwa kuwa mgombea wa
chama cha upinzani, Lowassa amepata fursa adimu ya kulipa kisasi kwa Kikwete, ambapo
anaweza kutumia kampeni zake kumshambulia rafiki yake huyo wa zamani waziwazi. Katika
hilo, inadaiwa kuwa Lowassa hana cha kupoteza, kwani hata akishindwa katika uchaguzi huu
anaweza kustaafu siasa na kuendelea na maisha yake bila hofu ya kutimuliwa uongozi, tishio
linalowakabili baadhi ya viongozi wa UKAWA pindi chama hicho kikishindwa kwenye uchaguzi
huo.

Hisia hizo zinaweza kupata uzito katika jinsi Lowassa anavyotumia muda mfupi kujinadi na
kuwanadi wagombea ubunge wa UKAWA.Licha ya kutoa ahadi zinazoonekana kuwavutia
wanaohudhuria mikutano yake, kwa kiasi fulani mwanasiasa huyo haonekani kama ana hofu ya
uwezekano wa kushindwa au ana mori wa kushinda. Pengine ni kujiamini sana lakini pia
pengine ni dalili kuwa hana cha kupoteza akishindwa.

Pengine kikwazo kikubwa zaidi kwa UKAWA kuweza kuishinda CCM ni mfumo kuwa dhidi
yao. Mfumo huu ndio uleule uliokuwa ukilalamikiwa miaka nenda miaka rudi na vyama vya
upinzani takriba kwenye kila uchaguzi. Umoja huo unashiriki uchaguzi unaosimamiwa na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi ileile ambayo Wapinzani wamekuwa wakiishutumu kwa kuipendelea
CCM. Taasisi mbalimbali za serikali zinazohusika na uchaguzi huo zipo Vilevile kama
ilivyokuwa huko nyuma ambapo zilishutumiwa na Wapinzani kuwa zinaipendelea CCM. Kama
tukiamini shutuma hizo za Wapinzani huko nyuma, iweje basi mwaka huu watarajie matokeo
tofauti? Ndio, ujio wa Lowassa umeleta hamasa kwa umoja huo wa vyama hivyo lakini kimsingi
haujabadili mazingira ya uchaguzi huu kulinganisha na chaguzi zilizotangulia, mabazo takriba zote
ziliishia kwa Wapinzani kuzilaumu kuwa hazikuwa huru na haki.
93

Kwa hitimisho, uchaguzi huu unahusisha pia vyama vingine ambavyo ushiriki wake haujajadiliwa
katika kitabu hiki. Vyama hivyo ni pamoja na ACT- Wazalendo, ADC, CHAUMMA, TLP, NRA
na UPDP. Kati ya hivyo, ACT-Wazalendo ndicho kinaonekana kuwa na maandalizi mazuri zaidi,
ambapo licha ya kusimamisha mgombea katika nafasi ya urais, pia kimesimamisha idadi kubwa
ya wagombea ubunge na udiwani. Haitarajiwi kuwa chama hicho kitatoa upinzani mkali kwa CCM
au UKAWA, lakini yatarajiwa kwamba matokeo mabaya kwa UKAWA yanaweza kupelekea
chama hicho kujitokeza kuwa chama kikuu cha upinzani, endapo matokeo hayo mabaya
yatapelekea vyama vilivyounda UKAWA kuingiza kwenye migogoro.

Sababu kuu ya kitabu hiki kutovijadili vyama hivyo na wagombea wake ni ukweli kwamba kwa
kasi kikubwa kabisa, ushindani mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni kati ya CCM na
UKAWA, na wagombea wao, Magufuli na Lowassa. Hata hivyo, kwa kuwa kitabu hiki
kinatarajiwa kuwa na mwendelezo baada ya uchaguzi huo, inatarajiwa kuwa mwenendo wa vyama
hivyo sita, pamoja na CCM na kila chama kinachounda UKAWA, utajadiliwa katika chapisho
lijalo.

Mwisho, sura hii imechambua kwa kina nafasi na vikwazo kwa CCM na UKAWA, na wagombea
wao, Magufuli na Lowassa, uchambuzi unaojenga msingi wa hitimisho la kitabu hiki katika sura
ijayo ambapo jaribio lisilo la moja kwa moja (indirectly) litafanyika kubashiri mgombea/chama
gani ataibuka na ushindi.
94

SURA YA SITA: Hitimisho

Sura hii fupi inahitimisha kitabu hiki ambacho kimejadili kwa undani kuhusu pande mbili zenye
ushindani mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yaani chama tawala CCM, na umoja wa
vyama vinne vya upinzani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD unaojulikana kama
UKAWA, pamoja na wagombea wao, John Magufuli kwa upande wa CCM na Edward Lowassa
wa UKAWA.

Kadri tarehe ya uchaguzi mkuu inavyozidi kukaribia, ndivyo shauku ya Watanzania kufahamu
mgombea gani ataibuka mshindi katika kiti cha urais, sambamba na kujua chama gani kitaibuka
mshindi kwenye ubunge na udiwani. Moja ya nyenzo muhimu za kubaishiri matokeo ya uchaguzi
kabla hata haujafanyika ni kwa kutumia utafiti wa kura za maoni. Japo kura za matokeo ya utafiti
wa kura za maoni sio uhakika wa asilimia 100 kuhusu matokeo ya uchaguzi husika, kwa kiwango
kikubwa hutoa mwelekezo wa mapendezeo ya wapiga kura kwa vyama na wagombea wake.

Hata hivyo, utafiti wa kura za maoni ni utaratibu mgeni katika siasa za vyama vingi nchini
Tanzania ambazo mwaka huu zinatimiza miaka 23. Wakati wa mfumo wa chama kimoja sio tu
hakukuwa na utaratibu wa utafiti wa kura za maoni bali pia hakukuwa na haja hiyo kutokana na
uwepo wa chama kimoja na mgombea mmoja tu. Kama ilivyoelezwa huko nyuma, uchaguzi mkuu
katika nafasi ya urais ilikuwa ni kama kumpitisha tu mgombea aliyepitishwa na chama kwani hata
kwenye karatasi ya kura kulikuwa na picha ya mgombea na mmoja dhidi ya kivuli.

Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, taratibu tafiti za kura za maoni zilianza
kujichomoza, lakini zilikabiliwa na upinzani mkali kwa madai ya kukibeba chama tawala. Iwapo
madai hayo yalikuwa na ukweli au la, suala lililojitokeza wazi ni kuwa wananchi wengi
hawakutilia maanani matokeo ya tafiti hizo, pengine kutokana na hisia za upendeleo kwa chama
tawala au ugeni tu wa utaratibu huo.

Hadi wakati ninaandika kitabu hiki, tayari kumefanyika tafiti tatu za kura za maoni. Katika tafiti
hizo, ya taasisi za Twaweza, IPSOS (Synovate) na TADIP, mbili zilionyesha CCM na mgombea
wake anaongoza kwa mbali huku tafiti ya tatu ikionyesha mgombea wa UKAWA akiongoza.
95

Katika utafiti wa kura za maoni wa Twaweza, Magufuli aliongoza kwa asilimia 65 ilhali Lowassa
akipata asilimia 25, na katika utafiti wa IPSOS (Synovate) Magufuli alipata asilimia 62 na Lowassa
asilimia 31, huku utafiti wa kura za maoni wa taasisi ya TADIP ukionyesha Lowassa akipata
asilimia 54 dhidi ya asilimia 40 kwa Magufuli.

Tafiti zote hizo za kura za maoni zilishutumiwa vikali, huku mbili zilizoonyesha Magufuli
akiongoza zikituhumiwa kuwa zilipikwa na CCM,ilhali ule ulioonyesha Lowassa anaongoza
ukilaumiwa kwa madai kuwa taasisi iliyofanywa utafiti huo inamilikiwa na Chadema.

Eneo moja ambalo wananchi wengi walionekana kuwa na mwafaka ni hoja kwamba kura pekee
za kuaminika ni zitakazopigwa siku ya uchaguzi mkuu, kwani sio za makadirio au za uwakilishi.
Kwahiyo, licha ya taasisi hiska kufanya jitihada kutetea matokeo ya tafiti zao hizo, yayumkinika
kuhitimisha kuwa ni wananchi wachache tu walioyapa matokeo hayo umuhimu stahili.

Kwa mujibu wa takwimu, takriban Watanzania milioni 24 wamejiandikisha kupiga kura katika
uchaguzi huo. Kwa kuzingatia kwamba idadi kubwa ya wapigakura hao sio wanachama wa chama
chochote cha siasa, yayumkinika kuhitimisha kuwa ushindi kwa Magufuli na CCM au Lowassa
na UKAWA utaamuliwa na kundi hilo. Kimahesabu, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi
ya jumla ya wanachama wa CCM ni milioni 8 hivi, ambao ni sawa na takriban asilimia 33 ya jumla
ya Watanzania takriban milioni 24 waliojiandikisha kupiga kura. Kwa makadirio, idadi ya jumla
ya wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA ni pungufu ya hao wa CCM, na hiyo inaweza
kufanya kundi la wapigakura wasiofungamana na chama chochote kuwa zaidi ya asilimia 50.

Kinacholipa uzito zaidi kundi hilo la wapigakura wasiofungamana na upande wowote ni ukweli
kwamba linaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza ndani ya CCM na
UKAWA kabla ya uchaguzi. Kwa upande wa CCM, kuondoka kwa Lowassa kunaweza kuwafanya
baadhi ya wana-CCM kutoiunga mkono CCM lakini bila kuchukua uanachama huko UKAWA.
Hawa wanaweza kuingiza katika kundi hilo la wasioungamana na chama chochote, licha ya
kuendelea kuwa wana-CCM.

Kwa upande wa UKAWA, yayumkinika kuhisi kuwa kuna baadhi ya wanachama wa vyama
vinavyounda umoja huo ambao sio tu hawajaridhishwa na suala la ushirikiano wa vyama hivyo,
96

lakini pia wale ambao wamechukizwa na ujio wa Lowassa, au kukerwa na sababu zilizopelekea
Prof Lipumba na Dkt Slaa kujiengua katika uongozi. Katika hawa, kuna wanaoweza kuamua
kujiunga na CCM, lakini uwezekano mkubwa ni wengi kubaki wanachama wa vyama hivyo lakini
wasiounga mkono ugombea wa Lowassa. Kwahiyo nao wanaweza kuingizwa katika kundi la
wasiofungamana na chama chochote, licha ya kuendelea kuwa wananchama katika vyama vyao.

Hadi kufikia hatua hii ya kuhitimisha kitabu hiki, mimi kama mwandishi nimesimami kwenye
kufanya uchambuzi bila kuelemea upande wowote. Nimejitahidi kuelezea mapungufu ya pande
zote mbili, sambamba na fursa walizonazo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Nimefanya
hivyo kwa sababu lengo la kitabu hiki sio kufanya simulizi tu, au kukampenia chama au mgombea
fulani bali kuweka kumbukumbu sawia, pamoja na kumsaidia msomaji kufanya maamuzi sahihi
wakati wa kupiga kura.

Na uamuzi wa kuvizungumzia vyama viwili tu, yaani CCM na UKAWA (kama muungano wa
vyama) ni kwa sababu kwa Vyovyote itakavyokuwa, rais ajaye atakuwa aidha Magufuli au
Lowassa, huku chama kitakachoshinda kwa jumla kitakuwa aidha CCM au UKAWA katika umoja
wao. Kwahiyo hatma ya nchi yenu ipo mikononi mwa Magufuli na CCM yake na Lowassa na
UKAWA yake.

Hata hivyo, na bila kupendelea upande wowote, mazingira yaliyopo yaipa nafasi kubwa CCM na
mgombea wake kuibuka mshindi katika uchaguzi huo. Nimeelezea sababu kadhaa zinazoweza
kuisadia CCM na Magufuli kushinda, katika sura iliyotangulia. Na nimefanya hivyo pia kwa
UKAWA na Lowassa. Ukilinganisha fursa na vikwazo kwa kila upande hutopata shinda kuelezwa
kwanini nafikia hitimisho hilo.

Ushindi kwa Magufuli na CCM unaweza kutokana zaidi na ninachoita sababu za kimfumo,
kwamba mfumo uliopo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi unamtengenezea mazingira
mazuri mgombea huyo na chama chake, ilhali ushindi kwa Lowassa na UKAWA unategemea zaidi
mapungufu ya CCM, sio tu katika kujinadi bali pia kupata mwanya wa kuwashawishi wapigakura
wengi zaidi katika kundi muhimu la wasiofungamana na chama chochote, ambalo kama
nilivyotanabaisha awali, ndilo litakaloamua mshindi katika uchaguzi huu.
97

Tukiamini kuwa wapigakura wasiofungamana na chama chochote ndio watakaoamua mshindi,


yayumkinika kuhisi kuwa ni rahisi zaidi kwao kumwamini Magufuli kutokana na rekodi yake,
kuliko Lowassa. Kwa kuwalinganisha wagombea hao wawili, Magufuli anaweza kutembea kifua
mbele kuonyesha mafanikio ya utendaji kazi wake, kubwa zaidi likiwa kumudu kutumikia awamu
mbili tofauti kwa ufanisi mkubwa. Hali ni tofauti kwa Lowassa, kwa sababu vyovyote ilivyo,
tuhuma dhidi yake kuhusu kashfa ya Richmond ni vigumu kufutika. Na tofauti na Magufuli,
Lowassa alilazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu kutokana na kashfa hiyo.

Kibaya zaidi, wakati Magufuli anaungwa mkono na takriba wana-CCM wote, tukiweka kando
ambao wanaweza kuwa wamejiweka kando kutokana na jina la Lowassa kukatwa na vikao vya
mchujo vya chama hicho, na baadaye kukihama chama hicho tawala, Lowassa hata kama
anaungwa mkono na asilimia kubwa ya wana-UKAWA, wengi wa hao wanaomuunga mkono
walitumia muda mrefu huko nyuma kumchafua.

Hoja hapa ni kwamba, wakati wanaomuunga mkono Magufuli ni watu waliomuunga mkono muda
wote, kwa maana ya ufuasi wao kwa CCM, kwa upande wa Lowassa, wengi wa wanaomuunga
mkono ni watu wapya, ambao huko nyuma walifanya kila jitihada kumchafua. Ni rahisi kwa
kundi la wapigakura wasiofungamana na chama chochote kushawishiwa na waliomuunga
mkono Magufuli tangu mwanzo kuliko hao wanaomuunga mkono Lowassa sasa lakini huko
nyuma walimbomoa.

Kimsingi, CCM haihitaji kuwashawishi wanachama wake kumuunga mkono Magufuli, kwa
sababu ni mwenzao. Kwa upande wa Lowassa, sio tu zinahitajika jitihada za kuwashawishi
baadhi ya wana-UKAWA kuwa actually tulikosea kumwita huyu mtu fisadi, lakini pia
kuwaaminisha kuwa atasimama nao hadi dakika ya mwisho, kwa kuzxingatia hofu niliyoeleza
katika sura iliyopita kwamba landa Lowassa ametumwa na CCM ili kuuwa upinzani.

Ndio, ni rahisi kwa UKAWA kudai kuwa fisadi pekee hakuwa Lowassa tu, na ufisadi CCM
haukuwa Richmond pekee, lakini kwa upande mwingine, ukiangalia watu wanaotajwa kuwa
karibu na Lowassa na wale walio karibu na Magufuli, mpigakura asiyefungamana na chama
chochote anaweza kushawishika kirahisi kumchagua Magufuli kuliko Lowassa, kwa sababu
98

wengi wa waliomzunguka Lowassa, waliomfuata kutoka CCM na baadhi ya wanaotajwa


kumuunga mkono bila kujitangaza hadharani, ni watu wenye rekodi zisizopendeza. Hili linaweza
kujenga hofu kwamba, laiti mgombea huyo wa UKAWA akishindwa, anaweza kuwawekea kando
wenye vyama vyao, na kuwateua maswahiba zake wanaotajwa kumsaidia katika kampeni zake.

Tukija kwenye suala la mgombea gani kati ya Lowassa na Magufuli mwenye nafasi ya kuleta
mabadiliko halisi ndani ya chama chake na kwa taifa kwa ujumla, pengine ni rahisi kwa Magufuli
angalau kuahidi hilo kwa sababu kimsingi tatizo la CCM ni ukosefu tu wa nia ya kufanya
mabadiliko kusudiwa, kwani uwezo na sababu zipo. Kwa upande wa Lowassa, hiyo tu kuamini
kwamba kuwa hivi sasa yeye ni mtu tofauti na yule aliyekuwa CCM ni mtihani tosha.

Lakini kingine, kushindwa kwa Lowassa kuelezea kwa undani kuhusu ajenda yake ya mabadiliko
kunaweza kutafsiriwa kirahisi kuwa ni yeye mwenyewe haamini katika mabadiliko anayohubiri.
Kimsingi, mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania, hususan wafuasi wa UKAWA, sio jambo
jepesi kama linavyozungumzwa majukwaani.

Ingekuwa sio jambo la faida kwa wapigakura na Watanzania kwa ujumla pekee bali lingeweza
kumsaidia Lowassa na UKAWA endapo dhana hiyo ya mabadiliko ingefafanuliwa kwa upana
zaidi. Kwa mfano, mgombea huyo angeweza kueleza kuhusu ratiba ya mabadiliko hayo,
sambamba na kutanabaisha ni maeneo yapi yatakayoanza kushughulikiwa. Orodha ya maeneo
yanayopaswa kukumbwa na mabadiliko hayo ni ndefu, na pasipo mipango ya kueleweka, basi hata
Lowassa akishindwa katika uchaguzi huu, anaweza kumaliza vipindi viwili vya urais pasipo
kutimiza ahadi ya kuleta mabadiliko.

Kulikuwa na haja kwa Lowassa na UKAWA kwa ujumla kujifunza kutoka katika ahadi ya
Kikwete wakati wa kampenzi zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambapo alitoa
ahadi ya jumla jumla ya Masiha Bora kwa Kila Mtanzania. Japo maisha bora ni rahisi
kuchanganuliwa kuliko mabadiliko, kwa kiasi kikubwa Kikwete anamaliza mihula yake muiwli
huku wananchi wengi wakidhani ahadi hiyo ya maisha bora ilikuwa hadaa tu. Hata hivyo, tatizo
linaloifanya ahadi hiyo kutoonekana kama imetekelezwa ni kutokana na ujumla jumla wake.
99

Kwa kuhubiri mabadiliko pasipo kuelezea kwa undani, kuna uwezekano kwa urais wa Lowassa
kukumbwa na matatizo mapema kutoka kwa wananchi watakaokuwa wakitarajia, kwa mfano,
mara baada ya mwanasiasa huyo kuingiza Ikulu, kila mwananchi ataweza kujimudu kiuchumi,
ajira zitapatikana mara moja kwa wasio na ajira, ada zilizoahidiwa kufutwa katika taasisi za elimu
zitafutwa mara moja, na matarajio mengine lukuki. Si kwamba wazo la mabadiliko ni baya au
lisilohitajika. Ni wazo zuri lakini sio tu linastahili kutolewa maelezo ya kina bali pia linahitaji
mipango makini ili kuweza kutekelezwa.

Lakini wakati pengine ingekuwa rahisi kwa Lowassa kueleza kuhusu ajenda ya mabadiliko kwa
upande wa kiutawala au sera, kikwazo kinaweza kuwa upande wa mabadiliko kijamii. Kwa mfano,
mwanasiasa huyo ana mkakati gani utakaoweza kubadili kasumba iliyoota mizizi katika nchi yetu
ya kuwapa wahalifu heshima wasiyostahili? Ni jambo la kawaida katika maeneo mengi ya
Tanzania yetu kuona muuza madawa ya kulevya akitukuzwa na kupewa wadhifa wa mzungu
wa unga badala ya kuitwa mhalifu. Kadhalika, imezoeleka kuona wabadhirifu makazini
wakipewa wadhifa wa mapedejee.

Miaka kadhaa wakati nikiwa mtumishi wa umma, nilishuhudia kijana mmoja aliyemaliza kozi ya
uhasibu na kupangiwa kitengo cha fedha kazini, akichekwa kwa kuishi kama sio mhasibu. Kwa
muda mrefu kijana huyo alikuwa akitumia usafiri wa wafanyakazi wote kwa vile hakuwa na usafiri
binafsi, kwa sababu mshahara wake ulikuwa haumruhusu, kama ambavyo likuwa akiishi nyumba
ya kupinga kwa vile hakuwa na uwezo kifedha kujenga au kununua nyumba. Kijana huyo
aliandamwa kwa muda mrefu mpaka, ghafla, alipoanza kusikia lawama dhidi yake na kuanza
kununua magari kadhaa ya thamani, sambamba na ujenzi wa mahekalu.

Licha ya tabia hizo, kuna masuala yanayopewa uzito mkubwa katika jamii ilhali yale ya muhimu
yakipuuzwa. Kwa mfano, watu wapo tayari kuchangia mamilioni ya shilingi kama michango ya
harusi lakini wanashindwa kuchangiana ada za watoto wao mashuleni. Laiti ushirikiano
unaoonyeshwa kwenye klabu za starehe, kile wenyewe wanaita kuzungusha raundi za kinywaji
ungehamishiwa kwenye ushirika kwenye miradi ya maendeleo, basi pengine mabadiliko
yanayohubiriwa na Lowassa yangekuwa yameanza kitambo.
100

Kuna tatizo la vijana wengi kutafuta njia za mkato za mafanikio, hali inayowavutia matapeli
kubuni miradi mbalimbali ya kula fedha za bure. Ni watu wangapi waliopoteza fedha zao katika
miradi ya kitapeli kama vile Dollar Jet, DECI, na mingineyo?

Licha ya miradi ya kitapeli wa utajiri wa chapu chapu, kuna imani katika vitu visivyo na
mwelekeo kama ilivyokuwa katika suala la kikombe cha babu, mtumishi wa Kanisa huko
Samunge, mkoani Arusha aliyeahidi tiba ya magonjwa mbalimbali, na kupelekea maelfu kwa
maelfu ya Watanzania kujazana huko. Hadi leo idadi ya waliopoteza maisha kwa kuamini tiba ya
kikombe cha babu haijawekwa hadharani lakini yayumkinika kuhisi kuwa ni kubwa.

Kuna tatizo kubwa la imani za ushirikina ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza
duniani kwa imani hiyo. Je mabadiliko ya kisera yanaweza kuwafanya waamini wa ushirikian
wabadilike? Licha ya ushirikina, kuna vijana lukuki wanaoamini kuwa njia ya mkato ya mafanikio
ni kujiunga na kikundi cha Freemasons, huku takriban kila kijana anyejituma na kufanikiwa
kimaisha akihisiwa kuwa mfuasi wa kundi hilo. Kibaya zaidi, imefika mahala baadhi ya vijana
kujizushia kuwa wao ni freemasons ili waonekane kuwa wanakaribia kupata utajiri punde.

Kama kuna eneo linalohitaji mabadiliko ya haraka ni katika suala la rushwa. Utafiti mmoja
uliofanyika mkoani Arusha ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya waliohojiwa waliamini kuwa
rushwa ilikuwepo, ipo na itaendela kuwepo milele. Sawa, rushwa imekuwepo kitambo na
itaendelea kuwepo kitambo lakini si kwa kiwango kilichopo hivi sasa nchini. Na uwepo wake wa
muda mrefu haumaanishi wananchi wakubaliane nayo, kwani hata maradhi kama malaria na
ukimwi yamekuwapo kitambo lakini bado twaendeleza jitihada za kupambana nayo.

Kwahiyo, ajenda ya Lowassa kuhusu mabadiliko, licha ya uzuri wake, licha ya kuwa na
mkanganyiko mkubwa, haijapatiwa maelezo ya kutosha. Na ni katika mazingira haya,
wanaomlaumu Lowassa kuhusu hotuba zake za dakika chache wanapata uzito katika lawama
hizo kwa sababu kuna masuala kadhaa yanayohitaji kuelezwa kwa kirefu, kubwa likiwa ni hilo la
ajenda ya mabadiliko.

Kwa kuhitimisha kitabu hiki, wakati ni vigumu kufanya ubashiri wa uhakika kuwa nani kati ya
Magufuli na Lowassa ataibuka mshindi, mazingira yaliyopo yanaashiria kuwa mgombea huyo wa
101

CCM na chama chake wana nafasi kubwa ya kushinda. Ni kweli kwamba kuna idadi kubwa ya
wananchi waliochoshwa na CCM lakini kuchoshwa pekee hakutoshi kukiondoa chama
madarakani. Kama alivyosema Dkt Slaa wakati anatoa maelezo kuhusu kujitenga kwake na
Chadema, mabadiliko ya kweli yanahitaji mikakati makini ya watu makini.

Jingine ambalo linapaswa kugusiwa katika Hitimisho hili ni hatma ya UKAWA iwapo mgombea
wao, Lowassa hatoshinda. Ukiondoa CUF, ambayo kwa kiasi kikubwa haijaathiriwa na uamuzi
wa kujiunga na umoja huo, tukiweka kando kujiuzulu kwa Prof Lipumba, viongozi wakuu wa
Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD wanaweza kuwa katika nafasi ngumu ya kuendelea
kuviongoza vyama hivyo, hasa kwa kuzingatia uwezekano wa kuelekezewa lawama na
wanachama wao kuhusu kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wao wa urais.

Mwisho, uchaguzi huu mkuu si kwa ajili ya Magufuli au Lowassa, CCM au UKAWA, bali
Watanzania wote. Kumekuwa na tatizo la muda mrefu la utegemezi kwa wanasiasa kiasi kwamba
wananchi wamekuwa wakitarajia miujiza kwa wananchi wenzao walioingia kwenye siasa, iwe
kwa minajili ya kuwaongoza wenzao au ulaji tu. Iifke mahala Watanzania watambue kuwa japo
tunahitaji wanasiasa kutuwakilisha na kutongoza, wananchi wana nafasi kubwa ya kujiongoza
wenyewe katika dhana maarufu katika nchi zilizoendelea ya uraia kama uongozi wa kijamii.
Lakini ili nasi tufike huko tunalazimika kuanza kutilia uzito haja ya kujitolea (volunteering),
kutotegemea malipo kwa kila tunalofanya na kuweka mbele maslahi ya jamii na nchi kwa ujumla
badala ya maslahi binafsi.

Ni muhimu kutambua kuwa mabadiliko yaliyotokea sehemu mbalimbali dunia yalichukua muda
mrefu, lakini kwa vile wahusika hawakuwa wakifikiria maslahi au mahitaji ya wakati huo tu bali
ya muda mrefu na ya vizazi vijavyo, matokeo yake ndio haya tunavyoshuhudia leo.

Lakini kwa tahadhari tu, licha ya hitimisho la kitabu hiki kuonyesha kuwa Magufuli na CCM wana
nafasi kubwa zaidi ya ushindi kuliko Lowassa na UKAWA, funzo moja kuhusu siasa, na hasa
katika chaguzi, ni kwamba mambo huweza kubadilika ghafla, au matokeo kuwa kinyume kabisa
na inavyotarajiwa. Kwa maana hiyo, tukiweka kando sababu mbalimbali zilizobainishwa katiks
102

kitabu hiki, yeyote kati ya Magufuli na LLowassa, na CCM na UKAWA ana weza kuibuka
mshindi, kwa kuzingatia 'kanuni isiyo rasmi' kuwa siasa haitabiriki.

Kwa upande wa uchaguzi huu mkuu, licha ya umuhimu mkubwa wa kuchagua viongozi bora,
ukweli ni kwamba kutakuwa na maishaha baada ya uchaguzi huo. Na Vyovyote itakavyokuwa,
kutakuwa na washindi na walioshindwa, na walioshindwa watalazimika kuongozwa na chama
ambacho hawakukipigia kura. Hiyo ndiyo demokrasia. Kwa mantiki hiyo, licha ya kutekeleza
jukumu la kidemokrasia la kuchagua wagombea tuwapendao, ni muhimu kukumbuka kuwa sote
ni Watanzania, na Vyovyote matokeo yatakavyokuwa, ni lazima tuendelee kubaki wamoja ili
kujenga taifa letu kwa amani na mshikamano.

Mungu ibariki Tanzania!

Das könnte Ihnen auch gefallen